OFISI YA MKUU WA MKOA WA ARUSHA WASHERHEKEA MWAKA MPYA NA WATOTO WAISHIO KWENYE MAKAO. - MAIPAC MEDIA TANZANIA

Breaking

MAIPAC MEDIA TANZANIA

A Centre for Indigenous and Pastoralists Community Informations




Tuesday 2 January 2024

OFISI YA MKUU WA MKOA WA ARUSHA WASHERHEKEA MWAKA MPYA NA WATOTO WAISHIO KWENYE MAKAO.

 





Na Elinipa Lupembe, Arusha


maipacarusha20@gmail.com


Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Arusha, chini ya uongozi wa Mhe. John V.K Mongella, wamesherehekea Sikukuu ya mwaka mpya na watoto wanaolelewa kwenye Makao ya watoto wanaotoka kwenye mazingira magumu kwa kushiriki pamoja chakula cha mchana.


Akizungumza wakati wa kuwakaribisha wageni kwenye hafla hiyo, Mhe. Mongella, amesema kuwa huo ni utaratibu wa kawaida wa ofisi yake, ukiwa na lengo la kukaa na kula pamoja na watoto hao kama familia kwa kuthamini uwepo wa watoto hao pamoja na kazi kubwa inayofanywa na walezi wa watoto hao kwa niaba ya Serikali.


Serikali inatambua na kuthamini kazi kubwa inayofanywa na walezi wa watoto katika Makao, kama watanzania na kwa niaba ya Serikali tunaungana nao kwa kidogo kinachopatikana ikiwemo kukaa pamoja na kushiriki chakula angalau mara chache panapo nafasi.


"Niwatie moyo watoto na vijana, mjisikie mko nyumbani na tushiriki pamoja chakula huku mkitambua changamoto mnazopitia ni sehemu ya maisha ambayo humkuta binadamu yoyote, mshukuruni Mungu kwa nafasi ya malezi mliyopata na kutambua thamani yenu kubwa kwa jamii" Ameweka wazi Mhe. Mongella


Hata hivyo wageni, viongozi pamoja na walezi wa watoto hao, wameishukuru Serikali kupitia Mkuu huyo wa mkoa,  kwa upendo mkubwa aliuonyesha kwa kuwathamini watoto hao wenye uhitaji na kusema kuwa huo ni moyo wa kipekee kwa kuwa kuwa kiongozi pekee haimaanishi unauwezo wa kutoa.


Katibu Mkuu wa Jumuia ya Maridhiano na Amani Tanzania, Askofu Dkt. Isarael Ole Gabriel Maasa, amesema kuwa, Mhe. Mongella ni kiongozi mwenye maadili anayemuheshimu Mungu, Sadaka aliyotoa ndio dini nzuri inayoelekezwa kwenye maandiko matakatifu.


"Mkuu wa mkoa, sadaka hii inakufanya uwe na dini safi, Maandiko yanasema, Dini iliyo safi, isiyo na taka mbele za Mungu Baba ni hii, Kwenda kuwatazama yatima na wajane katika dhiki yao, na kujilinda na dunia pasipo mawaa"Amenukuu Kitabu cha Yakobo 1:27


Naye Shekhe Mkuu wa mkoa wa Arusha, Shaban Juma, amekiri kuwa, wapo watu kwenye Serikali lakini hawafikirii kuwaleta wanyonge kama hawa nyumbani kwao, Mtume anatuambia wapo watu wameumbwa kwa ajili ya haja za watu hasa wanyonge, Mkuu wetu wa mkoa ndio aina ya watu hao.


Dominic mtoto anayelelewa kwenye Makao ya The Joy of God Orphanage Center, amemshukuru Mkuu wa mkoa, kwa kuwakaribisha, kukaa meza moja na kula pamoja, kwa niaba ya watoto wenzake ametoa shukurani za dhati na kumuombea dua jema,  Mwenyenzi Mungu ambariki na abariki pale anapofanyia kazi 


"Tunaishukuru Serikali haijawahi kutuacha, asante baba yetu kwa kutualika siku ya leo, tumekula, tumeshiba na tumefurahi sana, tunakuombea Mwenyenzi Mungu asikupungukie pale ulipotoa, lakini tunawaomba wengine wenye uwezo kuendelea kuwasaidia watoto wenye mahitaji ili wakue na wasome hatimaye waweze kufikia ndoto zao kama watoto wengine" Amesema Shazma Hassan wa Makao ya Dhi Nurney Ngaramtoni


Awali, hafla hiyo imejumuisha watoto 131 kutoka kwenye nyumba tano za Makao,  iliyofanyika nyumbani kwa mkuu huyo wa mkoa wa Arusha, eneo la Uzunguni, kata ya Sekei, Jiji la Arusha.

No comments: