Waziri wa Maliasili atangaza mkakati kuokoa Mapito 20 ya wanyamapori, Mabwawa kuchimbwa maeneo ya hifadhi, askari kuongezwa, elimu kutolewa - MAIPAC MEDIA TANZANIA

Breaking

MAIPAC MEDIA TANZANIA

A Centre for Indigenous and Pastoralists Community Informations




Sunday 25 February 2024

Waziri wa Maliasili atangaza mkakati kuokoa Mapito 20 ya wanyamapori, Mabwawa kuchimbwa maeneo ya hifadhi, askari kuongezwa, elimu kutolewa

 

     

Waziri wa Maliasili na Utalii, Angellah Kiuruki 




Na: Mussa Juma, Same 


maipacarusha20@gmail.com


Waziri wa Maliasili na Utalii, Angellah Kiuruki ametangaza mkakati wa kulinda maeneo 20 ya Mapito ya Wanyamapori (Shoroba ) kati ya maeneo 61 ambayo yalikuwa yametengwa.


Mkakati huo  pia unalenga kupunguza migogoro baina ya wanyamapori na Binaadamu nchini.


Miongoni mwa maeneo hayo ni Shoroba  ya Kwakuchinja iliyopo katikati mwa hifadhi za Taifa za Tarangire na Manyara na sasa imevamiwa.


Akizungumza katika Tamasha la Utalii wilayani Same mkoani Kilimanjaro, Waziri Kairuki alisema uvamizi maeneo ya Shoroba licha ya kuathiri wanyamapori lakini pia unasababisha migogoro baina ya Binaadamu na wanyamapori.


Alisema Wizara yake inakusudia kubainisha maeneo yote ya Shoroba kwa kupimwa na kulindwa.



Alisema Wizara katika kupunguza migogoro ya wanyamapori wanaotoka hifadhini inaendelea na Utafiti kubaini sababu za wanyamapori kutoka hifadhini na kwenda  kuvamia maeneo ya mashamba na hata kusababisha vifo.


Hata hivyo alisema Maeneo mengi ambayo yana migogoro baina ya wanyamapori na binaadamu ni yale ambayo kuna mapito ya Wanyamapori na  yamevamiwa kwa shughuli za Binaadamu ikiwepo kilimo na makazi.


Hata hivyo Wakati Serikali ikiendelea kuelimisha juu ya kuzuia uvamizi maeneo ya Shoroba inajiandaa pia kutangaza  viwango vipya vya vifuta jasho kwa wananchi walioathirika na maafa ya Wanyamapori nchini.


 Waziri  Kairuki alisema tayari Wizara yake, imeshawasilisha Wizara ya Fedha  kiwango walichopendekeza cha fidia kama Serikali itaweza kuhimili na kuweza  kulipika na kwamba muda sio mrefu vitatangazwa viwango vipya.



Alisema Sheria ya 2011 ambayo inaelezea Fidia na vifuta jacho kwa ambao wamepata adha za wanyamapori  itaboreshwa.



Akizungumzia alisema serikali pia, inaendelea kujenga vituo zaidi vya askari,kuchimba Mabwawa maeneo yaliyohifadhiwa  na kuongeza askari.


Waziri Kairuki akizungumzia adha za wananchi kuvamiwa na Tembo wilayani Same alisema, serikali inaendelea kuchukuwa hatua ikiwa ni pamoja na kuendelea kutoa elimu kwa wananchi na kuhakikisha changamoto hiyo inatatuliwa kwa njia mbalimbali.



"Niwaombe na niwape pole  ndugu zangu wa Same serikali inaendelea kuchukuwa hatua tumeshaanza kujenga baadhi ya mabwawa hifadhi ya Mkomazi na tutaendelea kufanya hivyo katika maeneo mengine ili wasilazimike kutoka nje ya hifadhi  kufuata maji kwasababu wakitoka nje kufuata maji watakutana na wananchi wetu na mazao ya wakulima."alisema


Alisema pia vimejengwa vituo vya askari wa Wanyamapori Gonja na Same Magharibi lengo ni kutoa msaada wa haraka Kudhibiti wanyamapori.


"Kama serikali hatufurahii kuona tembo hao wanakuja kumjeruhi mtu yeyote au kupoteza maisha ya wananchi wetu, tunachokifanya hivi sasa chini ya maelekezo ya Rais Samia Suluhu Hassan tunaangalia kiiini au chanzo kinachofanya tembo watokea hifadhini na kuingia kwenye makazi ya watu ni nini," alisema 



Alisema serikali hata hivyo imeendelea kulipa Fidia kwa wanaopata Shida za wanyamapori ambapo kwa  miaka  mitano imetoa zaidi ya Sh5.9 bilioni kama kifuta jasho na kifuta machozi .



" Serikali haiwezi hata kidogo kufidia uhai wa mtu kwani hakuna thamani kwa mwanadamu hivyo tunachokifanya sasa ni kulipa kifuta jasho "alisema


Alisema kwa wale ambao mazao yao yameathirika na tayari serikali imetoa Sh1.2 bilioni.



Waziri Kairuki alisema, zaidi ya Sh462 milioni kwa sasa zipo katika uhakiki na kadri fedha hizo zitakapopatikana zitalipwa  mapema iwezekanavyo kwa wananchi hao.


Awali Kamishna wa Uhifadhi wa Shirika la hifadhi za Taifa nchini, Juma Ikuji  alisema TANAPA itaendelea kuboresha mazingira ya hifadhi ili kuvutia watalii na kupunguza migogoro baina ya wanyamapori na Binaadamu.


Ikuji alisema ldadi ya askari wa Jeshi Usu imekuwa ikiongezwa lakini pia doria za mara kwa mara zinafanywa .


Kamishna Ikuji pia alisema miundombinu katika hifadhi zote itaendelea kuboresha ikiwepo barabara, maeneo ya kulala watalii na huduma nyingine muhimu kama mawasiliano.


Mkuu wa wilaya ya Same Kasilda Mgeni akizungumzia Tamasha Hilo la Utalii la Same alisema litakuwa likifanyika kila mwaka kwa lengo la kuvutia watalii.


Alisema wilaya ya Same imebarikiwa kuwa na vivutio vingi vya Utalii lakini bado havijatangwa ikiwepo maeneo 13 ya Mali kale, Msitu wa Shengena, ndege ambao hawapatikani eneo lolote duniani, Msitu wa Chome na tamaduni nyingi za asili.



No comments: