Na. Mwandishi Wetu- Dar es Salaam
maipacarusha20@gmail.com
Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe. Angellah Kairuki (Mb) ameitaka menejimenti ya Mamlaka ya Usimamizi wa Wanyamapori Tanzania (TAWA) kuhakikisha inaongeza makusanyo yake ya mapato ya ndani zaidi ya lengo iliyojiwekea la kukusanya shilingi bilioni 78.4 kwa mwaka wa fedha 2023/2024.
Waziri Kairuki ameyasema hayo leo tarehe 20 Septemba, 2023 katika kikao kati yake na Menejimenti ya TAWA kilichofanyika kwenye ukumbi wa Chuo cha Taifa cha Utalii jijini Dar es Salaam.
“Nataka makusanyo yaongezeke zaidi, hili lengo mlilojiwekea la kukusanya bilioni 78 .4 ni dogo sana” Mhe. Kairuki amesisitiza.
Aidha, ameielekeza TAWA kutafuta wawekezaji wazuri ili kuongeza kasi ya ukusanyaji mapato ikiwa sambamba na kuhamasisha wazawa kuwekeza kwenye maeneo ya uwekezaji mahiri (Special Wildlife Concession Areas - SWICA) yanayosimamiwa na TAWA.
Katika hatua nyingine, Mhe. Kairuki ametoa wiki mbili kwa TAWA na Wakala ya Huduma za Misitu Tanzania (TFS) kutatua migogoro ya umiliki wa maeneo.
“Ndani ya wiki mbili mkakubaliane katika kila eneo ambalo mna mvutano shida ni nini na mnamalizaje,” Alisema Mhe. Kairuki.
Kwa upande wake Kamishna wa Uhifadhi kutoka TAWA, Mabula Misungwi Nyanda amesema amepokea maelekezo yote na kuahidi kuyafanyia kazi sambamba na kutafuta njia bora katika kuongeza mapato.
Kikao hicho kimehudhuriwa na baadhi ya Watendaji kutoka Wizara ya Maliasili na Utalii pamoja na Taasisi zake ikiwemo Mamlaka ya Usimamizi wa Wanyamapori Tanzania (TAWA), Wakala ya Huduma za Misitu Tanzania (TFS), Mamlaka ya Usimamizi wa Eneo la Ngorongoro (NCAA) na Taasisi ya Utafiti wa Wanyamapori Tanzania (TAWIRI).
No comments:
Post a Comment