Mussa Juma, Maipac
maipacarusha20@gmail.com
Watafiti na Wahifadhi nchini wanakutana kwa siku mbili jijini Arusha kwa lengo la kujadili matumizi ya Technolojia za kisasa katika uhifadhi na mikakati ya pamoja ya kuimarisha uhifadhi na kukuza utalii nchini .
Mkutano wa watafiti na wadau wa uhifadhi ni sehemu ya maadhimisho ya Siku ya Wanyamapori Duniani ambayo huadhimishwa Machi 03 kila mwaka.
Kaimu Mkurugenzi wa ldara ya Wanyamapori nchini Dk Fourtunata Msoffe |
Akifungua mkutano huo ambao umeratibiwa na Wizara ya Maliasili na Utalii, Kaimu Mkurugenzi Idara ya Wanyamapori Dk. Fortunata Msoffe amesemakuwa wakati Taifa likiwa kwenye maombelezo ya kifo cha
aliyekuwa Rais wa awamu ya pili hayati Alli Hassan Mwinyi ni muhimu kwa wahifadhi na watanzania kwa ujumla kuenzi jitihada za viongozi katika kutunza Maliasili ya Wanyamapori.
Dkt. Msoffe amesema hayati Mzee Mwinyi amekuwa na mchango mkubwa kwenye uhifadhi wa rasilimali za wanyapori.
" Kuanzia awamu ya kwanza ya baba wa Taifa hadi sasa ambapo Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan viongozi wetu wamekuwa wahifadhi namba moja nchini wenye maono makubwa kwenye Uhifadhi wa raslimali na kukuza Utalii nchini.
"Hapa naomba nisisitize kuwa wamefanya jitihada kubwa kuhakikisha Maliasili inakuwepo kwa kizazi kilichopita, kilichopo na kijacho ili ziendelee kunufaisha Taifaletu" alisema Dk Msofe .
Mkutano huu unafanyika wakati Wizara ya Maliasili na Utalii ikiwa katika mkakati mkubwa wa kukuza Utalii lakini pia kukabiliana na changamoto za uhifadhi.
Miongoni mwa changamoto hizo ni pamoja na ongezeko la migogoro baina ya wanyamapori na Binaadamu lakini pia uvamizi maeneo ya Mapito ya Wanyamapori (Shoroba)
Waziri wa Maliasili na Utalii, Angellah Kairuki tayari ametangaza mkakati wa kuyapima na kuyalinda maeneo 20 ya Shoroba nchini ili kuendeleza uhifadhi.
Miongoni mwa maeneo hayo ni Shoroba ya Kwakuchinja ambayo ipo katika eneo la Ikolojia la Tarangire -Manyara.
Mkutano huo umejumuisha Watafiti na Wahifadhi kutoka Idara za Wanyamapori, Misitu na Malikale, Taasisi ya Utafiti wa Wanyamapori Tanzania (TAWIRI), Shirika la Hifadhi za Taifa (TANAPA),
Washiriki wengine ni Mamlaka ya Uhifadhi Ngorongoro (NCAA), Mamlaka ya Uhifadhi wa Wanyamapori (TAWA), Wakala wa huduma za Misitu (TFS), Chuo cha Wanyamapori Mweka na wadau kutoka taasisi zisizo za kiserikali za WWF, FZS, CWMAC, Nature Tanzania, TNRF na AWF.
Katika maadhimisho ya mwaka huu. Kaulimbiu ni‘ *"UNGANISHA WATU NA ULIMWENGU: VUMBUA MATUMIZI YA TEKNOLOJIA YA KIDIGITALI KATIKA UHIFADHI WA WANYAMAPORI"*
Katika mkutano huo pia taarifa mbalimbali za tafiti zinatarajiwa kutolewa katika kuimarisha uhifadhi nchini.
No comments:
Post a Comment