Na Mwandishi Wetu, Maipac
maipacarusha20@gmail.com
Chama kikuu cha Ushirika LINDI MWAMBAO, kimeuza Korosho Tani 693 kwa bei ya juu Shilingi 2,600/= na bei ya chini 2,450/= kwenye mnada uliofanyika leo Tarehe 30 Novemba 2024.
Mnada huo umefanyika katika kijiji cha Kiwalala Wilaya ya Lindi Mkoani Lindi, ukiendeshwa kwa njia ya mtandao kupitia soko la bidhaa Tanzania TMX.
Mrajisi msaidizi wa mkoa wa Lindi bw. Keneth Shemdoe, amewataka wakulima kutumia vema fedha za malipo ya Korosho wanazoendelea kuzipata ili ziwasaidia katika kujiendeleza kwenye mambo mbalimbali.
"Malipo haya ya korosho yatumike kufanya mambo ya maendeleo ikiwa ni pamoja na kupata mitaji ya kuanzishia biashara, tuwaombe wakulima wazingatie matumizi sahihi ya fedha hizi ili zije kuwasaidia katika mambo mengine ya msingi na yenye tija kwao" amesisitiza Shemdoe.
Wakizungumzia mfumo wa TMX unaotumika kwa mara ya kwanza kwenye minada ya Korosho mkoani Lindi msimu 2024/2025, baadhi ya wakulima wameeleza kufurahishwa na uwazi uliopo kwenye minada hiyo.
Hawa Mmakoja mkulima wa kijiji cha Kiwalala akizungumza kwa niaba ya wakulima wenzake, amesema awali hawakujua kama mfumo huo utakuwa na tija kwa wakulima.
"Mwanzoni tulijua huu ni mfumo wa majaribio tu na utashindwa tutarejea kwenye utaratibu wa mwanzoni, lakini hadi kufikia sasa mnada wa nane tunasema huu ndio utaratibu unaotakiwa kutumika kila mwaka" amezema Bi. Hawa.
No comments:
Post a Comment