VIONGOZI VYAMA VYA MPIRA WA MIGUU WANAWAKE WATAKIWA KUWEKEZA KWA VIJANA - MAIPAC MEDIA TANZANIA

Breaking

MAIPAC MEDIA TANZANIA

A Centre for Indigenous and Pastoralists Community Informations




Monday 25 March 2024

VIONGOZI VYAMA VYA MPIRA WA MIGUU WANAWAKE WATAKIWA KUWEKEZA KWA VIJANA

 

KATIBU Mkuu wa chama cha mpira wa miguu kwa wanawake nchini , TWFA, Somoe Ng'itu akizungumza na Viongozi wa mikoa na Wilaya 



Na: Lilian Kasenene, Morogoro


maipacarusha20@gmail.com


Viongozi wa  chama cha mpira wa miguu kwa wanawake nchini, TWFA, ngazi za mikoa na wilaya wametakiwa kuwekeza kwa vijana kwa kuanzisha mashindano ili kuibua vipaji vya wachezaji wanawake watakaodumu kwa muda mrefu kimichezo.


KATIBU Mkuu wa chama hicho cha mpira wa miguu kwa wanawake nchini , TWFA, Somoe Ng'itu alisema hayo mjini Morogoro wakati akifungua Mkutano mkuu wa chama cha mpira wa miguu kwa wanawake mkoa wa Morogoro, MWFA ambapo akahimiza ushirikiano miongoni mwa viongozi na wadau wa soka Ili kuinua mchezo huo kwa wanawake.


Somoe alisema kwa kuanzisha   timu za vijana na watoto  chini ya ya umri wa miaka 21, 17 na 14 kutasaidia kuwa na timu imara zitakazocheza na kushindana Katika michuano mbalimbali ndani na nje ya Tanzania.


Katibu Mkuu  huyo wa TWFA ambaye pia ni Kamishna wa michezo wa Shirikisho la soka barani Afrika, CAF,  akawahimiza viongozi WA soka la wanawake kuanzisha utaratibu wa kuwapata watoto wa kike wanaopenda mpira kuanzia ngazi ya chekechea na shule za msingi Ili kutengeneza timu nzuri za wanawake kuanzia ngazi za chini.


Kuhusu ushirikiano, alisema ni vyema  viongozi na wadau wa soka kushirikiana Ili kuendeleza soka la wanawake ambalo limekuwa na fursa kubwa ikiwemo ajira.


"Mahali popote penye mshikamano na upendo  huwa wafadhili wanajitokeza na kusaidia lakini kama hakuna ushirikiano hakuna mdau atakayejitokeza kusaidia timu,Sikilizeni ushauri wa wadau,fuateni katiba na maelekezo ya TWFA na MWFA lakini pia ya TFF na MRFA ili msonge mbele kwa manufaa ya mpira wa wanawake"Alisisitiza Somoe.


Kwa upande wake Mwenyekiti wa MWFA Beatrice selemani alisema  chama hicho kimedhamiriia kuweka mazingira mazuri ya kuchezwa mpira wa miguu wa wanawake mkoa mzima na kuimarisha utendaji Kazi wenye weledi katika ngazi zote.


Alusema katika kuhakilkisha kiwango cha  soka la wanawake kinainuliwa ni lazima ushirikishwaji uwepo katika ngazi zote za uongozi na utawala na MWFA kwa kushirikiana na wadau wa soka ni lazima wakae pamoja kujadili kwa kina mchezo huo ambao umeshika kasi kubwa na kutoa ajira kwa watoto wa kike.


"Tunatoa wito kwa wadau mbalimbali kujitokeza Ili kuunga mkono uendeshaji wa  soka la wanawake mkoa wa Morogoro, mwaka huu tumejipanga  na kuelekeza nguvu zaidi kuhakikisha soka la wanawake linachezwa kila wilaya, kutoa elimu na mafunzo kwa viongozi wa vyama vya wilaya vya soka la wanawakel na kuzalisha walimu wa soka wenye taaluma ya kutosha"aliongeza Mwenyekiti huyo wa MWFA.


Akaongeza kuwa upo umuhimu mkubwa wa wazazi kuwaelimishwa  wawaruhusu watoto wao wa kike kucheza mpira wa miguu kwani ni sehemu pia ya ajira kwao.


Naye Mjumbe wa Mkutano Mkuu Taifa wa TWFA akiwakilisha Mkoa wa Morogoro,Idda Mushi, aliwahimiza wachezaji wa kike kulinda nafasi yao ya uanamke wakishiriki michezo Ili kutopoteza uhalisia wao.


"Kama unasuka basi suka, kama unabana nywele bana, kucheza mpira hakukufanyi ubadili jinsia uwe mwanaume, uvae na kutembea kama mwanaume, unyoe kama mwanaume, lindeni uhalisia wenu kama wanawake"Alisema Idda.


Aidha Mwenyekiti wa chama cha mpira wa Miguu mkoa wa Morogoro, MRFA  , Paschal Kihanga, alihimiza mafunzo zaidi kutolewa kwa  walimu wa soka yaani makocha Ili wasaidie kufundisha soka kwani kwa kuwa na viongozi peke yao na wachezaji bila makocha haitasaidia kuendeleza mpira wa miguu.


'Niwahimize na makocha kuwa na timu za soka za wanawake, zikifanya vizuri sifa zinakuja kwenu, timu hizi ni sehemu ya kujitangaza na nyie kufahamika"Alisema Kihanga ambaye pia ni Meya wa Manispaa ya Morogoro.


Mmoja wa makocha wanaotambulika na CAF, Meja Sijovelwa Tandika kutoka JWTZ  Kikosi cha mazao,akawahimiza walimu wa Soka kutambua nafasi yao ya utaalamu kwenye soka na kubobea katika eneo hilo sambamba na kuwa na ratiba ya kile wanachokusudia kuwafundisha wachezaji, kupata mrejesho wa wanachofundisha Toka kwa wachezaji na kutafuta suluhisho la matatizo wanayogundua.


Katika mkutano huo  Somoe alikabidhi mipira miwili kwa MWFA ambayo alidai kupewa na TFF waliopata FIFA, Huku Mwenyekiti MRFA akatoa mipira saba, mmoja kwenye kila wilaya, kwaajili ya kusaidia kuendeleza soka la wanawake mkoani Morogoro.



No comments: