DK NCHIMBI AWATAKA WASOMI KUJITOKEZA KUPIGA KURA 📌RAIS SAMIA KUWA MGENI RASMI MAHAFALI MZUMBE - MAIPAC MEDIA TANZANIA

Breaking

MAIPAC MEDIA TANZANIA

A Centre for Indigenous and Pastoralists Community Informations




Saturday, 23 November 2024

DK NCHIMBI AWATAKA WASOMI KUJITOKEZA KUPIGA KURA 📌RAIS SAMIA KUWA MGENI RASMI MAHAFALI MZUMBE

 






Na: Lilian Kasenene, Morogoro


maipacarusha20@gmail.com


KATIBU  Mkuu  wa Chama Cha  Mapinduzi(CCM) Balozi Dk Emmanuel Nchimbi amewataka wasomi kujitokeza kupiga kura za viongozi wa vitongoji,vijiji na mitaa  na kwamba iwapo wasomi hao watashindwa kujitokeza kwa wingi katika uchaguzi wa Serikali za mtaa elimu yao itakuwa haijawasaidia.


Alisema hayo mkoani Morogoro wakati wa mkutano wa 24 wa Baraza la wahitimu wa Chuo  Kikuu Cha Mzumbe,ambapo Dk Nchimbi ni mjumbe wa baraza hilo aliyehitimu mwaka 1997 na alikuwa mgeni maalumu.


Akizungumza mara baada ya kumaliza kwa mkutano huo wa baraza Dk Nchimbi alisema Novemba 27 Mwaka huu ni siku muhimu ya kuchagua viongozi wa serikali za mitaa hivyo ni vyema wasomi hao wakawa mstari wa mbele kwenye zoezi hilo.


Aidha katibu mkuu huyo wa CCM alitumia fulsa hiyo kuhamasisha wananchi wote kutumia haki yao ya msingi kuchagua viongozi wanaowafaa kwenye maeneo yao.


Katibu mkuu huyo wa CCM alisema Serikali ya mtaa ndio nafasi ya mwanzo kwa wananchi kupata  huduma ikiwa ni pamoja na  maendeleo kwa ujumla.


"Hii ni nafasi muhimu, nafasi ambayo ndio kwanza mtanzania  akipata tatizo kwenye mtaa, kijiji na  kitongoji anapata huduma kuanzia huko sio nafasi ya kupuuzwa kabisa,"alisema.


Alisema vyama vyote vinaavyogombea  vimepimwa kwa  rekodi na historia yake ,  na kwamba, ni chama imara na madhubuti na hivyo  kuwataka Watanzania kukichagua ili kuendelea kukipa nguvu ya kuwaletea maendeleo.


"Ngoja niwaeleze wakati nikiwa chuoni hapa  niligombea Uraisi wa Serikali ya wanafunzi nilishindwa kwa kura 13 lakini sikununa na aliyenishinda ni rafiki yangu hadi leo nashangaa watu huko kwenye maeneo yetu wakishindwa tu wanaanza kulalamika tunatakiwa kuwa na subira,"alisema.


Alisema wapo watu wanagombea wakishindwa wananuna hata kama wamepata kura mbili ambapo aliwataka waliogombea kuacha tabia hizo wanapokosa nafasi za uongozi.


Pia Dk Nchimbi aliwaasa wahitimu kutambua kuwa kwa sasa waajiri walio wengi hawaangalii kuajiri peke yake bali wanatafuta waajiriwa wenye uwezo na ujuzi wa kufanya shughuli zaidi ya moja.


Aidha aliwasihi wasomi kutochukulia mabadiliko ya teknolojia yanayoendelea ikiwemo teknolojia  ya akili mnemba (AI) kama kikwazo katika ajira na shughuli zao badala yake watumie kama fursa ya kuonesha uwezo  wao zaidi wa kitaaluma.


Naye Makamu mkuu wa Chuo Kikuu Cha Mzumbe Profesa Wilium Mwegoha alisema wamevunja rekodi kwa kutoa Wahitimu wa Shahada ya  Uzamivu  Maprofesa (Phds)12 katika mahafari ya 23  yanayofanyika Novemba 24 mwaka huu ambapo mgeni maalumu  ni Rais wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania Samia Suluhu Hassan.


Alisema idadi hiyo ya Maprofesa imekuwa mara mbili ya mwaka 2023 ambapo walitoa maprofesa 6, huku mwaka 2022 walikuwa 3 na mwaka 2021 walikuwa 3.


Pia alisema chuo hicho kimeendelea kupata mafanikio makubwa kwa kudahili wanafunzi ambapo kwa sasa idadi ya wasichana na wanaume zinaribiana ambapo wanaume ni asilimia 50.2 na wasichana ni asilimia 49.8


Alisema wameongeza wigo wa masomo kwa njia ya online ili kutanua wigo wa kudahili wanafunzi wengi kutokana na kwamba  kwa sasa watu wengi wanatumia njia hiyo ya online.


Rais wa Baraza la wahitimu wa chuo kikuu Mzumbe CAG mstaafu CPA Ludocick Utoh akasema kwa mazingira  ya sasa unapojiendeleza  kwa maendeleo yeyote ni vyema kufanya hivyo kwa maendeleo ya watu na sio binafsi kama ilivyo kauli mbiu ya chuo hicho.


"Tujali zaidi kwa ajili ya maendeleo ya taifa badala ya kujijali kwanza sisi wenyewe"alisema.


Viongozi mbalimbali walialikwa katika baraza hilo walihudhuria mkutano huo akiwemo Waziri wa maliasili na utalii Balozi Dk Pindi Chana, Waziri wa Madini Anthony Mavunde, Mkuu wa mkoa wa Morogoro wa Adam Malima na baadhi ya wakuu wa Wilaya.


Mwisho

No comments: