Mawakili, wananchi wacharuka kukamatwa mbunge wa Ngorongoro na wananchi 31 - MAIPAC MEDIA TANZANIA

Breaking

MAIPAC MEDIA TANZANIA

A Centre for Indigenous and Pastoralists Community Informations




Wednesday 23 August 2023

Mawakili, wananchi wacharuka kukamatwa mbunge wa Ngorongoro na wananchi 31





Mwandishi wetu, MAIPAC

maipacarusha20@gmail.com


Baadhi ya wananchi wa Ngorongoro pamoja na mawakili wao,wamecharuka kuendelea kushikiliwa na polisi mbunge wa Jimbo Hilo, Emmanuel OleShangai na wananchi 31.


Wakizungumza na waandishi wa habari katika hoteli ya leonsi Jijini Arusha, baadhi ya wakazi wa Ngorongoro wakiwepo madiwani na mawakili wamesema wanapinga kuendelea kukamatwa wananchi hao bila kufikishwa mahakamani.


Wakili Joseph Oleshangay amesema ambacho kinaendelea Ngorongoro hakikubaliki na ni ukiukwaji wa sheria.


"Wamekamata watu tangu Agosti 16 Hadi Leo hawajafikishwa Mahakamani na wamekuwa wakiteswa kwa tuhuma za kujeruhi lakini pia wanahojiwa kuhusu kuhamia Msomera"amesema


Amesema sheria ipo wazi ndani ya  masaa 24 baada ya Watuhumiwa kukamatwa wanapaswa kufikishwa Mahakamani lakini kinachoendelea sio sahihi.


"Binafsi nimezungumza na wote waliokamatwa wamepigwa na wengine ni wagonjwa Sasa kama wanatuhumiwa kwa kujeruhi kwanini na wao wanajeruhiwa "amesema


Amesema hawapingi kukamatwa watu na hawapingi Jeshi la polisi kufanyakazi zao lakini wanachopinga ni kukiukwa sheria.


"Kinachofanyika ni kuwatisha wananchi wasiendelee kuzungumza kuhusu Haki zao Sasa hatukubaliani" alisema


Ole Shangay ambaye pia ni mkazi wa Enduleni Ngorongoro alisema wanataka sheria na taratibu kufuatwa kama watu wamefanya makosa basi sheria zichukuwe mkondo wake .



Naye Wakili Alais Melau alisema kuendelea kushikiliwa wananchi wa Ngorongoro wakiwepo wagonjwa ni makosa.


Melau alisema Kati ya walioshikiliwa Kuna mmoja ambaye ni mgonjwa wa kifua kikuu na alikamatwa akiwa anatoka kuchukuwa dawa.


"Huyu mgonjwa analalamika alitakiwa kupata dawa lakini hapati na kibaya zaidi hatakiwi kuchanganywa na watu lakini hadi jana amewekwa sero Moja na watu zaidi ya 20"alisema.


Alisema wanaomba Watuhumiwa kuachiwa au kufikishwa Mahakamani.


Hata hivyo Hadi jana mbunge wa Ngorongoro Emmanuel OleShangay alikuwa hajulikani alipo baada ya kujisalimisha kituo cha Polisi Karatu na baadaye kuondolewa usiku juzi.


Kamanda wa polisi mkoa Arusha Justine Masejo hajapatikana kuzungumzia tukio Hilo kutokana na kuwepo katika ugeni wa viongozi wa kitaifa mkoani Arusha.




No comments: