WANAKIJIJI VILIMA VITATU WAFUNGA OFISI YA KIJIJI MPAKA WAPATIWE HATI ZA MAKAZI - MAIPAC MEDIA TANZANIA

Breaking

MAIPAC MEDIA TANZANIA

A Centre for Indigenous and Pastoralists Community Informations




Sunday, 3 December 2023

WANAKIJIJI VILIMA VITATU WAFUNGA OFISI YA KIJIJI MPAKA WAPATIWE HATI ZA MAKAZI


Lango Kuu la Ofisi ya kijiji Cha VILIMA VITATU likiwa limefungwa na wanakijiji wa mfulwangombe kwa kutumia miba ili kuwazuia watendaji wa Serikali mpaka wapate muafaka wa eneo lao




Na: Andrea Ngobole, Babati


maipacarusha20@gmail.com


Wananchi wa Mfulwang'ombe, Kijiji cha Vilima vitatu wilayani  Babati mkoani Manyara, wamefunga Ofisi ya Kijiji hicho wakishinikiza kupewa anuani za makazi ya eneo lao.


Wananchi hao wa Jamii ya Kibarbeig  wanapinga Utendaji wa viongozi wa Kijiji hicho kushindwa kutatua changamoto zao za makazi.


Akizungumza nje ya ofisi ya kijiji hicho waliyoifunga na kuzuia utendaji kazi Udangwenga Bayayi amesema wamefunga Ofisi hiyo kutokana na serikali ya Kijiji hicho kushindwa kutatua kero zao.


Amesema awali waliandamana hadi ofisi ya Kijiji hicho kuomba kupatiwa ufumbuzi wa mgogoro wao wa ardhi na ndipo Mkuu wa wilaya hiyo, Lazaro Twange alifika.


"Baada ya Mkuu wa wilaya kuja aliomba tumpe siku 14 angetupa majibu lakini zimeisha Leo hajatokea ndio sababu tumekuja kufunga ofisi"amesema


Amesema waliondolewa eneo la Malamboi na kupelekwa Mfulwang'ombe lakini hadi sasa hawajuwi hatma Yao kwani hawajapewa anwani ya makazi.

Baadhi ya akina Mama wakiwa na watoto wao nje ya ofisi hiyo wakisubiri hatma yao toka uongozi wa Wilaya ya Babati


Khadija Loti amesema viongozi wa Serikali ya Kijiji hicho, wameshindwa kuwasaidia kwani wamekuwa wakishirikiana na viongozi wa Burunge WMA kuwanyima haki.


"Sisi hatuondoki hapa ofisini Hadi tujuwe hatma yetu kuhusu mgogoro huu wa ardhi"amesema


Manuu Mandanga na Helena Robert wamesema wameshangaa kuona eneo lao la Mfulwang'ombe  kuanza kuweka alama za mipaka kuwa wapo ndani ya hifadhi lakini wao walihamishiwa hapo toka Malamboi.


"Tunataka Mkuu wa mkoa Manyara asikie kilio chetu na aje kutusikiliza"alisema Mandanga.


Afisa Mtendaji wa Kijiji hicho,Selemani Nkola alikiri kufungwa ofisi na kueleza suala hilo tayari linafanyiwa kazi na serikali.


Amesema Ofisi ya Mkuu wa wilaya hiyo  itatoa maelezo ya kumalizwa kwa mgogoro huo kama alivyoahidi Mkuu wa wilaya, Lazaro Twange hivi karibuni.


Mwenyekiti wa Serikali ya Kijiji hicho,Abubakar Msuya amesema changamoto ya mgogoro huo inafanyiwa kazi na yeye aliingia madarakani aliikuta na tatizo sio serikali ya Kijiji .


Aliyekuwa Mwenyekiti wa Kijiji hicho,Erasto Belela amesema ni kweli Kaya 17 zilihamishiwa eneo la Mfulwang'ombe na ilitakiwa eneo hilo kuondolewa katika eneo la hifadhi na tayari Kijiji kilipeleka maombi WMA kupunguza eneo la hifadhi kidogo ili wananchi wapewe hati za makazi.


"Sasa wale ambao walipinga huo Mpango ndio Leo wanachochea wananchi kuandamana na kufunga ofisi kwa maslahi yao ya kisiasa kwa sababu wapo nje ya Uongozi "amesema.





No comments: