Maombi watuhumiwa ujangili yatupwa, wanakesi ya kujibu, - MAIPAC MEDIA TANZANIA

Breaking

MAIPAC MEDIA TANZANIA

A Centre for Indigenous and Pastoralists Community Informations




Thursday 28 March 2024

Maombi watuhumiwa ujangili yatupwa, wanakesi ya kujibu,

 




Na: Mwandishi wetu,Babati


maipacarusha20@gmail.com


Mahakama ya  wilaya ya Babati imetupa maombi ya wakili wa utetezi katika kesi ya uhujumu uchumi inayowakabili watuhuhumiwa wawili wa  ujangajili wa Twiga na kutoa maamuzi kuwa wanakesi ya kujibu.


Kesi hiyo inawahusu Watuhumiwa wa ujangili,Paulo Himid John (23) Athuman Misanya(23)  waliokamatwa februari 2, 2024  wakiwa na nyama ya Twiga na mzoga wa Twiga ikiwa na thamani ya shilingi millioni 50,079,208.


 Watuhumiwa hao, walikamatwa katika eneo la hifadhi ya jamii ya Burunge na Shehena ya nyama ya Twiga hao na kikosi cha kupambana na ujangili ambacho kinaongozwa na Askari wa Mamlaka ya usimamizi wanyamapori(TAWA), kwa kushirikiana na askari wa Burunge WMA na chem chem association.


Katika kesi hiyo ambayo inasikilizwa na hakimu mfawidhi wa mahakama ya wilaya ya Babati,Victor Kimario ,Wakili wa watuhumiwa hao, wakili Justine Jackson juzi aliwasilisha maombi ya kutaka mahakama kuwaita upya mashahidi wawili  wa mashitaka ili awaulize maswali baada ya kupitia ushahidi waliotoa kwani ameanza kuwatetea wateja wake wakati tayari mashahidi wawili wa jamuhuri walikwishatoa  ushahidi .


Alisema baada ya kusoma jalada la mahakama aliomba mahakama   iwaite tena mashahidi waliokwisha kutoa ushahidi mahakamani ili yeye aje kwaajili ya kuwadodosa maswali kwa ushahidi walioutoa mahakamani hapo awali kabla ya wakili huyo kupewa kazi na wateja wake ya kuwatetea ( Recall the witnesses for further Cross-examination S.147(4) ya sheria ya ushahidi 


Hata hivyo, Waendesha Mashitaka wa Serikali  Getrude Kariongi na Shahidu Kajwagya kutoka TAWA na mwendesha mashitaka  Mahundi, walipinga ombi la Wakili wa Utetezi .


Kariongi alisema  Wakati shahidi wa Jamuhuri namba moja na namba mbili wakitoa ushahidi watuhumiwa walikuwepo na kusikiliza ushahidi wao, na watuhumiwa hawakusema wana nia ya kuweka wakili mbele ya mahakama na pia mahakama iliwapa nafasi ya kuwadodosa maswali (cross-examination) mashahidi hao.


Waendesha mashitaka hao walieleza ,watuhumiwa hao walipewa fursa ya kuwauliza maswali mashahidi lakini walisema hawana maswali.


Hivyo walieleza kwa mujibu wa kifungu cha 147 kidogo cha 4 cha sheria ya ushahidi inazungumzia maswali zaidi ( further cross-examination or examinations inchief ) ni kwa maana ya kwamba kama watuhumiwa walisema hawana maswali yaani hawakuuliza maswali kabisa na kwa sheria hiyo maswali zaidi ni  kuwe na swali  lililoulizwa na wakili apate nafasi ya kuendelea kuuliza maswali mengine kutokea pale lilipoulizwa swali la awali.


Pia upande wa mashtaka walinukuu Maamuzi  ya mahakama kuu Moshi katika kesi ya  Bakari Yahaya Ausen Msambaa dhidi ya Jamuhuri namba 646/2016 na maamuzi ya Kesi yaliyotolewa na  mahakama ya rufaa kwenye kesi ya Shomari Mohamedi Mkwama dhidi ya Jamuhuri  namba 606 mwaka 2021 iliyoketi Dar es salam ambayo ilieleza mazingira ya mashahidi kuitwa tena.


 Hivyo baada ya hoja hizo,  Hakimu mfawidhi Kimario  alitoa uamuzi mdogo  na kukataa ombi la upande wa utetezi kwani wakati wa ushahidi wa mashahidi hao watuhumiwa walipewa nafasi ya kuuliza maswali na  walisema hawana na pia baada ya kusoma maamuzi ya kesi za mahakama ya rufaa mahakama imejirisha kwamba mazingira ya hizo yanafanana kabisa na kesi hiyo hivyo anaungana na maamuzi ya waheshimwa Majaji na kukataa ombi la kuita mashahidi kwa upya.


Alisema kutokana na maamuzi hayo kesi iedelee na shahidi wa upande wa Jamhuri ,Afisa Wanyamapori Godluck James ambaye alitoa ushahidi wake na kuwataja watuhumiwa kuhusika na ujangili.


Baada ya ushahidi huo, Jamhuri ilifunga ushahidi wake ambapo Hakimu Kimario alieleza baada ya kupitia ushahidi watuhumiwa wanakesi ya kujibu na hivyo  na watuhumiwa wataanza kujitetea.


Kesi hiyo ambayo inafatiliwa na watu wengi wakiwepo wadau wa uhifadhi na maafisa wa serikali imepangwa kuiendelea kusikilizwa April 17 mwaka huu 


 Wadau uhifadhi wapongeza mahakama Babati.


Katika hatua nyingine wadau wa uhifadhi wamepongeza mahakama ya wilaya Babati kwa hatua ambayo imeendelea kuchukuwa kukomesha ujangili.


Mhifadhi Joram Peter alisema wao kama wadau wa uhifadhi wanaridhishwa na hatua ambazo zimekuwa zikichukuliwa na mahakama na serikali kwa ujumla kukabiliana ujangili.


"Tunawashukuru sana watendaji wa mahakama akiwepo hakimu Kimario kweli wanatenda haki kuhakikisha rasilimali za taifa zinalindwa kwa manufaa ya sasa na vizazi vijavyo.



No comments: