Uchaguzi Viongozi ACT-Wazalendo Arusha, Manyara Wapingwa, Msimamizi wa uchaguzi adaiwa kutinga na majina yake - MAIPAC MEDIA TANZANIA

Breaking

MAIPAC MEDIA TANZANIA

A Centre for Indigenous and Pastoralists Community Informations




Saturday 20 January 2024

Uchaguzi Viongozi ACT-Wazalendo Arusha, Manyara Wapingwa, Msimamizi wa uchaguzi adaiwa kutinga na majina yake

 

Baadhi ya wanachama wa Act-Wazalendo Mkoa wa Arusha na Manyara, ambao wamekata rufaa baada ya Uchaguzi kukiukwa taratibu.


Na: Andrea Ngobole, Arusha


maipacarusha20@gmail.com


Wagombea wanane walioshiriki uchaguzi wa chama Cha ACT-Wazalendo Mkoa Arusha na Manyara wamepinga matokeo ya uchaguzi huo na kukata rufaa Kwa Karibu Mkuu wa Chama hicho.


Uchaguzi wa ACT-Wazalendo Mkoa wa Arusha na Manyara ulifanyika Januari 14  mwaka huu, ukisimamiwa na  Naibu Waziri Kivuli Ofisi ya Rais- Mipango, Uwekezaji na Hifadhi ya Jamii, Shangwe Mike Ayo ambaye anatuhumiwa kuvuruga uchaguzi huo.


Msimamizi huyo ambaye ni mwenyeji wa jimbo la Arumeru Mashariki anadaiwa kwenda kwenye uchaguzi na Wagombea wake ambao aliwachukulia fomu na kuwalipia ambao ndio wameshinda.


Alizungumza na waandishi wa Habari jijini Arusha, aliyekuwa mgombea nafasi ya Mwenyekiti wa chama hicho mkoa Arusha, Chief Johnson Mahuma amesema wamekata rufaa kupinga matokeo baada ya kukiukwa taratibu za uchaguzi.


Chief Mahuma alisema wamepeleka rufaa yao Kamati ya uchaguzi wa Taifa na wanaamini haki itatendeka ili kupatikana viongozi ambao watachaguliwa kihalali .


Alisema miongoni mwa sababu za Kukata rufaa ni msimamizi wa Uchaguzi kuenguwa ukumbi Wagombea ambao tayari walipitishwa na Kamati ya uteuzi ya Taifa.


Msimamizi kufika ukumbi na orodha ya wanachama wapya ambao aliwachukulia fomu na baadae baadhi ndio walishinda uchaguzi.


Amesema pia Wagombea kutopata fursa ya kuomba kura wala kuwa na Mawakala wakati wa kuhesabu kura.


Mgombea mwingine Baraka Veresi aliyekuwa anagombea nafasi ya Katibu Mwenezi mkoa Arusha, amesema sababu nyingine ya kukata rufaa ni kukamata kura feki hasa katika nafasi yake.


Amesema pia zoezi la uchaguzi liligubikwa na ukabila hasa kutokana na msimamizi kupeleka ndugu zake kugombea pamoja na rafiki zake wa Jimbo la Arumeru Mashariki ambao walishinda.



Amesema wengine ambao wameungana katika rufaa hiyo ni pamoja na Wagombea wa chama hicho, Pius Kasekwa, Gasper Laizer,Clif Shayo, Rahma Rashid na Amina Zuberi.


Kwa Upande wa mkoa Manyara pia aliyekuwa mgombea wa nafasi ya Katibu Mkuu, Said Issa Hango pia amekata rufaa kupinga kushindwa.


Katika rufaa hiyo, Hango pia anamlalamikia msimamizi wa Uchaguzi kukiuka taratibu ikiwepo kuwa na Wagombea wake na kuvuruga zoezi la uchaguzi kutokana na kushirikisha wapiga kura ambao sio halali.


Katika uchaguzi wa mkoa Arusha Elia Remmy alishinda Unyekiti kwa kupata kura 46,Chief Mahuma kura 25 na Kasekwa kura 3.


Katika uchaguzi wa mkoa Manyara, aliyeshinda Unyekiti wa mkoa ni Said Njuki alipata kura 56 akifuatiwa na aliyekuwa Mwenyekiti wa zamani wa Mkoa huo Daniel  Kyusilu alipata kura 18 huku Olais Silas  alipata kura moja.


 Mwanahamisi  Hamisi alichaguliwa kuwa Katibu wa chama Mkoa huo nafasi ambayo ushindi wake  unapingwa na Hango.


Katibu Mkuu wa ACT-WAZALENDO Taifa, Shaibu Addo amesema Hana cha kujibu Kwa Sasa kwani bado hajapata  rufaa hizo.

No comments: