Kinana Mgeni Rasmi Jukwaa la vijana wa Kiislam Mkoa Arusha - MAIPAC MEDIA TANZANIA

Breaking

MAIPAC MEDIA TANZANIA

A Centre for Indigenous and Pastoralists Community Informations




Saturday 23 December 2023

Kinana Mgeni Rasmi Jukwaa la vijana wa Kiislam Mkoa Arusha


Abdulrahman Kinana Makamu Mwenyekiti wa CCM Tanzania Bara 

Mwenyekiti wa jukwaa la vijana waislam mkoa Arusha, Kassim Degega akizungumza na waandishi wa Habari mapema leo


Na: Andrea Ngobole, Arusha

maipacarusha20@gmail.com

 Makamu Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi(CCM)Tanzania Bara, Abdurahman Kinana, kesho Desemba 24, anatarajiwa kuwa Mwenyekiti wa mkutano mkuu wa 10 wa jukwaa la vijana wa Kiislam mkoa Arusha, mkutano ambao utafanyika kituo cha mikutano cha kimataifa cha Arusha (AICC).


Mkutano huo, unatarajiwa kuwakutanisha zaidi ya vijana 400 mkoa Arusha, ambao ni wanachama wa jukwaa hilo, ambalo linalenga kuwauganisha vijana wa kiislamu katika kujikwamua na umasikini, lakini pia kupata fursa mbali mbali za kujiendeleza kielimu.


Akizungumza na waandishi wa habari, Amir wa Jukwaa hilo, Kassim Degega alisema maandalizi yote muhimu ya Mkutano huo, yamekamilika ikiwepo uthibitisho wa ushiriki wa viongozi mbali mbali.


"Jukwaa la vijana mkoa wa Arusha, tuna miaka 10 tangu kuanzishwa na tumekuwa tukifanya harakati kadhaa, ikiwepo kusaidia makundi ya vijana wa kike na kiume kupitia kikundi cha kuweka na kukopa bila riba, lakini tumekuwa tukitoa misaada mbali mbali kusaidia malipo ya ada kwa wanafunzi wasio na uwezo kiuchumi" amesema


Amesema jukwaa hilo pia limekuwa likichangia futari katika mwezi wa radhamani katika magereza, shule na taasisi mbali mbali lakini pia likiratibu elimu ya dini katika shule za msingi na sekondari katika jiji la Arusha.


Degega amesema mkutano huo mkuu, utakwenda sambamba na harambee ya kuchangia ujenzi wa kituo cha Waislam mkoa Arusha, ambacho kitajengwa eneo la Nduruma wilayani Arumeru.


Awali, Kaimu Katibu Mkuu wa Jukwaa hilo, Salum Mhina amesema maandalizi yote muhimu yamekamilika na wanaomba wakazi wa mkoa Arusha, kujitokeza katika maadhimisho hayo ya miaka 10 ya jukwaa hilo la vijana na harambee.


Mhina alisema jitihada za ujenzi zilianza mwaka jana, ambapo mgeni rasmi alikuwa ni aliyekuwa Mdhibiti na Mkaguzi wa Hesabu za Serikali, Profesa Mussa Assad na mwakani wanatarajia kuanza ujenzi wa kituo hicho.


Alisema katika maadhimisho ya miaka 10 ya jukwaa hilo, pia viongozi wengine kadhaa wamealikwa akiwepo Sheikh mkoa Arusha wa baraza kuu la waislam Tanzania (BAKWATA), Sheikh Shaban Juma, Mkuu wa mkoa Arusha, John Mongella, wahadhiri mbali mbali wa dini ya Kislam na wawakilishi wa taasisi kadhaa za dini.




No comments: