Mazingira safi na Chakula Cha mchana kinavyosaidia ufaulu wa wanafunzi shule za Msingi Mkoani Pwani - MAIPAC MEDIA TANZANIA

Breaking

MAIPAC MEDIA TANZANIA

A Centre for Indigenous and Pastoralists Community Informations




Tuesday 6 June 2023

Mazingira safi na Chakula Cha mchana kinavyosaidia ufaulu wa wanafunzi shule za Msingi Mkoani Pwani

Wanafunzi WA shule ya Msingi Mnindi wakigaiwa chai shuleni hapo ili kukabiliana na njaa

 



NA: JULIETH MKIRERI


maipacarusha20@gmail.com


UTORO na ufaulu duni kwenye baadhi ya shule umekuwa ukielezwa kusababishwa na mazingira mabaya kwa kuwa na miundombinu chakavu na isiyokidhi mahitaji ya wanafunzi pamoja na njaa.

Baadhi ya maeneo katika shule za Msingi wanafunzi wanakwama kwenda shule kutokana na kuchoka kukaa chini lakini pia wengine kukosa fedha ya kununulia chakula wakiwa shule.

Ili kukabiliana na mambo hayo Serikali imekuwa ikihamasisha uongozi wa shule kushirikiana na walimu kuandaa mikakati ya kukabiliana na vikwazo hivyo ambavyo vinashusha ufaulu kwa wanafunzi na kudumaza maendeleo kwenye maeneo husika.

Jitihada hizo zimeanza kutekelezeka kwenye baadhi ya shule na kuwafanya wanafunzi kupenda kusoma kwa bidi na kuongeza ufaulu kwa shule na Wilaya zao.

Hali hiyo imeonekana pia katika shule ya Msingi Mnindi ambayo ipo katika Kata ya Vigwaza Halmashauri ya Chalinze Wilaya ya Bagamoyo Mkoani Pwani.

Shule hii ambayo kwasasa ina wanafunzi 268 wavulana wakiwa 135 na  wasichana 133 ni kati ya shule ambazo zinapambana na kutokomeza utoro shuleni na kuinua kiwango cha ufaulu kwa wanafunzi.

 

Mwenyekiti wa Kijiji cha Mnindi Juma Chambwewe anaeleza kuwa awali shule hiyo ilikuwa na ufaulu duni huku ikishika nafasi ambazo zilikuwa haziridhishi katika ngazi ya Wilaya jambo ambalo liliwafanya wanakijiji kubuni mbinu ya kukabiliana nalo.

“Tulitafakari wapo wanafunzi wanatoka nyumbani hawajapata chochote na hawapewi fedha ya kununulia vyakula wawapo shule kutokana na familia wanazotoka kwa hali hii hawezi kumsikiliza vizuri mwalimu anapofundisha” anasema.

Chambwewe anaieleza kuwa walilazimika kukaa kikao wakazi wa Kijiji hicho na kujadili njia ya kuwakwamua wanafunzi kwa kuwezesha upatikanaji wa chakula shuleni.

“Baada ya kukutana tulikuwa na wazo la kuonana na Mkandarasi aliyejenga barabara ya Kwala kuelekea Bandari kavu, tumfikishie ombi letu la kuchangia chakula kwa wanafunzi”

Anasema baada ya wazo hilo kupita walilifikisha kwa mkandarasi huyo wa kampuni ya ESTIM ambaye alikubali na kuanza kutoa fedha kwa ajili ya chakula cha watoto shuleni.

“Wazo letu lilikubaliwa tangu mwaka 2021 na Mkandarasi huyo wa ESTIM alikuwa akitoa fedha kila wiki ambazo tulizitumia kununua mayai, ndizi  mbivu mbili na maziwa vyakula ambavyo walikuwa wanapewa kwa nyakati tofauti ilimradi wasishinde na njaa wakiwa shuleni” anaeleza.

Kwa mujibu wa Mwenyekiti huyo utoro ulianza kupungua katika shule hiyo na uandikishaji kuongezeka kutokana na chakula walichokuwa wakipatiwa wanafunzi lakini pia uboreshaji wa miundombinu ya madarasa uliofanyika .

Anasema baada ya kuanza kupata ushuhuda wa mabadiliko ya ufaulu kwa wanafunzi wanakijiji walikutana tena na kujadili kwa pamoja namna ya kuongeza chakula kingine na kuacha kutegemea msaada pekee kutoka kwa mfadhili huyo .

Anaeleza kuwa walikubaliana kuanza kulima zao la mtama kwenye shamba la Mkandarasi huyo ambaye bado hajaanza kulitumia kwa malengo yake.

“Nilitafuta mbegu ya  mtama tukapanda kwenye shamba la Mkandarasi huyu ambalo sasa wanafunzi wameanza kuvuna na kunufaika na uji shuleni na hakuna tena mwanafunzi anayeshinda njaa”

Anaeleza kuwa tofauti na ilivyo kwa shule nyingine ambazo wazazi wengine wanachanga sh. 500 au Zaidi kila siku ili mwanafunzi apate chakula wazazi wa shule hiyo wanalazimika kuchangia kiasi cha sh. 700 kwa mwezi kwa ajili ya kuwalipa wapishi.

“Mchango wa Halmashauri ya Kijiji chetu tumenunua vyombo vya kupikia ikiwemo masufuria na vikombe huku mchango wa mkandarasi ukiendelea kutolewa kila wiki na ndizi mbivu na vitu vingine tunaendelea kununua na kuwapatia wanafunzi” anaeleza.

Hata hivyo pamoja na yote hayo yanayofanywa na uongozi wa Kijiji hicho pia wanampango wakulima shamba la shule na kupanda mazao mengine pindi Mkandarasi atakapochukua shamba wanalotumia kwa sasa.

Aidha ili kunusuru wanafunzi wasishinde njaa Kijiji hicho kimejipanga kwa mtama ambao unaendelea kuvunwa kwasasa gunia mbili zitatengwa ili kila mwananchi atapatiwa mbegu ya mtama apande katika shamba lake na ikitokea uhaba wa chakula shuleni iwe rahisi kila mzazi kuchangia.

Mwenyekiti huyo anaeleza mipango mingine yam waka 2024/2025 kuwa ni kupeleka maombi kwenye chama cha wakulima wa Umwagiliaji Ruvu (CHAURU) kwa ajili ya kukodi shamba na kulima zao la mpunga huku mipango hiyo ikienda sambamba na kulima maharage kwa kutafuta shamba mikoa ya jirani.

“Mipango yote hii ni yam waka 2024/2025 lengo letu chakula kisikosekane shuleni na pia wasiwe na chakula cha aina moja wapate cha kubadilisha kwa kufanya hivi tunaamini hakuna mwanafunzi atakayekuwa mtoro na ufaulu katika shule yetu utakua” anabainisha Chambwewe.

Akizungumzia hali ilivyo kwa sasa Mwalimu Mkuu wa shule ya Msingi Mnindi Kelvin Selekwa anasema kwa mwaka 2023 makadirio ya uandikishaji kwa darasa la awali yalikuwa ni 57 lakini walioandikishwa walifikia 63 sawa na asilimia 111.

Selekwa anasema kwa upande wa darasa la kwanza makadirio yalikuwa 47 na mapaka sasa wameandikishwa wavulana 22 na wasichana 47 sawa na asilimia 100.

“Ongezeko kwa darasa la awali ni asilimia 11 ambalo limechangiwa na chakula kinachotolewa kwa wanafunzi pamoja na ushirikiano kati ya walimu na wazazi” anasema.

Selekwa anaeleza kuwa ufaulu kwa wanafunzi wa darasa la saba  mwaka 2021 na 2022 ni wa asilimia 100 ambao umechangiwa na mazingira mazuri ya kufundishia na ujifunzaji, huduma ya chakula inayotolewa shuleni.

Mwalimu mkuu huyo anaeleza kuwa hali ya utoro kwa mwaka 2022 ilikuwa ya wastani wa asilimia 12 na kwamba imepungua hadi kufikia asilimia saba kwa mwaka 2023. 

Anaeleza kuwa kupungua kwa utoro huo umechangiwa na huduma ya chakula inayotolewa shuleni pamoja na ushirikiano uliopo kati ya walimu na wazazi wa wanafunzi.

Selekwa anasema utoaji wa chakula shuleni ulianza baada ya kuwashirikisha wadau mbalimbali akiwemo Mkandarasi wa Kampuni ya Ujenzi ya ESTIM pamoja na uongozi wa Serikali ya Kijiji cha Mnindi.

“Kwa msaada wa wadau hao tumefanikiwa kulima ekari 40 za mtama ambazo ziko katika hatua ya uvunaji na uchangiaji wa chakula wazazi wanajitahidi ingawa si kwa kiasi kikubwa” anaeleza Mwalimu huyo.

Akizungumzia hali ilivyokluwa awali Selekwa anasema utoro kwa wanafunzi ilikuwa ikichangiwa na hali duni ya wazazi kumudu kuwapatia huduma muhimu watoto kama chakula pamoja na mwamko mdogo .

Selekwa anaelezea mikakati ya shule hiyo kuwa ni pamoja na kuhakikisha chakula kinapatikana mwaka mzima wa masomo, kutoa elimu ya kutosha kwa wazazi kuhusiana na umuhimu wa elimu kwa watoto wao .

Mikakati mingine ni kuzidisha ushirikiano kwa walimu na wazazi na kuhakikisha shule inakuwa na kilimo cha chakula endelevu.

Diwani wa Vigwaza Mussa Gama anapongeza jitihada zinazofanywa na Mkandarasi wa ESTIM ambapo pamoja na kusaidia upatikanaji wa chakula katika shule hiyo pia amejenga vyumba vitatu vya madarasa kukabiliana na uhaba wa miundombinu katika shule hiyo.

Gama anasema uhanmasishaji wa chakula shuleni katika kata ya Vigwaza unaendelea na shule nyingi zimeanza kutoa chakula kunusuru watoto kusoma wakiwa na njaa.

Anasema matarajio ya Kata hiyo ni kukuza ufaulu kwa wahitimu kupitia utakalezaji wa kutatua vikwazo katika sekta ya elimu na kuhakikisha kila mwanafunzi anayehitimu darasa la saba anajiunga na sekondari.

Kijiji cha Mnindi pia kinaelezwa kuanzisha utaratibu wa motisha kwa wanafunzi wanaofaulu katika shule hiyo na kupitia utaratibu huo pia umechangia kuinua kiwango cha ufaulu.

No comments: