Ezekiel Sumare akisoma tamko mbele ya waandishi wa Habari |
Arkayai Osiringeti akielezea madhila yanayowakumba wakazi wa eneo lake |
Na: Mwandishi wetu, Arusha
Maipacarusha20@gmail.com
Vijana jamii ya kimasai toka wilaya ya Ngorongoro wameiomba serikali kusitisha ukamataji wa mifugo na kuachilia mifugo 1,727 wanayoishikilia kwa madai ya kuingia katika pori tengefu la Pololeti.
Vijana hao, wameeleza tayari mahakama ilikwishabatilisha matumizi ya pori hilo na kuruhusu wafugaji kutumia kwa ajili ya malisho ya mifugo.
Mifugo hiyo inayoshikiliwa ni Ng’ombe 754 za wakazi wa kata ya Ololosokwan, na kata ya Arash Ng’ombe 327, Mbuzi na kondoo 645
Akisoma taarifa ya wananchi wa Loliondo mbele ya waandishi wa habari jijini Arusha October 10 Ezekiel Sumare kwa niaba ya vijana wenzake amesema kuwa kumekuwa na kutokuheshimiwa kwa amri ya mahakama kwa baadhi ya watendaji wa serikli wilayani humo.
Amesema kwamba baada ya mahakama kutoa amri ya kusimamisha tangazo la Rais namba 604 ya mwaka 2022, watumishi wa pori hilo wamendelea kukamata na kushikilia mifugo katika sehemu mbalimbali za Loliondo ambapo jumla ya mifugo inayoshikiliwa ni 1,727 wakiwepo Ng’ombe ni 1,081, Mbuzi 345 na kondoo 300 kwa madai ya kuingia katika pori la Pololeti.
Sayori Latajewo amesema kuwa mahakama iliweka wazi kuwa pori hilo la Pololet Wananchi wa Loliondo wana haki ya kutumia kwa ajili ya kulisha mifugo yao na kimsingi wananchi wanatekeleza kile ambacho Mahakama imeridhia ila wanashangaa kwa nini mifugo inakamatwa.
Arkayai Osiringeti mkazi wa Arash amesema kuwa wananchi wanateseka kwa kushikiliwa kwa mifugo yao kwa siku ya nne mfululizo kinyume cha sheria na mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro na kuwataka waiachie bila masharti yeyote.
Vijana hao wamesisitiza kuwa mihimili yote ya nchi itambue ya kwamba wananchi wa Ngorongoro tarafa ya Loliondo wana uhuru wa kufanya shughuli za malisho ya mifugo baada ya hukumu ya mahakama kwenye maombi ya kesi ya jamii juu ya GN 604 kwenye kesi namba 178 ya mwaka 2022 ambayo iliitaka jamii kutosumbuliwa kwenye eneo la Pololeti.
No comments:
Post a Comment