Na. Mwandishi wetu Jeshi la Polisi.
Wafanyabiashara wa mifugo nchini wametakiwa kufuata sheria, kanuni na taratibu zilizowekwa za kununua na kuuza mifugo ili kuepusha changamoto ambazo zinaweza kujitokeza hususani za kununua mifugo ya wizi.
Hayo yamesemwa leo na Kamanda wa Kikosi cha Kuzuia Wizi wa Mifugo Nchini Kamishna Msaidizi wa Polisi ACP Simon Pasua wakati alipotembelea mnada wa kimataifa wa Pugu pamoja na Machinjio ya Vingunguti Jijini Dar es Salaam kwa lengo la kuhakikisha mifugo yote inayouzwa ni halali kuelekea sikukuu ya Pasaka.
ACP Pasua amewataka wafugaji na wafanyabiashara wa mifugo kuhakikisha wanapelekea mifugo yao katika minada ya Serikali ili kudhibiti matukio ya wizi.
Sambamba na hilo pia ametoa onyo kwa wafanyabiashara wachache ambao wanakwepa kupeleka mifugo maeneo ya minada kuacha mara moja kwani jeshi hilo litaendelea kuwakamata na kuwachukulia hatua za kisheria.
Pia ametoa wito kwa wafanyabiashara kutoa ushirikiano kwa jeshi la Polisi kama kutatokea tukio la wizi wa mifugo.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa wafanyabishara wa Mifugo katika machinjio ya Vingunguti Bwana Joel Meshack amesema kutokana na elimu na maelekezo waliyoyapata changamoto mbalimbali zilizokuwa zinawakabili zinaenda kutatuliwa.
Naye Daktari Mkuu wa Mifugo katika Mnada wa Pugu Bwana Ayoub Mollel amesema mara zote wamekua wakishirikiana na Jeshi la Polisi kwa kukamata na kuzui mifugo yote inayobainika kuwa ni ya wizi katika mnada huo.
No comments:
Post a Comment