RC MONGELLA ATATUA MGOGORO WA KIWANJA NJIRO; AAGIZA KAMISHNA KUTAO HATI NDANI YA SIKU SABA. - MAIPAC MEDIA TANZANIA

Breaking

MAIPAC MEDIA TANZANIA

A Centre for Indigenous and Pastoralists Community Informations




Tuesday 19 March 2024

RC MONGELLA ATATUA MGOGORO WA KIWANJA NJIRO; AAGIZA KAMISHNA KUTAO HATI NDANI YA SIKU SABA.

 


Na Elinipa Lupembe, Arusha


maipacarusha20@gmail.com


Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Mhe. John V.K.Mongella, ametatua mgogoro wa Kiwanja namba 624 na 625 Block F eneo la Njiro, Jijini Arusha, mgogoro uliodumu zaidi ya miaka 17, na kuwataka Maafisa Ardhi kuandaa hati ndani ya siku 7. 


Mhe. Mongella ametatua mgogoro huo, mara baada ya kuzungumza na kwenda eneo la kiwanja na walalamikaji Anansia Everest na mwenzake waliowalalamikia Maofisa wa Ardhi kumgawia eneo la kiwanja hicho mtu mwingine anayejulikana kwa jina la Jeina.


Baada ya mazungumzo ya kina, kutoka pande zote, Mhe. Mongella amewaagiza Kamishna wa Ardhi mkoa wa rusha, kutengeneza hati za watu wote watatu kwa kutumia 'title deed' iliyopo na kurekebisha ukubwa wa viwanja hivyo ili wote watatu wapate hati miliki mpya kila mmoja na eneo lake.


"Kwa kuwa 'title deed na code nates' zipo, ninawapa wiki moja kufanya hili zoezi, rekebisheni ukubwa wa eneo, andaeni hati nyingine, kila mmoja apate hati mpya, kiwanja kimoja kitakuwa na mita za mraba 588, cha pili 740 na wa tatu atabaki na mita za mraba 440 na kila mmoja anapopewa hati mpya arudishe ile hati ya awali" Amefafanua Mhe. Mongella


Hata hivyo, walalamikaji wote wameridhishwa na maamuzi hayo na kukubali kupatiwa hati mpya kwa mujibu wa maelekezo yaliyotolewa na Mkuu wa mkoa huyo kulingana na title deed iliyopo.


Naye mlalamikaji wa kwanza, Anasia Evarest Malewas, amemshukuru mkuu wa mkoa, kwa kufanya maamuzi yanye hekima na busara ambayo yametuwezesha wote kupata haki, na sio kupata haki bali kila mmoja kupata eneo, eneo ambalo tumelihangaikia kwa muda mferu.


"Binafsi ninamshukuru mkuu wa mkoa, Mungu ambariki sana,  ninaamini sote tutapata haki yetu, ambayo tumezunguka kuhangaika na eneo hili, kwa miaka 17 sasa, huyu baba Mungu ambarikia sana" Amesema Anansia


Lembris Kipuyo, ambaye ni mtetezi wa walalamikaji ambao amedai yeye ni mtetezi na mwakilishi wa wajane, amemshuru pia mkuu wa mkoa kwa maamuzi mazuri yanayokwenda kuwapa haki kina mama hao wajane ambao walikuwa na hati na wakizilipia lakini viwanja vyao vilikuwa na mkanganyiko wa kiufundi.


Aidha, ametoa wito kwa Maofisa wa Ardhi, kutambua na kuthamini kazi wanayoifanya kwa kutenda haki kwa watanzania na sio kuwa vyanzo vya migogoro, migogoro haijengi bali inajeruhi mioyo ya watu na kusababisha chuki miongoni mwa wanajamii ni vyema kuiepuka


Hata hivyo, Kamishna wa Ardhi mkoa wa Arusha, Geophray Mwamsojo, ameahidi kusimamia zoezi hilo na kuhakikisha hati hizo zinapatikana ndani ya siku 7 kama yalivyo maagizo na maelekezo ya Mheshimiwa mkuu wa Mkoa.


"Hapa changamoto ilikuwa ni uelewa mdogo na makubalino baina ya wateja wetu, tunashukuru leo RC ameweka hili jambo sawa, wameelewa na wote wameridhika, tunakwenda kuwapa hati zao kama ilivyokusudiwa,,lengo ni kuhakikisha kila mmoja amepata hati yake" Amefafanua Kamishina huyo wa Ardhi.

No comments: