WANAFUNZI 1,000 NA WALIMU WAO WATUMIA VYOO VYA SHULE JIRANI, MBUNGE ABOOD ASIKITISHWA - MAIPAC MEDIA TANZANIA

Breaking

MAIPAC MEDIA TANZANIA

A Centre for Indigenous and Pastoralists Community Informations




Friday 23 February 2024

WANAFUNZI 1,000 NA WALIMU WAO WATUMIA VYOO VYA SHULE JIRANI, MBUNGE ABOOD ASIKITISHWA

 





Na Lilian Kasenene, Morogoro 


maipacarusha20@gmail.com


Wanafunzi zaidi ya 1,000 pamoja na walimu wao katika shule ya msingi Mgulu wa Ndege Manispaa ya Morogoro wanalazimika kutumia vyoo vya shule jirani ya sekondari Mkundi kutokana na wao kukosa vyoo vya kujisitiri.


Hali ya kukosekana kwa vyoo hivyo imebainika baada ya mbunge wa jimbo la Morogoro mjini Abdullaziz Abood kutembelea kata ya Mkundi kwa nia ya kusikiliza kero za wananchi.


Akiwa katika ziara yake Abood alijionea kuwepo kwa changamoto hiyo ya vyoo ambapo ameahidi kujenga choo Cha walimu wa shule hiyo ya msingi Mgulu.


Aidha Mbunge huyo pamoja na kuchangia ujenzi huo wa choo amesema atachangia kiasi cha shilingi milioni Moja(1 Milioni)kwa ajili ya malipo ya fundi wa vyumba vya madarasa vilivyotokana na nguvu za wananchi.


Akizungumzia suala la vyoo vya wanafunzi alimtaka Mkurugenzi wa Manispaa Ally Machela kusimamia ujenzi huo, pamoja na kwamba Serikali kusema itajenga vyoo hivyo vya wanafunzi kwa haraka na mapema iwezekanavyo.


Mbunge huyo kwa upande wa shule ya sekondari mkundi baada ya kutembelea na kujionea namna watoto wanavyojisomea na miundombinu kutokuwa ya kuridhisha ameahidi kutoa kompyuta saba kwa ajili ya wanafunzi na kompyuta mpakato mbili kwa ajili ya matumizi ya walimu.


Mbunge huyo mbali na masuala ya elimu, alitoa kiasi cha shilingi milioni 2.1 kwa ajili ya ujenzi wa ofisi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) kata ya Mkundi ambayo ujenzi wake umefikia kiwango cha madirisha.


"Kuna ujenzi wa kituo Cha Polisi viongozi kwenye hii kata hakikisheni mnafanya tathimini ya bajeti ya uwekaji kenchi kwenye hiki kituo wakati naendelea kushughulikia,". amesema.


Katika kusikiliza kero za wananchi Abood alipata malalamiko kwenye suala la kukosekana kwa Maji, ubovu wa miundombinu ya barabara pamoja na suala la Umeme, ambapo aliwataka wananchi kuwa wavumilivu wakati akifatilia, huku wataalamu wa maji walikuwepo waliahidi kuwa suala la maji litakuwa limeisha ndani ya wiki nne na maji kuanza kupatikana.


Pia Abood ameshukuru Serikali kupitia Rais Samia Suluhu Hassan kwa namna fedha nyingi za miradi ya maendeleo zilivyotolewa kwenye Jimbo la Morogoro mjini ambapo aliwataka wahusika kutunza miradi hiyo.


Diwani wa kata ya Mkundi Zahoro Chomoka alishukuru Mbunge kwa namna anavyojitoa kwa wananchi kwenye masuala mbalimbali ya maendeleo na kwamba amekuwa mwakilishi na mtetezi kwao.



No comments: