Kinana achangisha mamilioni Jukwaa la vijana wa Kiislamu Mkoa Arusha - MAIPAC MEDIA TANZANIA

Breaking

MAIPAC MEDIA TANZANIA

A Centre for Indigenous and Pastoralists Community Informations




Sunday 24 December 2023

Kinana achangisha mamilioni Jukwaa la vijana wa Kiislamu Mkoa Arusha

  





Na: Mwandishi wetu , MAIPAC

maipacarusha20@gmail.com


Makamu Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi Tanzania Bara (CCM) Abdurahman Kinana amechangisha zaidi ya shilingi milioni 20.7 za ujenzi wa Kituo cha Kiislamu Mkoa Arusha.


Kituo hicho, ambacho kitakuwa na Chuo Cha Ufundi, kitajengwa eneo la Nduruma wilayani Arumeru mkoani Arusha na Jukwaa la vijana wa Kiislamu.


Katika harambee  hiyo, iliyofanyika kituo cha mikutano Cha Kimataifa Arusha, ambayo ilikwenda sambamba na maadhimisho ya miaka 10 tangu kuanzishwa Jukwaa hilo, Kinana alichangia sh 5 Million na kuahidi kuendelea kuchangia atakapokutana na marafiki zake.

Mkuu wa Mkoa wa Arusha John Mongela kulia  akichangia jukwaa Hilo la vijana wa kiislamu


Katika harambee hiyo, Mkurugenzi wa Taasisi ya Islamic Foundation Arif Nahd alichangia kiasi cha sh 2 milioni, Mkurugenzi Islamic foundation Kanda ya kaskazini, Badru Nahdi alichanga million 2 huku Jukwaa la vijana likichanga million 11.


Baadhi ya watu walioshiriki mkutano huo papo hapo walichangia kiasi Cha sh 755,050 ambapo michango mingine ilikuwa ikiendelea kukusanywa kupitia Simu na account ya Jukwaa hilo.


Akizungumza kabla ya harambee hiyo, Kinana alipongeza Jukwaa la vijana wa Kiislamu mkoa Arusha kwa kuamua kuwaunganisha vijana na kufanya shughuli za kiuchumi kwa kufuata maadili ya Dini.


"Nawapongeza Vijana kwa kuanzisha jambo hili la kheri ikiwepo kusaidia makundi mbalimbali yenye uhitaji katika Jamii"amesema


Kinana pia aliwataka viongozi wa Jukwaa hilo katika mradi wao kujenga Chuo Cha Ufundi ili kusaidia vijana kujiajiri na kuajiriwa.


"Elimu ya ufundi kama kutengeneza magari ufundi umeme ujenzi, ushonaji, udereva na nyingine ukiwa nayo ni rahisi kupata ajira kuliko elimu ya nadharia"amesema .


Kinana alieleza kuridhishwa na mipango ya  Jukwaa la Vijana wa Kiislamu mkoa Arusha  kusaidia vijana katika masuala ya kiuchumi, ikiwepo kuanzisha vikundi vya kuweka na kukopa bila riba.


 Mwenyekiti wa jukwaa la Vijana mkoa Arusha, Kassim Degega amesema lengo la Jukwaa hilo ni kuwasaidia vijana kujikwamua na umasikini lakini pia kuwasaidia Jamii ikiwepo kulipa ada, kuchangia matibabu na vifaa vya shule.


Degega amesema wanakusudia kujenga kituo cha Waislam mkoa Arusha katika eneo la Nduruma ambapo kutakuwa na shule za ufundi, kituo cha Afya na sekondari.


Akizungumza katika mkutano huo, Mwenyekiti wa Taasisi ya Islamic Foundation, Arif Nahd licha ya kupongeza kazi nzuri ya Jukwaa la Kiislamu Arusha, alishauri Makao makuu ya jukwaa hilo nchini kufanyika Arusha.


"Mimi nawaheshimu sana Arusha katika harakati za dini hivyo nashauri hata Makao makuu ya jukwaa la vijana Taifa liwe Arusha"amesema 


Hata hivyo, Nahdi amesema ni muhimu  Waislamu kujitokeza kuchangia Maendeleo ya Waislam na Uislam .


Amesema shughuli za dini zinahitaji gharama kubwa na kutolea mfano kituo cha TV Imani kwa mwezi wanalipiwa Setelaiti pekee millioni Saba.


Hata hivyo, alikemea suala la Waislam kula riba kwani ni dhambi kubwa na  akawataka kuachana nayo badala yake  wajiunge na benki ambazo zinatoa huduma za Kiislamu.


Mkuu wa kitengo cha huduma za Kiislamu katika benki KCB, Amour Muro amesema, benki hiyo ina  huduma sa Sahl  ambayo inafuata sheria za Kiislamu na akawataka vijana wa Kiislamu na wasio waislam kujiunga.


Muro amesema, huduma za benki za Kiislamu ni nzuri na hata mtu ambaye si muislam anaweza kujiunga na Sasa Kuna wateja wa Dini nyingine katika huduma hiyo.


Akizungumza katika maadhimisho hayo Sheikh Juma Ikusi aliwataka Waislam kuwa na maadili mema na kufuata maamrisho ya mwenyezi Mungu.

No comments: