DAFTARI LA MPIGA KURA KUBORESHWA KWA WAKAZI WA ARUSHA NA KILIMANJARO MWEZI DRSEMBA - MAIPAC MEDIA TANZANIA

Breaking

MAIPAC MEDIA TANZANIA

A Centre for Indigenous and Pastoralists Community Informations




Friday, 29 November 2024

DAFTARI LA MPIGA KURA KUBORESHWA KWA WAKAZI WA ARUSHA NA KILIMANJARO MWEZI DRSEMBA



Mwenyekiti wa Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC), Mhe.Jaji (Rufaa) Jacobs Mwambegele, akizungumza wakati akifungua mkutano wa siku moja wa Tume na Wadau wa Uchaguzi uliofanyika leo Novemba 29, 2024 mkoani Arusha ikiwa ni maandalizi ya Uboreshaji wa Daftari la Kudumu la Wapiga Kura ambao unataraji kuanza Disemba 11 hadi 17, 2024. Wadau hao ni pamoja na Viongozi wa vyama vya siasa, Viongozi wa Dini, Wawakilishi wa Asasi za Kiraia, Wahariri wa Vyombo vya habari, Waandishi wa habari, Maafisa Habari wa Mikoa na Halmashauri, Wawakilishi wa Makundi mbalimbali ya Vijana, Watu wenye ulemavu, Wanawake na Wazee wa Kimila. (Picha na INEC)





Na. Mwandishi Wetu, maipac


maipacarusha20@gmail.com

Uboreshaji wa Daftari la Kudumu la Wapiga Kura Mkoani Arusha na Kilimanjaro utafanyika kwa siku saba kuanzia tarehe 11 hadi 17 Desemba, 2024.


Akifungua mkutano wa wadau wa uchaguzi mkaoni Arusha leo tarehe 29 Novemba, 2024, Mwenyekiti wa Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi, Mhe. Jaji wa Rufaa, Jacobs Mwambegele amesema uboreshaji huo pia utajumuisha Mkoa wa Dodoma kwenye Halmashauri za Wilaya ya Kondoa, Chemba na Mji wa Kondoa ambapo vituo vitakuwa vinafunguliwa kuanzia saa 2:00 asubuhi na kufungwa saa 12:00 jioni.


Amesema mikoa hiyo inafanya uboreshaji wa Daftari ikiwa ni mwendelezo wa zoezi hilo ambalo lilizinduliwa tarehe 20 Julai, 2024 mkaoni Kigoma.


Akifungua mkutano kama huo mkoani Kilimanjaro, Makamu Mweneyekiti wa Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi, Mhe Jaji wa Rufaa (Mstaafu) Mbarouk Salim Mbarouk amesema zoezi hilo tayari limeshafanyika Kigoma, Tabora, Katavi, Geita, Kagera, Mwanza, Shinyanga, Mara, Simiyu, Manyara, Dodoma, Singida na Zanzibar.


Katika hatua nyingine Mkurugenzi wa Uchaguzi wa Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi, Bw. Kailima Ramadhan amesema Tume imeridhia kuongezeka kwa vituo 44 vya kupigia kura ambavyo vinafanya idadi ya vituo vya kupigia kura nchini kuwa 40,170 kutoka 40,126 vilivyokuwepo awali.

“Tume imeridhia kufanyika kwa mabadiliko ya idadi ya vituo vya kuandikisha wapiga kura kutoka vituo 40,126 hadi kufikia vituo 40,170 kwa kurejesha vituo 44 vya Kata 11 za Halmashauri ya Wilaya ya Ngorongoro. Vituo 39,753 vipo Tanzania Bara na 417 vipo Zanzibar,” amesema.




Hatua hiyo ya Tume imetokana na amri ya Waziri wa Nchi, mwenye dhamana ya TAMISEMI kupitia Tangazo la Serikali Na. 796 ya tarehe 06 Septemba, 2024 ambayo pamoja na mabadiliko mengine, imerejesha kata 11 za Halmashauri ya Wilaya ya Ngorongoro ambazo zilifutwa hapo awali.


Kailima amesema kwenye Mkoa wa Arusha Tume inatarajia kuandikisha wapiga kura wapya 224,499 ikiwa ni ongezeko la asilimia 18 ya wapiga kura 1,255,584 waliopo kwenye Daftari la Kudumu la Wapiga Kura.


Ameongeza kuwa Tume inatarajia baada ya uandikishaji Mkoa wa Arusha utakuwa na wapiga kura 1,480,083.


Amesema kwa Mkoa wa Arusha kuna vituo 1,454 vitakavyotumika kwenye uboreshaji kwa mwaka huu ikiwa ni ongezeko la vituo 86 katika vituo 1,368 vilivyotumika kwenye uboreshaji mwaka 2019/20.


Akiwasilisha nada mkoani Kilimanjaro, Mkurugenzi wa Huduma za Kisheria wa Tume, Bw. Selemani Mtibora amesema kwa mkoa wa Kilimanjaro Tume inatarajia kuandikisha wapiga kura wapya 180,540 ikiwa ni ongezeko la asilimia 18 ya wapiga kura 1,009,726 waliopo kwenye Daftari la Kudumu la Wapiga Kura.


“Tume inatarajia baada ya uandikishaji Mkoa wa Kilimanjaro utakuwa na wapiga kura 1,190,266,” amesema.

Ameongeza kuwa Mkoa wa Kilimanjaro una vituo 1,316 vitakavyotumika kwenye uboreshaji kwa mwaka huu ikiwa ni ongezeko la vituo 30 katika vituo 1,286 vilivyotumika kwenye uboreshaji mwaka 2019/20.


Mwisho.
.

No comments: