![]() |
Picha ya pamoja na mgeni rasmi mwenyekiti wa halmashauri ya wilaya ya Monduli |
NA: MAIPAC TEAM, MONDULI
maipacarusha20@gmail.com
Vyombo vya habari nchini, vimeombwa kutoandika habari hasi pekee juu ya sekta ya mifugo, kwani mifugo ina mchango mkubwa katika uchumi wa taifa na inategemewa na mamilioni ya Watanzania kuendesha maisha yao
Mchango wa sekta ya mifugo kwa pato ya Taifa ni asilimia 7 na Tanzania kuna jumla ya ng’ombe 35.3 milioni, mbuzi 25.6 milioni na kondoo 8.8 milioni .
Hata hivyo, katika siku za karibuni, kumekuwepo na operesheni kadhaa ya kukamata na kutaifisha mifugo inayoingia maeneo yaliyohifadhiwa na kuwaondoa wafugaji katika maeneo mbali mbali nchini.
Mshauri Mwelekezi wa mradi wa uboreshaji na uzalishaji nyanda za malisho ya mifugo wilaya ya Monduli, Mkoa Arusha Dk Stephen Nindi Akizungumza katika uzinduzi wa mradi wa uendeshaji na uboreshaji wa Nyanda za malisho wilaya ya Monduli, amesema mchango wa sekta ya mifugo ni mkubwa katika taifa lakini inavyoripotiwa ni kama mifugo ni uharibifu wa mazingira pekee.
“tunawaomba wanahabari mtusaidie muandike na habari nzuri za mifugo, sio kila siku kuwaondoa huku, kufukuzwa kama vile mifugo haina faida katika jamii”amesema
Amesema ufugaji ni jambo muhimu kwa taifa kwani inasaidia maisha ya mamilioni ya watu, ikiwepo kupata fedha, kusomesha watoto,kupata maziwa na nyama na mazao mengine .
Awali Profesa Ismail Selemani amesema sekta ya mifugo ikiwezeshwa ina manufaa makubwa kwa jamii na ndio sababu kuna miradi ya kuboresha nyanda za malisho ili kuwahakikisha wafugaji malisho ya uhakika.
Profesa Seleman amesema kupitia mradi wa uanzishwani na uboreshwaji wa nyanda za malisho wlaya ya Monduli, ambao unatekelezwa na shirika la Utafiti na Maendeleo(CORDS) wamefanya tafiti na kubaini majani ambayo yanaweza kuoteshwa katika maeneo mbali mbali na kupunguza tatizo la malisho.
“tumefanya tafiti za majani ya malisho, katika maeneo yenye, ukame, maeneo yenye baridi na maeneo mengine na tumejiridhisha kuwa majani yakipandwa katika maeneo hayo yataota na kuondoa tatizo la malisho”amesema
Afisa Malisho wa halmashauri ya wilaya ya Monduli, Mamus Toima amesema maeneo ya malisho ya asili yanaendelea kupungua kutokana na athari za mabadiliko ya tabia nchi katika wilaya hiyo.
“tunaimani kupitia mradi huu wa CORDS majani ya asili ambayo yametoweka yatarudi lakini pia tutapata majani mapya ambayo yanastahimili ukame”amesema
Mkurugenzi wa shirika la CORDS, Lilian Looloitai, amesema mradi huo ambao unadhaminiwa na shirika la Maendeleo ya umoja wa mataifa (UNDP) kupitia programu ya miradi midogo na kuratibiwa na shirika la jumuiko la maliasili Tanzania(TNRF) utasaidia wafugaji wanawake wilaya ya Monduli.
No comments:
Post a Comment