WAZIRI NDALICHAKO-UTANDAWAZI UMECHOCHEA KASI YA MABADILIKO SOKO LA AJIRA - MAIPAC MEDIA TANZANIA

Breaking

MAIPAC MEDIA TANZANIA

A Centre for Indigenous and Pastoralists Community Informations




Friday 19 January 2024

WAZIRI NDALICHAKO-UTANDAWAZI UMECHOCHEA KASI YA MABADILIKO SOKO LA AJIRA

 




Na Lilian Kasenene,Morogoro


maipacarusha20@gmail.com


Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Kazi, Vijana na Wenye Ulemavu Profesa Joyce Ndalichako amesema kuongezeka kwa utandawazi kumechochea kasi ya mabadiliko ya soko la ajira, hivyo Serikali inahitaji kupata takwimu za kina za soko hilo zitakazoakisi hali halisi kwa ajili ya kufanya maamuzi yenye tija zaidi.


Amesema hayo mjini Morogoro wakati akifunga mafunzo kwa Wadadisi na Wasimamizi wa Utafiti wa Watu Wenye Uwezo wa kufanya Kazi wa Mwaka 2024 ambapo jumla ya washiriki 139 wamepatiwa mafunzo hayo kutoka mikoa yote ya Tanzania Bara na Zanzibar.


Profesa Ndalichako amesema utandawazi huo pia umechochea kasi ya kukua kwa Teknolojia  na kwamba taarifa zanye takwimu zitaisaidia Serikali kufahamu hali halisi ya soko la Ajira nchini ilivyo kwa kubainisha maeneo yanaayofanya vizuri na maeneo yenye changamoto kwa ajili ya kuweka mikakati zaidi ya kukuza uchumi na ajira zenye staha Nchini.


“Haya Mafunzo yanalenga kutoa mbinu za kuhoji na namna ya kujaza madodoso katika ngazi ya kaya kwa kutumia vishikwambi na yatawezesha ninyi Wadadisi kutumia namna bora ya kudodosa ili kukusanya taarifa sahihi kwa lengo la kudhibiti ubora wa takwimu zitakazokusanywa na kutuma taarifa hizo kwenye server zilizoko makao makuu ya Ofisi ya Taifa ya Takwimu,”amesema.


Aidha amesema Serikali iliidhinisha Mpango kabambe wa kuboresha na kuimarisha takwimu, ambapo awamu ya Pili utatekelezwa kati ya Mwaka 2022/23 hadi 2026/27, katika Mpango huo, Utafiti wa Watu wenye Uwezo wa Kufanya Kazi utakuwa unafanyika kila mwaka badala ya miaka mitano ili kuongeza hali ya upatikanaji wa takwimu za soko la ajira Nchini na kuisadia Serikali kuweka mikakati ya kufikia malengo iliyojiwekea ifikapo Mwaka 2025.


Waziri huyo wa Kazi, amewataka washiriki hao kutambua kuwa, Serikali imewapa dhamana kubwa ya kuhakikisha kuwa zoezi zima la Utafiti na udadisi huo linafanikiwa kwa ufanisi na kwa viwango vya ubora vinakusudiwa.


Alitoa wito kwa viongozi wote wa Serikali katika ngazi zote za utawala kutoa ushirikiano wa kutosha kwa wadadisi na wasimamizi wa Utafiti huo katika maeneo yote yatakayohusika, huku akiwaomba wananchi maeneo yaliyochaguliwa kwa ajili ya utafiti kutoa ushirikiano wa kutosha kwa kujibu maswali watakayoulizwa na kutoa taarifa sahihi wakati wa zoezi la kukusanya taarifa katika ngazi ya kaya.


“Napenda kuwahakikishia kuwa, taarifa watakazotoa ni siri na zitatumika kwa shughuli za kitakwimu pekee kwa mujibu wa Sheria ya Takwimu Sura 351, na nawahakikishia wananchi kuwa, shughuli zao za kiuchumi na kijamii hazitasimamishwa wakati wa zoezi la Utafiti huu kwa kuwa wadadisi watakusanya takwimu za Utafiti wakati shughuli zingine zikiendelea kama kawaida,”amsema.


Kwa upande wake Mtakwimu mkuu wa Serikali Dk Albina Chuwa amesema Utafiti huo wa Mwaka 2024 utakuwa ni wa Saba kufanyika Nchini kwani tafiti nyingine zilifanyika katika miaka ya 1965, 1990/91, 2000/01, 2006, 2014 na 2020/21, na kwamba Lengo kuu la Utafiti huo ni kukusanya taarifa zitakazowezesha uandaaji wa takwimu zitakazoonesha kupima mwenendo halisi wa soko la Ajira Nchini.


Dk Chuwa amesema matokeo ya Utafiti yatatumika pia kupima na kufuatilia mabadiliko yaliyotokea katika soko la ajira ili kuiwezesha Serikali kuboresha sera na programu za kukuza ajira, kupanga na kufuatilia utekelezaji wa mipango mbalimbali ya maendeleo ya Nchi.


Amesema Utafiti huo umehusisha wadadisi 139 na wasimamizi 26 ambao ni Mameneja wa Takwimu wa Mikoa, utafanyika katika mikoa yote ya Tanzania Bara na Zanzibar ambapo kwa upande wa Tanzania Bara,Utafiti utafanyika kwenye mikoa yote 26 Maeneo ya Kuhesabia ni 441 ambayo yamechaguliwa kitaalamu kuwakilisha maeneo mengine Nchini.


Mtakwimu huyo mkuu amesema Utafiti huo utafanyika kwa muda wa miezi 12 ili kuwezesha kupima kikamilifu mienendo ya ajira na ukosefu wa ajira kwa vipindi au misimu yote ya mwaka na inatarajiwa kufanya jumla ya kaya 10,584 zitahojiwa Nchini kote.  


Amsema Serikali na wadau wa maendeleo hasa Benki ya Dunia kupitia mradi wa“Eastern Africa Regional Statistics Program for Results” pamoja na Shirika la Kazi Duniani (ILO) kwa kutoa msaada wa kifedha na kiufundi kwa ajili ya kufanikisha Utafiti huu.


Kamisaa wa Sensa ya Watu na Makazi Anne Makinda akizungumza katika mafunzo hayo amewataka vijana walipatiwa mafunzo hayo kufanyakazi hiyo kwa uadilifu na kuacha kufanya janja janja pindi wanapokuwa kwenye utafiti.


Lengo kuu la Utafiti ni kupata viashiria vya soko la Ajira nchini, ikiwemo kiwango cha ukosefu cha Ajira ( Unemployment rate), Kiwango cha Ajira isiyotimilifu (Underemployment rate), Kiwango cha Nguvu Kazi( Labor Force Participation rate) kiwango cha Ajira mbayá kwa watoto (Child labor) na kiwango cha Ajira kwa aina ya Kazi (0ccupation rate)   





No comments: