Timu za Macklion FC na Macedonia zatinga robo fainali Chemchem CUP 2023 - MAIPAC MEDIA TANZANIA

Breaking

MAIPAC MEDIA TANZANIA

A Centre for Indigenous and Pastoralists Community Informations




Monday, 9 October 2023

Timu za Macklion FC na Macedonia zatinga robo fainali Chemchem CUP 2023








Na Mwandishi Wetu, Babati

maipacarusha20@gmail.com

Mabingwa watetezi wa Kombe la chemchem timu ya Macklion FC ya kijiji cha Mwada wilayani Babati, mkoa wa Manyara imekuwa timu ya kwanza kutinga robo fainali ya michuano ya chemchem cup mwaka 2023 baada ya kuongoza katika kituo cha Mwada.


Michuano hiyo, ambayo inaandaliwa kila mwaka na Taasisi cha chemchem ambayo imewekeza shughuli za uhifadhi na Utalii, katika eneo la Jumuiya ya hifadhi ya wanyamapori Burunge, lengo lake ni kupiga vita ujangili wa Twiga .


Mkurugenzi wa chem chem Association, Fabia Bausch alisema katika michuano ya mwaka huu, kiasi cha zaidi ya shilingi 99 milioni kinatarajiwa kutumika katika kuendesha michuano hiyo, na kugharamia zawadi kwa washindi, vikombe na kila timu ambayo inashiriki imepewa seti ya jezi na mpira.


Katika michuano hiyo, mwaka huu timu 33 zinashiriki, ikiwepo za wanawake na vijana ambapo bingwa wa soka akipata zawadi ya sh 2.5 milioni,upande wa wanawake 1.5 na vijana sh milioni moja huku pia washindi wa pili hadi wa tatu watapewa zawadi.


Timu ya Macklion FC imeungana na timu ya Macedonia FC ya kijiji cha Ngolei wilayani Babati, kutinga robo fainali baada ya kuzinyanyasa timu za Star Boys na Mwada na Tembo FC ya Sangaiwe.


Katibu wa chem chem Cup John Bura amesema Macklion imetinga robo fainali baada ya kushinda michezo yake mitatu, ikiwepo kuwachapa Macedonia 1-0 katika mchezo mkali ambao ulichezwa uwanja wa vilima vitatu.


Katika mchezo huo, goli pekee la Macklion lilifungwa na Marwa Abdallah Dk ya 22 baada ya kombora lake kumzidi kipa wa Macedionia FC Jackson Muna.


Katika michezo ya timu za watoto wenye umri chini ya miaka 18 timu za vijana za Mack Lion na Macedonia pia zimeshinda kuingia robo fainali.


Bura alisema timu nyingine katika michuano hiyo, zipo katika kanda ya Magara na Ngaiti ambapo pia timu mbili kila kundi zitaingia robo fainali ,michezo ambayo itachezwa katika viwanja vya Mdori ,wilayani Babati.


Michuano hiyo, ilizinduliwa na Mkuu wa mkoa Manyara, Queen Sindiga ambaye aliwakilishwa na Mkuu wa wilaya ya Babati, Lazaro Twange Septemba 30 ambapo pia zawadi mbali mbali zilitolewa na chem chem ikiwepo baiskeli kwa walemavu.




No comments: