WANAWAKE WA MAGONGA TANZANITE WATEMBELEA MAONYESHO YA MADINI GEITA - MAIPAC MEDIA TANZANIA

Breaking

MAIPAC MEDIA TANZANIA

A Centre for Indigenous and Pastoralists Community Informations




Monday, 2 October 2023

WANAWAKE WA MAGONGA TANZANITE WATEMBELEA MAONYESHO YA MADINI GEITA

 




Na Mwandishi wetu, Geita


maipacarusha20@gmail.com


WANAWAKE wanaofanya biashara ya madini ya Tanzanite Mji mdogo wa Mirerani Wilayani Simanjiro Mkoani Manyara, kupitia magonga wametembelea maonyesho ya sita ya kimataifa ya teknolojia ya madini Mjini Geita.


Diwani wa Kata ya Mirerani Salome Mnyawi na Mwenyekiti wa wanawake wa Magonga Mirerani (MIWOTAMA) Joyce Mkilanya wamewaongoza wanawake hao katika ziara hiyo.


Diwani wa Kata ya Mirerani, Salome Nelson Mnyawi amewapongeza wanawake hao kwa kushiriki maonyesho hayo ya sita ya kimataifa ya teknolojia ya madini mjini Geita.


"Wanawake ni jeshi kubwa, niwapongeze wamama wa magonga kwani wametoka mbali kwa kupita mamia ya kilomita kutoka Manyara hadi Geita kushiriki maonyesho haya," amesema Salome.


Mwenyekiti wa wanawake hao wa magonga (MIWOTAMA) Joyce Mkilanya amesema lengo la ziara hiyo ni kujifunza namna wanawake wa dhahabu wanavyofanya na pia wanawake wa dhahabu wajifunze kwa wanawake wa Tanzanite.


"Wanawake wa Tanzanite tumepiga hatua kubwa na tumeona wanawake wa dhahabu wamefanikiwa pia hivyo tunakutana na kupeana uzoefu ili kila mmoja ajifunze kwa wenzake na kupata wanawake marafiki," amesema Mkilanya.


Mmoja kati ya wanawake wanaofanya biashara ya magonga hayo Veronica Charles amesema amefurahia ziara hiyo kwani imewajengea uwezo zaidi katika shughuli zao.


Maonyesho ya sita ya kimataifa ya teknolojia ya madini yamefanyika kwa muda wa siku saba kwenye kituo cha uwekezaji cha EPZA Bombambili mjini Geita na kushirikisha wadau zaidi ya 300 wa nchi mbalimbali ikiwemo Tanzania, Kenya, Malawi, Zambia, DRC Congo, Uganda, Rwanda na Burundi.



No comments: