Mkurugenzi JamiiForums ataka wazazi kusomesha watoto elimu bora kwani fursa zipo. - MAIPAC MEDIA TANZANIA

Breaking

MAIPAC MEDIA TANZANIA

A Centre for Indigenous and Pastoralists Community Informations




Monday 4 September 2023

Mkurugenzi JamiiForums ataka wazazi kusomesha watoto elimu bora kwani fursa zipo.


Mkurugenzi Mtendaji wa JamiiForums Maxence Melo akizungumza katika mahafali ya kwanza ya darasa la sana shule ya msingi Patmos Island jijini Arusha

Mkurugenzi wa shule ya Msingi Patmos Island ya jijini Arusha Upendo Mmbaga akizungumza katika mahafali hayo

Na: Andrea Ngobole, MAIPAC

maipacarusha20@gmail.com



Mkurugenzi Mtendaji wa JamiiForums, Ndugu Maxence Melo amewataka wazazi nchini kuwapa watoto wao elimu bora kama urithi ili iwasaidie kupambana na umaskini na kujikwamua kiuchumi.


Akizungumza katika mahafali ya kwanza ya shule ya msingi Patmos Island iliyopo jijini Arusha, Melo amesema bila watoto kupata elimu bora ni vigumu kukabiliana na umasikini na kunufaika na fursa zilizopo.


Amesema yeye binafsi anafahamu umuhimu wa elimu kwani katokea katika familia masikini ambapo elimu ndiyo msingi thabiti iliyomuwezesha kufanikiwa kuanzisha kampuni tatu zilizotoa ajira kwa watu 100.


“Msinione hivi leo nimetokea familia ya chini sana elimu ndiyo iliyonikomboa, wakati nasoma Bwiru Boys nilikuwa natembea umbali mrefu kwenda kuomba msaada wa fedha za kujikimu, nafahamu pia changamoto wanazokutana nazo watoto yatima katika kupata elimu ndiyo maana nina mfuko wa kusaidia watoto wanaotokea mazingira magumu kupata ufadhili wa masomo.” amesema

Maxence Melo akiwa na wahitimu Atukuzwe na Victor waliochaguliwa kuingia katika mfuko wa ufadhili Maxence utakaogharamia masomo yao ya sekondari Hadi chuo kikuu



Amesema anapenda kurejesha kwa jamii kwa kuwapatia Ufadhili watoto wawili waliopendekezwa na shule hiyo, Atukuzwe na Victor ambao ni yatima kuingia katika mfuko wa ufadhili wa Maxence Melo.

Amewataka wahitimu hao kuwa na nidhamu na juhudi ya kutosha katika kupigania ndoto zao za kupata elimu ili kila mmoja aweze kufikia malengo yake aliyojiwekea.

Akijibu risala iliyosomwa na mkuu wa shule hiyo Hadija Shaban na Mkurugenzi wa shule hiyo Upendo Mmbaga, Maxence Melo ameahidi kuwajengea maktaba na chumba cha computer ili watoto wao waweze kupata ujuzi wa matumizi ya computer wakiwa bado shuleni.



Melo amesema ulimwengu kwa sasa umeegemea Zaidi katika teknolojia ya kidigitali na kuna masomo mengi ambayo yana msaada mkubwa kwa jamii hivyo atasaidia shule hiyo kufikia malengo yake.

Awali Mkurugenzi wa shule hiyo Upendo Mmbaga alisema kuwa shule hiyo ilianzishwa mwaka 2012 na Baba yake mzazi Joel Mbaga akiwa na maono ya kusaidia jamii kupambana na umaskini kupitia elimu.


Alisema shule hiyo ilipatiwa usajili wa kufundisha kwa mchepuo wa lugha ya kiingereza mbapo walianza na wanafunzi hao 12 na kwa sasa wana wanafunzi 163 ambapo kati yao wavulana ni 95 na wasichana 68.

Mmbaga amewapongeza wazazi kwa kuwapatia wanafunzi hao elimu bora na kuwaasa waendelee kuwapatia elimu bora ili watoto hao watimize malengo yao na kuwa kichocheo cha mabadiliko ya kiuchumi katika familia, jamii na Taifa kwa ujumla.

“Niwapongeze sana wahitimu kwa elimu mliyoipata hapa imewasaidia kupata mwanga wa maisha yenu ya baadae, kumbukeni safari ya kujifunza Zaidi inawasubiri mfike mbali Zaidi, nawatakia maisha mema yenye tija mkawe na nidhamu sana katika masomo ya sekondari mtakayoanza mwaka 2024.” Alisema

Mratibu elimu Kata ya Olasiti Thomas Martini ameupongeza uongozi wa shule ya Patmos Island kwa kudumisha nidhamu kwa watoto hao, kutumia mitaala ya Tanzania kufundishia elimu ya kujitegemea ambayo ni msingi thabiti wa maendeleo ya kila mmoja.

Amewataka wazazi wa watoto hao kuhakikisha wanakuwa salama kwa kupata elimu ya sekondari na kuwalinda dhidi ya vitendo vyote vya ukatili kwa mtoto ili kuwa na mazingira rafiki ya kujifunzia na kutimiza malengo yao.


Frank Kissamu akizungumza kwa niaba ya wazazi amesema kuwa wanajivutia elimu bora inayotolewa shuleni hapo.


"Binafsi najivunia mwanangu kufanya vizuri shuleni hapo na sasa shule imemjengea uwezo wa kukuza kipawa chake ,kujieleza na kutawala vema jukwaa.

Wahitimu wakisoma risala kwa mgeni rasmi





No comments: