WATUMISHI OSG WAONYWA KUVUJISHA NYARAKA ZA SERIKALI WATAKIWA KUWA NA UADILIFU NA USIRI - MAIPAC MEDIA TANZANIA

Breaking

MAIPAC MEDIA TANZANIA

A Centre for Indigenous and Pastoralists Community Informations




Friday 12 January 2024

WATUMISHI OSG WAONYWA KUVUJISHA NYARAKA ZA SERIKALI WATAKIWA KUWA NA UADILIFU NA USIRI

 




Na Lilian Kasenene,Morogoro


Maipacarusha20@gmail.com


Kaimu Naibu Wakili Mkuu wa Serikali, Ofisi ya Wakili Mkuu wa Serikali Mark Mulwambo amesema pamoja na ofisi hiyo kutambua umuhimu wa watumishi wake, amewataka waendelee kuzingatia uadilifu na usiri katika kutenda kazi zao.


Alisema hayo mjini Morogoro wakati wa mafunzo elekezi juu ya mfumo wa usajili wa mashauri ya mahakama kuu ya Tanzania (e-CMS) na utunzaji wa nyaraka za serikali kwa watumishi wa kada ofisi hiyo ya wakili mkuu wa serikali.


Mulwambwo alisema kumekuwa na tabia ya baadhi ya watumishi wa serikali kwenye kada mbalimbali nchini kuvujisha nyaraka za serikali na kuonekana zikichambuliwa kwenye mitandao ya kijamii kinyume cha sheria na taratibu


Aidha alisema chanzo cha kuvuja kwa nyaraka za serikali mara nyingi huwa ni ama watumishi walipewa dhamana ya kuzitunza kutokuwa makini ama kuzivujisha kwa makusudi kwa maslahi yao binafsi.


“Niwasihii kuwa makini na kutumia ujuzi wenu katika mafunzo hayo kuondoa hali hiyo ya kuvuja nyaraka za serikali, sitarajii kuona mtumishi tena aliyepata mafunzo anakuja kuwa katika tuhuma za uvujishajii wa nyaraka hizo, na hiyo ni njia ya kuepuka madhara ya kufanya hivyo,”alisema.


Mulwambwo alisema serikali haitakuwa na muamana na mtumishi atakayebainika kuhusika na uvujishaji wa taarifa zake za aina yoyote.


Pia alisema katika kipindi cha mwaka 2023 ofisi ya wakili mkuu wa serikali kupitia kitengo cha masjala ya sheria imeweza kufanya mambo mbalimbali ikiwemo upokeaji wa nyaraka za malalamiko na mawasiliano ya sheria, kupokea na kusajili mashauri yote yanayofunguliwa dhidi ya serikali na kutunza taarifa kwenye mfumo wan CIMS, kufuatilia na kuratibu Causelist za mahakama na mabaraza ya maamuzi na usuluhishi, kuandaa ushaidi wa migogoro ya usuluhishi.


Kaimu naibu huyo alisema mafunzo hayo ni ya kujitathimini utendaji wa kazi na kupata fursa ya kukumbushwa miiko na taratibu za kiutendaji hasa katika usiri na utunzaji wa nyaraka za serikali kwa njia ya Kielektroniki.


Kaimu mkuu wa kitengo cha masjala ya sheria, ofisi ya wakili mkuu wa serikali Dennice Leonard alisema mfumo wa mahakama wa e-CMS na mfumo wa OWMS wa CIMS utaongeza matumizi ya TEHAMA, kasi ya uelewa, uwazi, uwajibikaji na ufanisi ambayo itaongeza imani kwa wananchi kuhusu utendaji kazi wa vyombo vinavyotoa haki kwa wananchi.


Pia alisema katika mfumo huo wa mashauri wa mahakama umetambua wadau mbalimbali wakiwamo wakili wa kuwasilisha namba ya uwakili ambaoipo kwenye mfumo wa e-Wakili, Mawakili wa serikali ambao taarifa zao zinapatikana Nida , waendesha mashtaka, wananchi na taasisi/wawakilishi wa taasisi ambao wanasajili mashauri ya taasisi husika.


“Msingi wa mafunzo ni kujengeana uwezo kati ya watumishi wa ofisi ya wakili mkuu wa serikali na wale wa mahakama ili sasa tuweze kwenda pamoja,sasa tumeshaenda digitali hivyo utunzaji wa nyaraka za serikali na usiri kwa njia ya eleketroniki ambapo kuna sheria zake,”alisema.


Katibu sheria katika Ofisi ya Wakili Mkuu wa Serikali Victoria Kawacha alisema kama mshiriki mfumo huo utasaidia kuondokana na utendaji kazi wa kizamani na kwenda kwa kielektroniki zaidi ambapo wateja wao wanaendelea kuwa na imani na vyombo vya sheria


“Mwanzoni tulikuwa tukifanya kazi kwa ugumu katika kusajili mashauri ya serikali lakini kutokana na mfumo huu kwa sasa umerahisisha kwemye utendaji wetu wa kazi,”alisema.


Mafunzo hayo jumuishi yamewajumuisha washiriki 27 kutoka Ofisi ya Wakili Mkuu wa Serikali(OSG),ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali(OAG) na yanalenga kuwawezesha watumishi kubadilishana uzoefu kwenye masuala ya usajili wa mashauri na utunzaji wa kumbukumbu za kielektroniki na ubora wa kuhudumia wateja wan je na ndani.


Ofisi ya Wakili Mkuu wa Serikali ipo kwenye mikoa 17 pale ambapo serikali imefungua mahakama kuu.



No comments: