Wafugaji wahimizwa kuzingatia matumizi sahihi ya dawa kudhibiti usugu wa vimelea - MAIPAC MEDIA TANZANIA

Breaking

MAIPAC MEDIA TANZANIA

A Centre for Indigenous and Pastoralists Community Informations




Sunday, 7 June 2026

Wafugaji wahimizwa kuzingatia matumizi sahihi ya dawa kudhibiti usugu wa vimelea

 



Na Mwandishi wetu, Kilimanjaro 


maipacarusha20@gmail.com 


Moshi.Wafugaji wa kuku wa nyama nchini wametakiwa kuzingatia matumizi sahihi ya dawa pamoja na mbinu bora za ufugaji ili kupunguza tatizo la usugu wa vimelea dhidi ya dawa, ambalo limeendelea kuwa tishio kwa afya ya binadamu.


Akizungumza leo  katika mafunzo kwa wafugaji wa kuku wa nyama, Mkurugenzi Mtendaji wa Tanganyika Farmers Association (TFA), Jastin Shirima, amesema usugu wa vimelea dhidi ya dawa ni changamoto kubwa duniani inayohitaji juhudi za pamoja ili kuudhibiti kutokana na athari zinazoweza kuwakumba  walaji.


Shirima amesema kuwa, tafiti mbalimbali zimeonyesha kuwa ikiwa matumizi ya dawa  yataendelea kufanyika bila kufuata taratibu sahihi, kuna hatari ya dawa nyingi zinazotumika kutibu magonjwa ya wanyama kupoteza uwezo wake wa kutibu magonjwa na hivyo kusababisha athari kwa binadamu.


"Unapotumia antibiotiki bila kumaliza dozi au kutumia dawa pasipo ushauri wa kitaalamu kwenye mifugo, unachochea usugu wa dawa. Masalia ya dawa yanaweza kubaki kwenye bidhaa za mifugo na kuathiri afya ya watumiaji pamoja na kuongeza tatizo  la usugu wa vimelea," amesema Shirima 


Aidha, amesema TFA inaendelea kutoa elimu kwa wafugaji kuhusu matumizi bora ya dawa, ikiwemo kutumia dawa kwa wakati sahihi, kwa kiwango kinachotakiwa na kwa kuzingatia ushauri wa wataalamu ili kuepuka athari zinazoweza kujitokeza kwa binadamu.


"Ikiwa hatutabadili namna tunavyotumia dawa, kuna hofu kuwa dawa nyingi zilizopo hospitalini na kwenye mifugo hazitakuwa na uwezo wa kutibu magonjwa. Hii ni hatari kubwa kwa afya ya binadamu na maendeleo ya sekta ya mifugo," amesema Shirima 


Kwa upande wake, Mkufunzi kutoka Wakala wa Vyuo vya Mafunzo ya Mifugo (LITA)Misheck Mulilo, amesema uwepo wa mafunzo hayo kwa wafugaji unalenga kuongeza uelewa wa jamii kuhusu namna ya kukabiliana na tatizo la usugu wa vimelea dhidi ya dawa ambalo linaendelea kukua kitaifa na kimataifa.


"Tusipotumia mbinu mbadala za kulidhibiti tatizo hili la usugu wa dawa dhidi ya vimelea linaweza kusababisha athari kubwa kwa afya ya binadamu, mifugo na mazingira," amesema Mulilo.


Aidha, amesema  kuwa endapo tatizo hilo halitadhibitiwa kwa ushirikiano wa serikali, sekta binafsi na jamii kwa ujumla, linaweza kuathiri afya za watu, mifugo na hata biashara za mifugo.


"Zipo tafiti mbalimbali zinazoonyesha kuwa tatizo la usugu wa vimelea dhidi ya dawa linaendelea kukua. Hivyo, ni muhimu kuunganisha nguvu za wadau wote ili kulidhibiti kabla halijaleta madhara makubwa zaidi," alisisitiza.


Mulilo amesema kuwa njia mojawapo ya kupunguza matumizi ya dawa ni kuzingatia kanuni za 'biosecurity' ambazo husaidia kuzuia magonjwa kuingia katika mabanda ya mifugo.


Akizungumza moja wa wafugaji wa kuku, Erasto Massawe, amesema:


"Kwa kuwa tunafuga kuku kwa gharama kubwa, ikitokea kuku anaumwa katika wiki ya mwisho kabla ya kuuzwa au kutolewa, mara nyingi tulikuwa tunampa dawa. Hata hivyo, mafunzo haya yametusaidia sana, na tumejifunza kuepuka matumizi ya dawa kupita kiasi. Tunaomba mafunzo haya yaendelee kutolewa mara kwa mara kwa sababu yanatupa elimu na kutusaidia kuboresha ufugaji wetu."


Mwisho.

No comments: