MAMIA YA WAKAZI MIRERANI WAJITOKEZA IBADA YA IJUMAA KUU - MAIPAC MEDIA TANZANIA

Breaking

MAIPAC MEDIA TANZANIA

A Centre for Indigenous and Pastoralists Community Informations




Saturday, 4 April 2026

MAMIA YA WAKAZI MIRERANI WAJITOKEZA IBADA YA IJUMAA KUU

 


Na Mwandishi wetu, Mirerani 


maipacarusha20@gmail.com 


MAMIA ya Wakristo Wakatoliki wa Mji mdogo wa Mirerani Wilayani Simanjiro Mkoani Manyara, wamejitokeza kwa wingi katika maadhimisho ya ibada ya Ijumaa kuu iliyofanyika katika Parokia ya Bikira Maria Malkia wa Rozali Takatifu Jimbo Kuu la Arusha.


Wakristo hao wameungana na wenzao ulimwenguni kushiriki ibada ya Ijumaa kuu wakikumbuka mateso na kifo cha Yesu msalabani zaidi ya miaka 2000 iliyopita.


Paroko wa Parokia ya Bikira Maria Malkia wa Rozali Takatifu, Padri Aristarki Tarimo amewataka wakristo wanaoishi na wanawake wao majumbani bila kufunga ndoa wabadilike na kubariki ndoa zao.


Padri Tarimo ameeleza kwamba wakristo wasiishi kwa mazoea majumbani mwao na wanawake wao bila kufunga ndoa kwani fursa ya kubariki ndoa zao wanazo pindi wakiamua.


"Maisha ya suria siyo vyema kwa wakristo hivyo wanaoishi na wanawake bila kufunga ndoa badilikeni na kufunga ndoa kwani nafasi na fursa mnazo," amesema padri Tarimo.


Pia, ameonya jamii kutojihusisha na ushirikina kwa ajili ya kutafuta kazi, kupata mchumba, kutafuta mali, kuongeza kipato au kufaidika na chochote kile pasipokuwa na imani kwa Mungu.


Amesema jamii isijihusishe na ushirikina na kujificha kwenye kichaka cha kudai kuwa Mungu amesema jisaidie nami nitakusaidia hivyo kushiriki katika dhambi hiyo.


Hata hivyo ameeleza kuwa kwenye ibada ya Ijumaa kuu inatoa nafasi nzuri ya kutafakari mateso na kifo cha Yesu kuwa ni ukombozi wa watu.


Amesema mtu akiwa na orodha ya matendo mema anayofanya hayawezi kuwa tiketi ya kwenda mbinguni bila yeye mwenyewe kumkiri Yesu kuwa ni mwokozi wa ulimwengu huu.


"Unafanya mema kwa sababu Yesu ameshawakomboa binadamu kupitia kifo chake kwani wewe mwenyewe hauwezi kuwa mwokozi wako mwenyewe," amesema Padri Tarimo.


Ameeleza kuwa wakati huu dunia inakumbuka kifo cha Yesu Kristo msalabani bado watu mbalimbali wanasikitika na kifo hicho akiwemo raia mmoja wa nchi jirani aliyefungua kesi mahakamani akieleza kuwa Yesu alionewa.


MWISHO

No comments: