Na Mwandishi wetu, Simanjiro
maipacarusha20@gmail.com
DIWANI wa Kata ya Loiborsoit, Wilayani Simanjiro Mkoani Manyara, Siria Baraka Kiduya, amesoma taarifa ya utekelezaji wa ilani ya uchaguzi wa CCM kwa kipindi cha Novemba mwaka 2020 hadi Novemba mwaka 2023.
Diwani Siria akisoma taarifa hiyo kwa wajumbe wa Halmashauri kuu ya CCM kata ya Loiborsoit, amewashukuru wana CCM na wataalam na wananchi wote ndani ya kata kwa namna wanavyompa ushirikiano katika kutatua kero na changamoto mbalimbali.
“Ndugu Mwenyekiti wa CCM, naomba nichukue fursa hii kukishukuru chama changu (CCM) kwa kuniamini kupitia vikao mbalimbali na kupitisha jina langu kugombea nafasi ya udiwani wa kata ya Loiborsoit,” amesema Siria.
“Pia ndugu Mwenyekiti wa CCM wa Kata ya Loiborsoit na wajumbe kwa ujumla naomba niwashukuru ninyi kwa moyo wa unyenyekevu mkubwa kwa namna mlivyojitoa kwa namna moja au nyingine ili kupambana na kuhakikisha CCM inaendelea kushika dola na kuongoza Taifa hili kwa kipindi cha miaka mitano hadi 2025,” amesema.
Amewashukuru wataalam wote ndani ya Kata kwa namna wanavyopambania kutatua kero na changamoto mbalimbali ambazo zipo ndani ya kata hivyo itoshe kusema anawashukuru mno na kazi iendelee.
“Ndugu Mwenyekiti wa CCM Kata ya Loiborsoit, naomba nichukue fursa hii kumpongeza Mama yetu Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dokta Samia Suluhu Hassan kwa kuchaguliwa kuwa Mwenyekiti wa CCM kwa kura zote asilimia 100 na kwa namna anavyolipambania Taifa, tunamuombea Mungu ili aweze kutimiza majukumu yake vizuri na salama,” amesema.
Amesema Kata ya Loiborsoit ni miongoni mwa kata 18 zinazounda Wilaya ya Simanjiro ina wakazi wapatao 11,204 yenye vijiji viwili vya Loiborsoit B chenye vitongoji vitatu vya Engurash, Mazinde na Oltibu na kijiji cha Ngage, ambacho kina vitongoji vitatu vya Ngage A, Ngage B na Ndepesi.
Ametaja utekelezaji uliofanyika kwa kipindi cha Novemba 2020 hadi Novemba 2023 ni kumalizia chumba kimoja cha maabara cha shule ya sekondari Loiborsoit kilichogharimu shilingi milioni 30.
“Tumefanikiwa kujenga chumba kimoja cha darasa na ofisi moja ya walimu, iliyogharimu shilingi milioni 29 ambapo shilingi milioni 20 ilitoka kwenye pochi ya mama na shilingi milioni 9 ni michango ya wananchi wa vijiji vyote viwili vya Loiborsoit B na Ngage,” amesema Diwani Siria.
Amesema wamefanikiwa kujenga chumba kimoja cha darasa kwenye shule hiyo ya sekondari lililogharimu shilingi 27 ambapo UVIKO 19 ilitoa shilingi milioni 20 na michango ya wananchi wa vijiji vyote viwili ni shilingi milioni 7.
Amesema kwenye shule ya msingi Mazinde walipata madarasa nane ya wavulana na matundu nane ya vyoo ya wasichana, yaliyofadhiliwa na shirika la ECLAT FOUNDATION na nguvu ya wananchi.
“Kwenye shule ya msingi Ndepesi tumefanikiwa kujenga ofisi ya walimu iliyogharimu shilingi milioni 9 fedha ambazo zilitolewa na halmashauri ya wilaya ya Simanjiro,” amesema Diwani Siria.
Amesema pia wamefanikiwa kujenga nyumba ya walimu iliyogharimu kiasi cha shilingi milioni 10 fedha zilizotolewa na Halmashauri ya Wilaya ya Simanjiro.
Amesema walipokea madawati 75 kutoka Halmashauri ya Wilaya ya Simanjiro, ambayo yapo kwenye shule hiyo ya msingi Ndepesi, yanayotumiwa na wanafunzi.
Amesema kwenye shule ya msingi Loiborsoit B wamefanikiwa kujenga choo chenye matundu saba ya wasichana kilichogharimu shilingi milioni 3.4 ambapo TAWA walichangia shilingi milioni 2.850 na wananchi walichangia shilingi 600,000.
“Kwenye shule ya msingi Ngage tumefanikiwa kujenga choo cha matundu saba ya wasichana iliyogharimu shilingi milioni 15 zilizotolewa na Halmashauri ya Wilaya ya Simanjiro,” amesema Diwani Kiduya.
Amesema kwenye shule hiyo ya Ngage, wamefanikiwa kujenga vyoo viwili vya walimu, ambapo walimu wa kiume choo kimoja na walimu wa kike choo kimoja vilivyogharimu shilingi milioni 5 zilizotolewa na Halmashauri ya Wilaya ya Simanjiro.
Diwani huyo amesema pia wamefanikiwa kumalizia chumba cha kompyuta kwenye shule ya msinig Ngage, chenye thamani ya shilingi milioni 5.
Amesema matarajio ya mwaka 2024/2025 kwenye suala la elimu ni umaliziaji wa shule shikizi zote mbili za Songoyo na Ngage B.
“Ndugu Mwenyekiti wa CCM kata ya Loiborsoit, kwenye suala la afya, kata yetu ina zahanati mbili zilizopo kila kijiji ambapo kijiji cha Ngage kina zahanati yake na kijiji cha Loiborsoit B, pia kina zahanati yake,” amesema Diwani Siria.
Amesema kwenye zahanati ya Ngage wamefanikiwa kufanya ukarabati kwenye chumba cha kujifungua wakiwa mama na kujenga choo chenye matundu manne na mabafu mawili, kujenga choo cha watumishi na hivyo vyote vimejengwa kupitia mradi wa WARSH kwa gharama za shilingi milioni 34.
Amesema kwenye zahanati ya Loiborsoit wamefanikiwa kufanya ukarabati wa chumba cha kujifungulia wakina mama na kujenga choo chenye matundu manne na mabafu mawili na vyoo vya watumishi vilivyogharimu shilingi milioni 35 kupitia mradi wa WARSH.
“Hata hivyo, tupo kwenye mchakato wa uanzishwaji wa kituo cha afya Loiborsoit kwani kwenye kata yetu hatuna kituo cha afya zaidi ya zahanati hizo,” amesema Diwani Siria.
Amesema kuhusu usalama wana mpango wa ujenzi wa kituo cha polisi Loiborsoit na miundombinu ya barabara kuna mpango wa upatikanaji wa daraja la kuunganisha wilaya za Simanjiro na Same mkoani Kilimanjaro kupitia kijiji cha Ngage.
“Katika miundombinu ya nishati ya umeme usambazaji unatarajiwa kufanyika katika vitongoji vyote vilivyobaki vya Mazinde, Ngage A,Ndepesi na Endurashi,” amesema Diwani Siria.
Amesema usambazaji wa maji katika vitongoji vyote vilivyobaki vya kijiji cha Loiborsoit B vya Mazinde na kijiji cha Ngage vitongoji vya Ngage A na Ndepesi na usambazaji wa majumbani na maeneo yote yaliyobakia.
Amesema katika kilimo kuna uendelezaji wa uchimbaji wa mfereji wa Songoyo hadi mashamba mapya ya Ngage B Lesurenge mpaka nguzo za umeme.
Amesema kwenye utatuzi wa migogoro wa kijiji cha Loiborsoit B na Edonyongijape uliodumu kwa muda mrefu sasa tangu mwaka 1991 umetatuliwa mwaka 2024 kwa kushirikiana na wataalam wa ofisi ya mkuu wa wilaya kwa kurejesha takribani hekari 816 ambazo zilishikiliwa na kijiji jirani na kurejeshwa Loiborsoit B na mgogoro kutatuliwa kwa amani na kumalizika rasmi.
“Mgogoro wa mashamba kijiji cha Ngage umetatuliwa baada ya watu kulalamika CCM juu ya ugawaji haukuwa halali kwa hiyo chama kikatoa maelekezo kwa Serikali ili kuumaliza na kisha kumalizika rasmi ambapo mashamba ya kitongoji cha Ngage B eneo la nguzo ya umeme hadi Tela (Lesurenge) hekari 974 zimerejeshwa kwa watu na kugawanywa upya,” amesema.
Amesema mradi wa maji kutoka kijiji cha Loiborsoit B hadi Orkesumet umetekelezwa na Wizara ya Maji na umesambazwa katika maeneo ya zahanati ya Loiborsiret B, shule ya msingi Loiborsoit B na eneo la kitongoji cha Ngurashi kwenye makazi ya watu.
“Mradi wa maji kwenye kijiji cha Ngage kitongoji cha Ngage B, mradi huu umesambaza maji katika maeneo ya shule ya msingi Ngage, zahanati ya kijiji cha Ngage na kwenye makazi ya watu mitaani karibu na kwa kidevu, kwa Tesha na masaini karibu na boma la mzee Lembosho,” amesema.
Amesema katika sekta ya kilimo miradi ya maendeleo iliyotekelezeka ni usambazaji wa mbolea ya ruzuku kwa mwaka 2023/2024 ambapo takribani tani za mbolea ya urea (mbolea ya ruzuku) 462 kutoka kampuni za YARA na TFC na mbolea ya kupandia tani 128.
“Sumu za kuua wadudu (viuatilifu) kutoka Halmashauri ya Wilaya ya Simanjiro kwa ajili ya kuua wadudu wa viwavijeshi kwa zao la mahindi, takribani lita 4,500 zilisambazwa kwa wakulima wa vijiji vyote viwili,” amesema Diwani Siria.
Amesema uendelezaji wa skimu ya Songoyo takribani shilingi 15,670,000 zilikarabati banio na kutengeneza mfereji kwa sakafu, mawe, mita 100 na kufanya usanifu wa mfereji wa kilomita 2.5 ila zilitumika na nguvu za wananchi.
Amesema kwenye sekta ya mifugo kuna uanzishwaji wa majosho mawili ya Mazinde na Songoyo.
Amesema kwenye kata ya Loiborsoit idadi ya mifugo kuna ng’ombe 24,924 mbuzi 10,800 kondoo 10,095 na punda 1,056.
“Tumefanikisha ujenzi wa josho katika kijiji cha Loiborsoit B eneo la booster three, ujenzi huo umegharimu shilingi milioni 23, fedha zilizotolewa na Halmashauri ya Wilaya ya Simanjiro na nguvu kazi ya jamii ni shilingi milioni 3.5,” amesema.
“Kwenye hitimisho namshukuru Mwenyekiti wa CCM Kata ya Loiborsoit, Katibu Kata, wajumbe wote, wanachama na wataalam wote pamoja na viongozi kidini, kimila (malaigwanani) na wananchi wote,” amesema Diwani Siria.
No comments:
Post a Comment