Matokeo ya Zabuni kitalu cha uwindaji Makao WMA yapingwa - MAIPAC MEDIA TANZANIA

Breaking

MAIPAC MEDIA TANZANIA

A Centre for Indigenous and Pastoralists Community Informations




Tuesday 26 December 2023

Matokeo ya Zabuni kitalu cha uwindaji Makao WMA yapingwa

 



Katibu wa Makao WMA, Jeremia Nishon akizungumza na waandishi wa Habari


Mwiba Holding wakikabidhi kituo cha ulinzi kwa ajili askari wa TAWA kukabiliana na ujangili na wanyama wakali ambao wamekuwa kero wilaya ya Meatu mapema mwaka huu


Na: Joseph Mallya,Meatu


Maipacarusha20@gmail.com


Mgogoro mkubwa umeibuka kutokana na Zabuni ya Kitalu cha   Uwindaji wa Kitalii  katika kitalu cha Jumuiya ya Hifadhi ya Jamii ya  Wanyamapori Makao(MAkao WMA),wilayani Meatu .


Kampuni tatu zilizoshiriki katika Zabuni hiyo,zimepinga matokeo yaliyotangazwa na kamati ya Makao WMA na wameiomba wizara ya Maliasili na Utalii na halmashauri ya Meatu kutengua matokeo hayo.


Katika zabuni hiyo,kampuni nne, zilishiriki ambazo  ni Kampuni ya  Bushman Safaris Trakers Limited, Kampuni ya Kilombero North Safaris Limited, Kampuni ya EBN Hunting Safaris na kampuni ya Mwiba Holdind Limited.


Hata hivyo, katika mazingira yenye "utata",kampuni ua Kilombero North ilitangazwa kushinda zabuni hiyo.




Hivyo,Kampuni za  Bushman, Mwiba na EBN, zimepinga matokeo hayo na kueleza kanuni na taratibu za Zabuni zilikiukwa ikiwepo mshindi kuingiza maombi yake nje ya muda uliotangazwa na kupewa fursa ya kuboresha zabuni yake


Katika barua za malalamiko za kampuni hizo, ambazo Maipac blog umeziona,kampuni hizo zimetaka kutenguliwa matokeo yaliyotangazwa kutokana na kukiukwa taratibu za kisheria za zabuni.


Afisa wa  Kampuni ya Mwiba, Eribariki Lucas alisema wao wanacholalamikia ni taratibu za Zabuni, kukiukwa  kwa sababu zabuni zilitangazwa kisheria ikiwepo kufanya malipo ya Zabuni lakini kufunguliwa kabla ya mwisho  na kufanywa maboresho ni kinyume cha sheria.


“Sisi wote ambao hatukubaliani na matokeo tayari tumeandika barua za kupinga kilichofanyika na kutaka sheria ifuatwe”alisema




Katibu WMA akiri kuvunjwa sheria,atetea


Katibu wa Makao WMA, Jeremia Nishon anakiri kukiukwa taratibu za Zabuni ikiwepo kuzifungua kabla ya muda na kuzitaka kampuni kuboresha.




"Kama ni kosa labda hili la kufungua lakini tulifanya hivi kwa nia njema kuhakikisha tunapata mapato zaidi"alisema




 Alisema wamepata malalamiko ya Kampuni hizo, juu ya  zabuni iliyofunguliwa Desemba 5,2023 na sasa wanasubiri maelekezo ya ngazi za juu.


“Tumesikia malalamiko ya kampuni hizo na tayari tulipata rufaa rasmi ya Kampuni ya Bushman Safaris Ltd na kampuni za EBN na Mwiba wao walipeleka ngazi za juu ila tumepata taarifa”alisema


Alisema Kampuni ya Kilombero North Safaris Limited ndio imeshinda kitalu hicho, ambacho kilikuwa kimekodishwa kwa kampuni ya Mwiba kwa zaidi ya miaka 10.


“Tunasubiri maamuzi ya halmashauri na Wizara kwani sisi tulifata taratibu zote ikiwepo kufanya tathimini na mwekezaji aliyekuwepo Mwiba Holding Ltd ambaye alipata asilimia 65  lakini pia baadaye tulifanyia tathimini kampuni zote kwa kuzitembelea na kuona jinsi wanavyofanyakazi”alisema




Alisema katika zabuni hiyo,Kampuni Kilombero North ilishinda kwa kuahidi  kulipa pango sh 650 milioni kwa mwaka,   Mwiba iliahidi kutoa 635, kampuni ya EBN safari Ltd iliahidi kulipa sh 437 milioni na kampuni ya Bushman iliahidi kulipa sh 382.


“Kwa mujibu wa Kanuni, kampuni ambayo haikubaliani za matokeo ya zabuni ilipewa siku 14 kukata rufaa na tumepokea rufaa moja na tumeona malalamiko yaMwiba na EBN ambayo wao walipeleka kwa Mkurugenzi wa Wanyamapori hivyo tunasubiri maelekezo mengine”alisema


Mwenyekiti wa Makao WMA,Daniel Sagika alisema wao wanaamini mchakato ulikwenda vizuri na sasa wanasubiri maamuzi ngazi za juu baada ya kuomba wapewe taarifa.


Mkurugenzi wa Idara ya Wanyamapori ,Dk Fortunata Msoffe akizungumza na mwandishi wa habari hizi, alikiri kufanyika zabuni ya kitalu cha Makao WMA lakini hata hivyo, alikuwa hajapata malalamiko rasmi.


“Sina taarifa rasmi za malalamiko rasmi na tukipata yatafanyiwa kazi kwa mujibu wa sharia”alisema


Hata hivyo,kiongozi mmoja wa serikali mkoani Simiyu ambaye aliomba kuhifadhiwa jina  alisema Makao WMA ilifanya makosa kikanuni kufungua zabuni kabla ya muda na kuwataka waliopeleka maombi kurekebisha.




"Nadhani sheria za zabuni zipo wazi inawezekana walikuwa na nia njema lakino wamevunja sheria ya Zabuni kwani duniani kote hakuna zabuni ya aina hiyo"amesema




Hata hivyo,kiongozi huyo amesema suala hilo linashughulikiwa na ngazi mbalimbali ili kumaliza mgogoro huo.

Mwiba holding ikiwa imezindua mradi wa chukula cha bure kwa wanafunzi wa shule ya msingi makao mradi ambao umekuwa ma faida kubwa wilaya ya meatu kutokana na kupunguza utoro na kuongeza ufaulu.


Mkataba wa Kampuni ya Mwiba Holding Ltd unatatajiwa kuisha rasmi Desemba 31 mwaka huu,baada ya kumiliki kitalu hicho kwa zaidi ya miaka 10.



No comments: