TWFA MOROGORO YAPATA VIONGOZI WAPYA - MAIPAC MEDIA TANZANIA

Breaking

MAIPAC MEDIA TANZANIA

A Centre for Indigenous and Pastoralists Community Informations




Monday 8 January 2024

TWFA MOROGORO YAPATA VIONGOZI WAPYA

 




Na Lilian Kasenene,Morogoro.


maipacarusha20@gmail.com


Chama cha Soka la Wanawake (TWFA) Mkoa wa Morogoro kimefanya uchaguzi wake na kuwapata viongozi watakao ongoza kwa kipindi cha miaka minne ijayo, huku aliyekuwa Katibu wa chama hicho, Beatrice Selemani, akishinda nafasi ya Uenyekiti kwa kupata kura zote kutokana na kuwa mgonbea pekee katika nafasi hiyo.


Akitangaza matokeo ya uchaguzi huo uliofanyika Shule ya sekondari ya Bungo, mjini Morogoro, msimamizi wa uchaguzi huo Deo Achimpota alisema Beatrice alishinda nafasi hiyo kwa kupata kura zote 12 za ndio baada ya kupigiwa kura na wajumbe 12 wawakilishi wa wilaya sita za mkoa wa Morogoro huku wilaya moja ya Malinyi ikishindwa kupeleka wawakilishi.



Mwingine aliyeshinda ni mwandishi wa habari wa IPP Media, Idda Mushi, aliyepata kura 12 dhidi ya 0 katika nafasi ya uwakilishi wa Mkutano mkuu taifa baada ya kumshinda mpinzani wake Jack Meena aliyekuwa akitetea nafasi hiyo.


Achimpota alimtangaza mwingine aliyechaguliwa kuwa ni Flora ambaye hakuwepo kutokana na dharura aliyeshinda ujumbe wa mkoa huku nafasi mbili za Katibu na mjumbe mwingine wa mkoa zikikosa wagombea na maamuzi ya kuwapata wa kuziba nafasi hizo yakiachwa kwa viongozi wapya waliochaguliwa 


Akizungumza baada ya kuchaguliwa, Mwenyekiti wa TWFA Mkoa wa Morogoro Beatrice Selemani akasema soka la wanawake mkoani humo linakabiliwa na elimu ndogo ya utambuzi kwa jamii kuhusiana na umuhimu wake na kufanya mabinti wengi kukumbwa na vikwazo kujitokeza kushiriki mchezo huo.


Hata hivyo akataja hatua ambayo uongozi huo unaenda kutekeleza kuwa ni kuifikia jamii kwa kuwapa elimu kwa uwazi juu ya namna mchezo wa soka  ulivyogeuka kuwa fursa adiimu kwa Watoto wakike katika soko la ajira.


“Katika kipindi hiki cha miaka minne tuliyopewa kuongoza, moja ya eneo tukalofanyia kazi kazi ni kuinua soka la wanawake, ninatambua bado jamii inakabiliwa na uelewa mdogo wa utabuzi wa soka la wanawake, kwa kuwa bado wengi wao wanaotaka kushiriki wanakumbana na vikwazo katika jamii na familia,” alisema Beatrice


Aidha aliwapongeza viongozi na wadau wa soka la wanwake waliojitokeza katika uchaguzi huo ambao aliwania nafasi hiyo pasipo kuwa na mpinzani, na wapiga kura waioshiriki zoezi hilo kumpitisha kwa kura zote.

 

Kwa upande wake Idda alisema watahakikisha wanaenda kuweka nguvu ya pamoja na viongozi ngazi za Wilaya katika kuanzisha ligi za wanawake katika maeneo ya vijijini ili kuibua vipaji vipya na kuongeza hamasa ya Watoto wa kike kujitokeza zaidi kushiriki soka.


Mikakati mingine ni pamoja na kutafuta wafadhili watakaofadhili mashindano mbalimbali yatakayoanzishwa pamoja na vifaa vya michezo.


Alisema kwa miaka minne ya uongozi wao, wanatarajia kuanzia vijini kuibua vipaji vya Watoto wakike katika mchezo wa soka ili kuvipa nafasi ya kuonekana, huku wakitazamia kufanya kazi karibu na vilabu vya soka la wanawake vilivyopo kwasasa mkoani humo.


Naye Mwenyekiti Chama cha Soka  Mkoa wa Morogoro MRFA Paschal Kihanga mbali na kuwapongeza viongozi waliochaguliwa, aliwasihi kufanya kazi kwa ushirikiano, kuepuka misuaguano inayoweza kukwamisha mikakati ambayo wamepanga kwenda kuitekeleza.


“Binafsi nawapongezeni kwa kuchaguliwa kuongoza gurudmu hili, viongozi waliokuwepo walikuwa hawana malumbano, shirikianeni kwa umoja, ikitokea kuna jambo halipo sawa, kutaneni mpate ufumbuzi kwa pamoja, hakikisheni hamruhusu kelele zenye kuvuruga mikakati mtakayokwenda kutekeleza” alisema Kihanga


Nafasi zilizowaniwa katika uchaguiz huo ni nafasi ya Mwenyekiti chama cha mpira wa miguu kwa wanawake Mkoa, Mjumbe wa Mkutano Mkuu Taifa, Mjumbe wa Vilabu Mkoa huku nafasi ya Katibu pamoja na Mjumbe wa mkutano mkuu wa mkoa zikibaki wazi kwa kukosa wagombea, hivyo Uongozi uliochaguliwa chini ya Mwenyekiti mpya watapendekezs viongozi wa kujaza nafasi hizo kwa mujibu wa katiba.



No comments: