Madarasa mapya ya shule ya Msingi Kibohehe yaliyojengwa na Ubalozi wa Japan nchini Tanzani |
Shule ya zamani ambayo madarasa yake yaliezuliwa na upepo mkali na kusababisha kifo Cha Mwanafunzi February 21 mwaka 2018 |
Na: Andrea Ngobole
maipacarusha20@gmail.com
Balozi wa Japan nchini Tanzania YASUSHI MISAWA Amekabidhi vyumba vya madarasa 8 na ofisi mbili za walimu Vyenye thamani ya shilingi milioni 204 Kwa shule ya Msingi Kibohehe iliyopo wilayani Hai mkoani Kilimanjaro.
Vyumba hivyo vimejengwa na Ubalozi wa Japan nchini Tanzania kufuatia kuanguka kwa darasa na kusababisha kifo Cha Mwanafunzi Mmoja mwaka 2018
Balozi wa Japan nchini Tanzania Yusush Misawa, akizindua madarasa hayo na pembeni ni Mkuu wa Wilaya ya Hai Amiri Mkalipa |
Akikabidhi madarasa hayo Leo October 17 shuleni hapo Balozi YASUSHI MISAWA Amesema kuwa wanayo furaha kubwa kutimiza Ujenzi wa Madarasa hayo na kuwawezesha wanafunzi kusoma katika mazingira mazuri na salama ya kusoma na kujifunza.
Amesema Lilikuwa ni tukio la kusikitisha sana mnamo Februari 2018, jengo la shule hiyo liliporomoka kutokana na mvua kubwa iliyonyesha na kusababisha madhara makubwa katika jamii ya Kijiji cha Roondoo ambapo Wanafunzi wengi walilazimika kwenda shule nyingine ya mbali kusoma.
Hata hivyo ulikuwa uamuzi mzuri kwamba wafanyakazi wa kujitolea wa shirika la kimataifa la msaada la Japan (JICA) ambao walifanya kazi katika Halmashauri ya Wilaya ya Hai, walipoona hali mbaya na matatizo ya watoto wengi na wazazi wao na walipendekeza kwamba jengo la shule lijengwe upya kwa kutumia mpango wa misaada wa GGHSP.
"Leo, nina furaha kuona jengo jipya la madarasa limekamilika kwa mafanikio na zaidi ya wanafunzi 200 wanafurahia kusoma hapo." Alisema balozi YASUSHI MISAWA
Amewasihi walimu na wanafunzi wa shule hiyo kutumia ipasavyo na kudumisha ipasavyo madarasa hayo kwa muda mrefu ili kuchangia maendeleo zaidi ya watoto wa kijiji hicho.
Amewashukuru wakazi wa kijiji hicho kwa kushiriki kwa namna moja ama nyingine kufanikisha Ujenzi wa Madarasa hayo
Amesema Serikali ya Japan imekuwa ikitoa misaada ya mara kwa mara katika mikoa mbalimbali nchini Tanzania na anaamini kuwa kukabidhi madarasa hayo ni hatua nyingine katika kuimarisha uhusiano mzuri uliopo kati ya Tanzania na Japan.
Awali Mkuuu wa Wilaya ya Hai Amiri Mkalipa akimkaribisha balozi aliishukuru Serikali ya Japan kwa msaada huo wa Ujenzi wa shule nzima na kuwawezesha wanafunzi kusoma katika mazingira mazuri.
"Mheshimiwa Balozi tunakushukuru wewe na Serikali ya Japan kwa msaada huu muhimu wa Ujenzi wa shule nzima ya Kibohehe mara baada ya madhila yale tuliyopata mwaka 2018, madarasa haya yarakuwa chachu ya maendeleo katika sekta ya Elimu" Alisema Mkuu wa wilaya
Mapema Akisoma ripoti ya Ujenzi wa Madarasa hayo Mkuu wa shule hiyo Alisema ilikuwa ni huzuni kubwa tarehe 21 February, 2018 baada ya mvua kubwa kunyesha na kuezua paa na kuangusha ukuta wa darasa uliosababisha kifo Cha Mwanafunzi Mmoja Derick Albert na kujeruhi wanafunzi wengine watano na kuleta simanzi kubwa kijijini hapo, Hali iliyopelekea kufungwa Kwa shule hiyo na kuwahamishia wanafunzi wote katika shule za jirani.
Amesema shule hiyo ina wanafunzi 224 ambapo wavulana ni 109 na wasichana 115 Ina walimu 9 kati yao mwalimu wa kiume ni Mmoja na nane ni wanawake.
Balozi wa Japan yupo katika ziara ya kukagua Miradi inayofadhiliwa na Serikali ya Japan pamoja na shirika la kimataifa la msaada la Japan (JICA) katika Mikoa ya Kilimanjaro na Arusha.
No comments:
Post a Comment