AJIRA MPYA 231 ZA RAIS SAMIA KUTATUA KERO ZA TEMBO- MCHENGERWA - MAIPAC MEDIA TANZANIA

Breaking

MAIPAC MEDIA TANZANIA

A Centre for Indigenous and Pastoralists Community Informations




Thursday 27 April 2023

AJIRA MPYA 231 ZA RAIS SAMIA KUTATUA KERO ZA TEMBO- MCHENGERWA

 

Waziri wa Maliasili na Utalii Mheshimiwa Mohamed Mchengerwa akizungumza wakati WA kuhitimisha mafunzo ya askari WA Uhifadhi 

Katibu Mkuu Wizara ya Maliasili na Utalii Dkt Hassan Abbas akizungumza wakati wa kuhitimisha mafunzo ya askari wa uhifadhi





Mwandishi wetu, Mlele

maipacarusha20@gmail.com


Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe. Mohamed Mchengerwa   amewaelekeza watendaji wa Wizara yake kuhakikisha  kuwa askari  wote wapya wapatao 231  wa uhifadhi waliohitimu mafunzo ya awali ya  kijeshi katika Kituo cha Mafunzo ya Kijeshi  ya Jeshi  la Uhifadhi (JU) Mlele, Mpanda  mkoani Katavi,  waende mara moja  kwenye maeneo  korofi ili  kudhibiti wimbi la  Wanyama waharibifu  kwa  kuhakikisha  wanadhibitiwa na kurudishwa hifadhini.


Pia  amempongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania  Mhe. Rais Samia Suluhu Hassan kwa kutoa ajira  hizo  mpya na kutoa miongozo  mbalimbali inayosaidia uhifadhi wa raslimali na kuwa mstari  wa mbele kutangaza utalii kiasi cha yeye mwenyewe  kucheza  filamu ya Royal Tour ambayo imeleta  mageuzi makubwa nchini kwenye sekta ya utalii.  


Waziri Mchengerwa ametoa kauli  hizo Jana  wakati akifunga   mafunzo ya awali  kwa askari  wenye ajira mpya 231 wa jeshi  la  uhifadhi kutoka Wakala wa Huduma za Misitu nchini (TFS) na Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro katika Kituo cha Mafunzo ya Kijeshi  ya Jeshi  la Uhifadhi (JU) Mlele, Mpanda  mkoani Katavi ambapo ameambatana na Katibu Mkuu, Dk.Hassan Abbasi .


Waziri pia aliwatunukia  vyeo askari wawili wa jeshi la uhifadhi,  Abel Masota  na Carloline Malundo  kuwa  Naibu Kamishna. 



Pia wakati akimkaribisha Waziri Mchengerwa atoe  hotuba yake, Dk.Abbasi  alitoa taarifa kuwa wahitimu hao wote watapatiwa barua zao  Jana hiyo hiyo za kuripoti katika  vituo  vyao vya uhifadhi na  kwamba hiyo ni dhamira ya Serikali inayoongozwa  na Rais Samia Suluhu Hassan ya kutaka kazi iendelee. 




Mchengerwa amewataka  askari hao wakawe wabunifu  na kutanguliza uzalendo  huku akiwaasa  kutumia mbinu  za  kijeshi walizofundishwa ili kulinda kikamilifu raslimali zilizopo na kuepusha   madhara  makubwa  inapotokea uvamizi wa aina  yoyote  kwenye  maeneo ya Hifadhi.



" Na kwa kuwa  jukumu hili la udhibiti ni la kila  mmoja wetu (Serikali na Wananchi) ninawaagiza  wakuu wote  wa hifadhi nchi nzima  kujipanga  kikamilifu kwa kuweka  mikakati thabiti na endelevu la kukabiliana na Wanyama hao wakali na waharibifu, shirikianeni  na wananchi kutoa elimu na  nyenzo kwa  VGS za kukabiliana  nao” amesisitiza "Mchengerwa 



Pia amewaasa wahifadhi  kushuka chini kwenye  jamii na kutoa elimu  kuhusiana na uhifadhi  kwa kushirikiana na  viongozi wa serikali na dini mbalimbali pamoja na  viongozi wa  makundi  mbalimbali  ya kijamii ili akiwepo  mwanananchi anayekaidi   achukuliwe sheria.



Amewatia  moyo wananchi wote ambao wanaishi maeneo jirani na hifadhi kuwa Serikali yao ipo  pamoja nao katika kuhakikisha kuwa changamoto zote za uvamizi  wa Wanyama wakali  na waharibifu  zinatatuliwa  katika  kipindi kifupi kijacho.“ Pia  leo tunapoadhimisha  miaka 59 ya Muungano wetu  ni kipindi  tunachoona  Serikali  yetu tukufu ikichukua  hatua mbalimbali  kuimarisha uhifadhi eneo la Hifadhi ya Ngorongoro kwa kuwahimiza wananchi  kuhama  maeneo haya kwa hiyari na  kuwatafutia  makazi  mbadala na bora. Jambo hilo limeleta tija sana  katika uhifadhi wa eneo hilo” amefafanua Mhe. Mchengerwa



Waziri pia ameonya  tabia ya  baadhi ya wahalifu ya  kujivika cheo cha “wananchi”  na kufanya uhalifu ambapo amesema sheria itachukua mkondo wake ambapo pia  amewaonya wananchi ambao wanavamia maeneo ya hifadhi na kuwataka  kuondoka mara moja kwa  kuwa  maeneo hayo yaliyohifadhiwa ni  kwa manufaa ya kizazi cha sasa na baadaye.




Naye Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Huduma za Misitu Nchini (TFS)  Prof. Dosantos Silayo  akizungumza kwa  niaba ya Watendaji Wakuu wa Taasisi bza Uhifadhi zilizo chini nya Wizara  hiyo amemweleza  Mhe. Mchengerwa  kuwa  kumekuwa na  mafanikio makubwa  kutokana na uhifadhi.


Ameyataja  baadhi  ya mafanikio hayo kuwa ni pamoj a na  kuimarika kwa uhifadhi, kuongezeka  kwa maeneo  ya uhifadhi, kuongezeka kwa upandaji wa miti na mashamba ya misitu pamoja na  kuwepo kwa miundombinu ya utalii ambayo imesaidia kuwavuta watalii kutembelea  katika maeneo hayo.


Chuo cha Mafunzo ya kijeshi  Mlele ni chuo kilicho chini ya Wizara ya Maliasili na Utalii, kinatoa mafunzo  ya kijeshi kwa Maafisa na Askari wa Jeshi la Uhifadhi.




No comments: