DC NASSARI AWATAKA WAFUGAJI KUPUNGUZA MIFUGO, AKABIDHIWA KITABU CHA MAARIFA YA ASILI KATIKA UHIFADHI - MAIPAC MEDIA TANZANIA

Breaking

MAIPAC MEDIA TANZANIA

A Centre for Indigenous and Pastoralists Community Informations




Thursday, 13 April 2023

DC NASSARI AWATAKA WAFUGAJI KUPUNGUZA MIFUGO, AKABIDHIWA KITABU CHA MAARIFA YA ASILI KATIKA UHIFADHI

 

Mkuu WA Wilaya ya Monduli Joshua NASARI Kulia akipokea kitabu Cha maarifa ya ASILI KATIKA UTUNZAJI WA MAZINGIRA KILICHOANDALIWA na MAIPAC anayemkabidhi ni Mkurugenzi wa Maipac Mussa Juma 


Mwandishi wetu,Monduli


maipacarusha20@gmail.com


Mkuu wa wilaya ya Monduli,Joshua Nassari amewataka  wakazi wa Monduli  kupunguza idadi ya mifugo yao, Ili kutoathirika zaidi na  mabadiliko ya tabia nchi, ambayo yanaendelea kupunguza malisho ya mifugo yao.


Amesema wafugaji hao wanapaswa kuuza sehemu ya mifugo Ili kusomesha watoto badala ya kuwaacha machungani.


Wafugaji wilaya ya Monduli mkoa wa Arusha,mwaka  2021/22 walipata  hasara ya sh 18.3 bilioni baada ya mifugo yao 127,786 kufa kutokana na ukame ambao umesababishwa na mabadiliko ya tabia nchi.




Licha wa wafugaji kupata hasara hiyo,pia serikali wilaya ya Monduli,  ilipoteza Kodi na tozo kiasi cha sh 487.3 milioni ambazo zimekusanywa katika minada na masoko  kama mifugo hiyo isingekufa.


Akizungumza na Viongozi wa shirika la wanahabari la kusaidia jamii za Pembezoni(MAIPAC)  baada ya kukabidhiwa kitabu cha maarifa ya asili katika utunzwaji wa Mazingira,vyanzo vya maji na misitu kilichoandaliwa na MAIPAC kwa udhamini wa shirika la maendeleo la umoja wa mataifa (UNDP) kupitia program ya miradi midogo inayodhaminiwa na mfumo wa Mazingira duniani (GEF) alisema ni muhimu jamii za wafugaji kubadilika.


"nawaomba  wafugaji tukubali kubadilika  na kupunguza mifugo na fedha ambazo zitapatikana tusomeshe watoto kwani mazingira ya sasa sio rafiki katika ufugaji wa mifugo mingi"alisema


Nassari alisema kuna ushindani mkubwa hivi sasa duniani ambao unahitaji kuwa na vijana wenye elimu nzuri ambao wataweza kupambana katika soko la ajira lakini pia kuongeza ubunifu katika utekelezwaji wa miradi mbali mbali.



Awali Mkurugenzi wa MAIPAC Mussa Juma amesema kitabu hicho ni sehemu ya mradi wa Uhifadhi wa Mazingira vyanzo vya maji na misitu kwa maarifa ya asili.


Amesema mradi huo umetekelezwa katika wilaya za Monduli, Longido na Ngorongoro ambapo wazee wa Mila, wanawake na vijana wameshiriki katika kutoa simulizi za maarifa ya asili.


Amesema katika mradi huo pia viongozi wa Halmashauri, viongozi wa vijiji na viongozi wa Mila walishirikishwa katika utoaji wa maarifa ya asili lakini pia kupata mbinu za kuunganisha maarifa ya asili na maarifa ya kisiasa katika uhifadhi wa Mazingira.


Mradi huo ambao ulikuwa unaratibiwa na Jumuiko la Maliasili Tanzania (TNRF) ulizinduliwa na Mkuu wa mkoa Arusha John Mongela ambapo pia kitabu cha maarifa ya asili kilizinduliwa na Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais Mazingira na Muungano Dk Selemani Jafo.

 

No comments: