KAMISHNA MABULA AIELEKEZA TAWA KANDA YA KATI KUWEKA MIFUMO MADHUBUTI YA USIMAMIZI WA KARAKANA - MAIPAC MEDIA TANZANIA

Breaking

MAIPAC MEDIA TANZANIA

A Centre for Indigenous and Pastoralists Community Informations




Monday 15 January 2024

KAMISHNA MABULA AIELEKEZA TAWA KANDA YA KATI KUWEKA MIFUMO MADHUBUTI YA USIMAMIZI WA KARAKANA

 





Na: Lilian Kasenene,Morogoro 


maipacarusha20@gmail.com


Kamishna wa Uhifadhi wa Mamlaka ya Usimamizi wa Wanyama Pori Tanzania (TAWA) Mabula Misungwi Nyanda ameelekeza uongozi wa Tawa Kanda ya kati kuweka mfumo madhubuti wa usimamizi wa karakana ya matengenezo ya magari na mitambo inayojengwa kwa kuwapeleka wataalamu wa vifaa ili iweze kusimamiwa na kuendeshwa Kisasa.


Aidha ameeleza kufurahishwa kwake na ubora wa viwango vya ujenzi wa karakana hiyo inayotajwa kuwa ni kubwa kuliko karakana zote zilizojengwa na taasisi hiyo.


Ameyasema hayo wilayani Manyoni mkoani Singida akiwa katika ziara yake Makao Makuu ya Tawa Kanda ya Kati, ziara yenye lengo la kukagua shughuli za uhifadhi na utalii zinazotekelezwa na Mamlaka hiyo wilayani humo.


"Nimetembelea na kukagua karakana, kimsingi nimeona imejengwa vizuri na pia nimeona ina uwekezaji mkubwa wa vifaa vitavyotumika na nina imani hii karakana itatusaidia sana" amesema


Akibainisha sababu za kuifanya karakana hiyo kuwa kubwa wilayani humo, Kamishna Mabula alisema Manyoni ni katikati ya nchi na ni sehemu inayofikika kwa urahisi, hivyo kutokana na ukubwa wake itatumika kutengeneza magari si tu ya Kanda ya Kati bali ya taasisi nzima.


Aidha, Kamishna Mabula ametumia ziara hiyo kuwahimiza Maafisa na Askari wote wa TAWA kurejea mpango mkakati wa  taasisi hiyo ambao unafikia kikomo Mwaka 2026 ili waweze kutekeleza majukumu yao ipasavyo.


Amefafanua kuwa mpango mkakati wa TAWA una malengo makuu matatu ambayo ni kuhakikisha rasilimali ambayo TAWA imepewa kusimamia inakuwa salama, pia kuhakikisha wateja wote wa taasisi wakiwemo wawekezaji wanapata huduma na kuridhika na huduma inayotolewa na lengo la tatu ni kuhakikisha TAWA inafanya kazi kwa ufanisi na tija.


Kamishna huyo amesisitiza kuwa malengo hayo hayataweza kutimia bila kuishi  katika tunu za taasisi hiyo ambazo ni uadilifu, kufanya kazi kwa ushirikiano, kutenda kazi kwa ubunifu pamoja na kufanya kazi kwa juhudi na maarifa.


Naye Kamishna Msaidizi Ulinzi wa Rasilimali za Wanyamapori Hadija Malongo akimwakilisha Kamishna wa Uhifadhi wa Kanda ameishukuru Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia TAWA kwa kuwezesha ujenzi  wa karakana hiyo ambayo kukamilika kwake kutasaidia kupunguza gharama za matengenezo ya magari ambayo ilikuwa changamoto kubwa


Mradi wa ujenzi wa karakana hiyo umegharimu zaidi ya shilingi 217 Million.



No comments: