Na Mwandishi wetu, Geita
maipacarusha20@gmail.com
WAZIRI wa Madini, Anthony Peter Mavunde, amezindua ofisi za kampuni ya GF Trucks & Equipment LTD Mjini Geita na kuipongeza kwa kufungua ofisi hizo zitakazosaidia wachimbaji wadogo wa madini katika kufanikisha shughuli zao.
Waziri Mavunde amezindua ofisi za kampuni hiyo zilizopo katika soko kuu la dhahabu mjini Geita na kukata utepe kwenye malori matatu yaliyonunuliwa na wachimbaji madini.
Mavunde amesema hatua hiyo ni muhimu kwa kushirikiana na sekta ya madini hasa wachimbaji katika kuwapatia vifaa kwani ofisi hizo zitarahisisha shughuli za uchimbaji ili watanzania washiriki kikamilifu katika sekta ya madini.
“GF Trucks nawapongeza kwa kuamua kusogeza huduma karibu na wachimbaji, niwaombe muendelee kutanua wigo, wachimbaji ni waaminifu wanao uwezo mkubwa wa kuchukua mitambo kwa njia ya mkopo na kuirejesha,” amesema Mavunde.
Amelitaka shirika la madini la Taifa (STAMICO) kusimamia vyema makubaliano hayo ili wachimbaji mchanga na wenye leseni ya madini ya ujenzi waondokane na changamoto ya kushindwa kupakia mashapo kwa kukodisha malori.
"Wachimbaji wadogo wanakusanya madini ya ujenzi ila mwenye gari anapata mara tatu zaidi ya mwenye leseni, tukimsaidia katika mnyororo wa thamani atanufaika," amesema Mavunde.
Mkurugenzi wa masoko na Biashara wa kampuni ya GF Trucks, Salman Karmali, amesema walianza kufanya upanuzi wa kiwanda kwa lengo la kuanza kuunganisha magari madogo na mwaka huu wanatarajia kuunganisha magari 1,500.
Amesema wameingia makubaliano na Shirika la Madini la Taifa (STAMICO) ambalo lina vifaa vya kuchoronga na kufanya tafiti huku kampuni hiyo ikitoa mashine na maroli.
Karmali amesema wamekubaliana kuweka mashine karibu na wachimbaji ili kuwa karibu na wachimbaji wadogo.
Amesema Geita inategemea uchimbaji kwa asilimia kubwa na wao GF Trucks wanategemea ushirikiano wa wachimbaji hao kwani magari wanayouza ni matunda mazuri ya Serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Rais Samia Suluhu Hassan kwa kuweka mazingira mazuri kwa wawekezaji.
"Tunajivunia kiwanda chetu kilichopo Kibaha Mkoa wa Pwani ambacho ni kiwanda pekee cha kuunganisha magari,” amesema Karmali.
Mkurugenzi wa STAMICO Dkt Venance Mwasse amesema miongoni mwa mambo waliyokubaliana ni kusogeza huduma sehemu za wachimbaji na kuwauzia au kuwakodishia vifaa.
“Tukio la leo ni utekelezaji wa miongoni mwa mambo ambayo tulikubaliana, jambo lingine tulilokubaliana ni kukodisha vifaa pamoja na kuuza," amesema Dkt Mwasse.
Amesema sekta ya madini inahitaji mtaji mkubwa au uwekezaji mkubwa, ila inahitaji muda mrefu na ukimuangalia mchimbaji mdogo siyo lazima awe na resource (rasilimali) nyingi, anaweza akachimba bila kuwa na uwekezaji wa muda mrefu.
“Kwa hiyo tukaona tukae pamoja tujadiliane tuone namna ya kumrahisishia mchimbaji mdogo asipate presha ya kuwa na mtaji mkubwa wa kumiliki trucks, buldoza ndiyo aweze kuchimba,” amesema Dkt Mwase.
No comments:
Post a Comment