Biashara ya mkojo wa sungura yageuka "lulu" kwa wakulima nchini. - MAIPAC MEDIA TANZANIA

Breaking

MAIPAC MEDIA TANZANIA

A Centre for Indigenous and Pastoralists Community Informations




Friday 24 February 2023

Biashara ya mkojo wa sungura yageuka "lulu" kwa wakulima nchini.

 





Sungura wakiwa katika Banda maalum ambalo hufugwa ili kukusanya mkojo.





Mwandishi wetu, Maipac
maipacarusha20@gmail.com


Changamoto za matumizi ya mbolea na madawa ya kilimo  ya viwandani,kumeibua biashara mpya ambayo inakuwa kwa kasi nchini.

Biashara hiyo ni ya mkojo wa sungura ambao unauzwa kwa lita kati ya sh 7000 hadi 10,000 bei kubwa kupita hata bei ya mafuta ya petroli.

Wateja wakubwa wa mkojo huu ni wakulima wa maeneo ya mkoa wa Arusha na Kilimanjaro,Mbeya,Njombe,Songwe na mikoa mingine ambayo inalima mboga mboga na matunda.

Lakini soko hili pia  limeibua biashara ya ufugaji sungura katika mashamba makubwa na kuwa na sungura kati ya 5000 hadi 10,000.

Mkojo wa sungura  umethibitishwa na wataalamu wa kilimo kama dawa la kufukuza wadudu shambani ,kupata mbolea na kuimarisha afya ya mimea. 

Mahitaji ya mkojo huo, yamekuwa yakiongezeka siku hadi siku, hasa kutokana na kuthibitika una uwezo mkubwa wa kufukuza wadudu waharibifu  shambani lakini pia kuimarisha afya ya mmea.

Uchunguzi uliofanywa katika baadhi ya mashamba ya kilimo Hai,(kilimo ambacho hakitumii mbolea za viwandani na pembejeo za viwandani) umebaini kwa sasa kuna ongeko la mahitaji ya mkojo wa sungura kwa wakulima na kumesababisha bei yake kupaa kutoka kiasi cha sh 2000  kwa lita hadi  kati ya sh  7000 hadi 10000.

Lita moja  na nusu ya mkojo wa sungura inachanganywa na lita 10 za maji na baada ya kuchanganya huweza kupulizia shamba hadi hekali moja kulingana na mazao yaliyopo shambani.

Mtaalam wa ufugaji Sungura katika  shamba la kiogani la  St Joseph  lilipo  Kwanyange Wilaya Mwanga Mkoa Kilimanjaro, Felisian Pius anasema matumizi ya mkojo wa Sungura imekuwa ni suluhu kwa wakulima ,kudhibiti wadudu waharibifu na  kuimarisha afya ya mimea.

Anasema matumizi hayo ya mkojo wa Sungura  yamevutia watu wengi kujikita pia katika ufugaji wa sungura ili kuvuna mkojo huo kwa matumizi ya mashambani na kwenye bustani.

Dr.Peter Mushi mtaalamu wa dawa za kilimo na mifugo anasema kitaalamu imethibitika mkojo wa sungura una kemikali ambazo zinaua wadudu lakini hazina athari kwa binadamu.

"Bado tafiti zaidi zinaendelea duniani kuhusiana na mkojo wa sungura huenda miaka ijayo ukaboreshwa na kuuzwa kitalaamu wa zaidi"amesema

Mtaalam wa ufugaji sungura na kutengeneza dawa ya kuuwa wadudu na kuimarisha mmea Felisian Pius katika shamba la kiogan la st Joseph kwanyange Mwanga akionesha jinsi ya kukusanya mkojo

    Jinsi ya kuwandaa Sungura hadi kuvuna mkono wao.
Pius anasema Sungura wanapaswa kufugwa katika mabanda maalum ambayo ni rahisi kukusanya mkono wao na kupewa chakula cha kutosha hasa majani yenye ukavu na maji kwa wingi.

Anasema  Sungura wanapaswa kujengewa banda la mabanzi na kuishi juu na kuhakikisha sungura wa familia moja hawazaliani ili kuepuka magonjwa na vifo.

Anasema  Sungura watano hadi kumi walioshiba vizuri na kupewa maji ya kutosha wanaweza kuzalisha mkono wa kutosha kwa ajili ya shamba na bustani kwa mwaka mzima na kwa siku wanaweza kuzalisha lita moja ya mkojo.

Anasema  mkojo unaweza kukusanywa kupitia mfumo wa kuwa na sehemu ya kukusanya mkojo kupitia boma maalum, ambao sio rahisi kuharibika ama kumwagika.

Mkojo huo wa  Sungura  ukiwa unakusanywa kwenye bomba hilo ambalo unaweza kuliweka   nyuma ya Banda lililojegwa kwa  kuliweka upande mmoja umeinuka kidogo na upande mwngine unakuwa chini.

"boma hilo litasaidia  mkojo uweze kutiririka kwa urahisi na kuingia katika chombo maalumu  ambacho utakuwa umeandaa"anasema

Anasema Mfugaji anatakiwa kukusanya mkojo wa sungura mara mbili mpaka Mara tatu kwa siku ili kuzuia kuchanganyika na maji ikiwepo ya mvua kama ikinyesha.

Jinsi ya kutumia Mkojo.

Mkojo wa Sungura ukikusanywa  lita moja na nusu na kuchanganywa na lita 10 za  maji na mkulima atapuliza  katika  shamba la ekari moja.

Mkojo huo unatumika kama  Dawa ya kufukuzia wadudu na mbolea ya kurutubisha mimea Katika shamba lako lenye mchanganyiko wa mimea.

"Jambo la kuzingatia Katika utiaji wa mkojo wa sungura katika shamba la mkulima ni kuhakikisha anaweka kwa kila shina kwa chinina sio kuweka katika majani ya mmea.

Anasema muda mzuri ya kupuliza dawa hiyo na mkojo wa sungura ni asubuhi kabla ya jua kuwa kali kwani ikipuliziwa mchana jua likiwa kali mimea inaweza kuungua.

Faida zitokanazo na matumizi ya mkojo wa sungura.

 Mkulima anayetumia mkojo mavuno uongezeka kwa wingi,shamba halitakuwa halina wadudu waharibifu wa mimea.

anasema mkojo huo wasungura kwa kuchanganya na maji pia inasaidia shamba kuwa na rutuba ya kutosha na ulinzi wa udongo.


Mkulima Leokadia Peter wa kijiji cha kwanyange wilaya ya mwanga mkoa wa Kilimanjaro anasema  tangu aanze kutumia mkojo wa Sungura ameweza kuimarisha afya ya mimea shambani kwake.

Leokadia anaeleza amefanikiwa  sana katika kilimo cha mbogamboga mara tu alipoanza kutumia mkojo wa sungura na kubadili hali ya uvunaji kwani amekuwa akipata mazao mengi hasa mbogamboga ambazo awali zilikuwa zikisumbuliwa kwa kuliwa na wadudu.

Julius Kanangira ni mkulima wa mbogamboga anasema, tangu ameanza kutumia mbolea zaasili na mkojo wa sungura mavuno yameongezeka.

"mimi situmii mbolea za viwandani, natumia kinyesi cha ng'ombe na mkojo wa sungura tu na nalima mbogamboga kwa ufasini "anasema

Hata hivyo anasema changamoto kubwa ni upatikanaji wa mkojo wa kutosha wa sungura wakati wote.

"nafikiria na mimi kuanza kufuga sungura ili iwe rahisi kupata mkojo na mbolea nyingine"anasema

Akizungumza na mwananchi,Meneja wa mradi wa mkulima mbunifu Erica Rugabandana anasema matumizi ya mbolea za asili na mkojo wa Sungura ni suluhisho na kuacha matumizi ya mbolea na viwandani na madawa kwa ajili ya kukuza mazao na kupambana na wadudu.

"sisi tumekuwa na mradi huu ambao ni kilimo endelevu unafadhiliwa  na shirika la biovision (BV) foundation lilipo switzerland na tunaona mafanikio makubwa kwa wakulima wa kilimo hai"anasema
Mtaalam wa ufugaji sungura na kutengeneza dawa ya kuuwa wadudu na kuimarisha mmea Felisian Pius katika shamba la kiogan la st Joseph kwanyange Mwanga akionesha jinsi ya kukusanya mkojo
 
Mratibu wa programu  ya mawasiliano ya shirika la  Biovision  Afrika Trust,Fredrick Ochieng anasema kumekuwepo na ongezeko la matumizi ya pembejeo na mbolea za viwadani ambazo baadhi huzalisha sumu ambayo inaathiri afya za watu.

"kwa wakulima kurejea katika kilimo cha asili kwa kutumia mbolea za asili na pembejeoza asili ni suluhu kubwa katika kupata vyakula salama"anasema 


Wengi hufuga Sungura kwa ajili ya matumizi ya chakula na urembo lakini sasa Sungura ni dili kwa wakulima hasa baada ya kuthibitika mkojo wake ni dawa ya kufukuza wadudu lakini pia ni mbolea katika mimea na kurutubisha ardhi.

No comments: