![]() |
Na Lilian Kasenene,Morogoro
maipacarusha20@gmail.com
WANAWAKE wametakiwa kupima afya zao mara kwa mara ili kugundua mapema magonjwa hatari kama saratani ya shingo ya kizazi na saratani ya matiti, hatua itakayosaidia kuokoa maisha na kupunguza madhara yanayoweza kuzuilika.
Wito huo umetolewa na Mkemia na Mtafiti wa Miti Dawa kutoka Chuo kikuu Cha Sokoine Cha kilimo SUA, Prof Faith Mabiki, alipokuwa akizungumza katika kongamano maalum la afya ya wanawake lililofanyika chuoni hapo.
Prof Mabiki alisema wanawake wengi bado huweka afya zao kama jambo la pili kutokana na hofu au ukosefu wa taarifa sahihi, hali inayoweza kusababisha madhara makubwa yanayozuilika.
“Kuna hofu kubwa miongoni mwa wanawake kuhusu vipimo vya afya, lakini teknolojia ya kisasa imerahisisha uchunguzi na kutoa matokeo sahihi bila usumbufu mkubwa,"alisema.
"Ni bora kugundua mapema, kutibiwa na kuendelea na maisha yenye afya njema,” alisema Prof. Mabiki.
![]() |
Alisisitiza kuwa mwanamke mwenye afya bora huongeza tija katika familia, kazini na katika jamii kwa ujumla, hivyo kuchangia maendeleo ya taifa.
Mwenyekiti wa bChama Cha wafanyakazi wa taasisi ya Elimu ya juu, sayansi, teknolojia, Ufundi stadi,habari na utafiti(RAAWU) Tawi la SUA, Faraja Kamendu, alisema menejimenti ya chuo inatambua na kuthamini mchango wa wanawake katika maendeleo ya taasisi hiyo.
Alieleza kuwa kupitia semina hiyo ya afya, wanawake wanapata elimu muhimu kuhusu changamoto za kiafya na namna ya kujikinga nazo. Aliongeza kuwa chama hicho kinaendelea kushirikiana na menejimenti ya chuo kuhakikisha ustawi wa wafanyakazi, hususan wanawake, unaimarishwa.
Aliwahimiza wanawake wa SUA kujali afya zao, kujiamini na kutambua uwezo wao mkubwa katika utendaji wa kazi na majukumu ya kijamii.
Naye Dk Graca Chotamawe, Daktari wa watoto katika Hospitali ya SUA, akitoa mada katika kongamano hilo,alisema magonjwa yasiyoambukiza yanaendelea kuwa tishio kubwa duniani na barani Afrika.
Alieleza kuwa takribani watu milioni 41 hupoteza maisha kila mwaka duniani kutokana na magonjwa yasiyoambukiza, huku barani Afrika, magonjwa hayo yakiongezeka kwa kasi na kuchukua nafasi kubwa kuliko baadhi ya magonjwa ya kuambukiza.
Kwa mujibu wa Dk Chotamawe, sababu kuu za ongezeko hilo ni mabadiliko ya mtindo wa maisha, kupungua kwa kufanya mazoezi, kuongezeka kwa matumizi ya magari, bodaboda na bajaji, matumizi ya dawa za kulevya, mabadiliko ya mifumo ya kilimo pamoja na umasikini.
Aliongeza kuwa magonjwa yasiyoambukiza huongeza mzigo wa kiuchumi kwa familia nyingi kwa kuwa ni ya muda mrefu na huhitaji gharama kubwa za matibabu, jambo linaloweza kusababisha watu wengi kuangukia katika umasikini.
Kongamano hilo limehudhuriwa na watumishi wanawake wa SUA, likijumuisha wanafunzi, likiwa ni sehemu ya juhudi za kuongeza uelewa, kuhamasisha uchunguzi wa mapema na kujenga utamaduni wa kujali afya miongoni mwa wanawake.
Pia wanawake hao zoezi la upimaji wa afya wa magonjwa mbalimbali ikiwemo sukari na presha.
Mwisho



No comments:
Post a Comment