Waziri MCHENGERWA: awaalika watalii kushuhudia maajabu ya nyumbu wa Serengeti - MAIPAC MEDIA TANZANIA

Breaking

MAIPAC MEDIA TANZANIA

A Centre for Indigenous and Pastoralists Community Informations




Thursday 24 August 2023

Waziri MCHENGERWA: awaalika watalii kushuhudia maajabu ya nyumbu wa Serengeti

 






Mwandishi wetu, MAIPAC 

maipacarusha20@gmail.com 


Waziri wa Maliasili na Utalii Mhe. Mohamed Mchengerwa  amewaalika Watalii wa ndani na nje ya nchi   kujitokeza kwa wingi kutembelea Hifadhi za Taifa Tanzania ikiwemo Serengeti kushuhudia maajabu ya nyumbu wanaohama Serengeti.


Ameyasema hayo akiwa Kogatende, katika Hifadhi ya Taifa Serengeti baada ya kushuhudia tukio kubwa na la kipekee duniani la uvukaji wa nyumbu Mto Mara pamoja na wanyama wengine. 


   " Nawaasa na kuwakaribisha watanzania kuja kujionea wao wenyewe uvukaji wa nyumbu mubashara. Hili tukio ni la kipekee na la kihistoria".



" Nawapongeza sana kwa jitihada mnazofanya fanyeni kazi kwa bidii na kwa kujituma bila kukata tamaa na wala bila kumwonea mtu. Kazi mnayofanya ni nzuri fanyeni kazi kwa kufuata kanuni, sheria, taratibu na maadili".

 

Aidha, Alimpongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt Samia Suluhu Hassan kwa kuanzisha harakati za kuitangaza nchi yetu kupitia filamu ya The Royal Tour.


"Takwimu zinaonyesha idadi ya watalii imeongezeka,  kwa mfano katika mwaka wa fedha 2022/2023 tulipata zaidi ya watalii milioni 1.6. Matarajio ya wizara ni kiwango hiki kuongezeka zaidi".


Pia, aliwasifia watumishi wa TANAPA kwa Hifadhi ya Taifa Serengeti kushinda tuzo mara nne mfululizo na kuiwezesha kujulikana kimataifa, kuwa miongoni mwa maajabu saba ya dunia pamoja na kuwa na wanyama wengi na wakubwa.


Tukio hili linaloshangaza na kuvuta hisia za watalii wengi duniani la Nyumbu na Pundamilia kuvuka Mto Mara hufanyika kila mwaka kuanzia mwezi Agosti hadi katikati ya mwezi Septemba.


Viongozi wengine waliokuwa wameambata na Waziri Mchengerwa ni Naibu Waziri Mary Masanja, Katibu Mkuu Dkt. Hassan Abbasi, Naibu katibu Mkuu Kamishna Benedict Wakulyamba, wajumbe wa kamati ya Bunge Ardhi Maliasili na utalii, wakiongozwa na mwenyekiti wao  Timotheo Mnzava na watumishi wa wizara.




No comments: