UJENZI WA KITUO KIPYA CHA UTAFITI WA WANYAMAPORI NYANDA ZA JUU KUSINI KUANZA RASMI MKOANI IRINGA. - MAIPAC MEDIA TANZANIA

Breaking

MAIPAC MEDIA TANZANIA

A Centre for Indigenous and Pastoralists Community Informations




Thursday 18 April 2024

UJENZI WA KITUO KIPYA CHA UTAFITI WA WANYAMAPORI NYANDA ZA JUU KUSINI KUANZA RASMI MKOANI IRINGA.

 


Na Mwandishi wetu


maipacarusha20@gmail.com


Taasisi ya Utafiti wa Wanyamapori Tanzania (TAWIRI) inaendelea kupanua wigo wa tafiti za wanyamapori kwa ustawi wa uhifadhi na  kukuza utalii nchini ambapo, tarehe 13 Aprili 2024 zoezi la  utiaji saini nyaraka za makabidhiano ya eneo la  ujenzi wa kituo kipya cha utafiti  Nyanda za Juu Kusini katika eneo Kihesa-Kilolo Mkoani Iringa kwa Mkandarasi limefanyika .


Ujenzi wa kituo hiko unatekelezwa kupitia mradi wa Kuboresha Usimamizi wa Maliasili na Kukuza Utalii Kusini mwa Tanzania (REGROW) ambao umejikita kuboresha miundombinu, kuwezesha tafiti na kuboresha Maisha ya Jamii yanayozunguka hifadhi za Taifa za Udzungwa, Mikumi, Ruaha na Nyerere kwa utalii endelevu. 


Akitia saini Nyaraka hizo  kwa niaba ya Wizara ya Maliasili na Utalii, Dkt.Edward Kohi ambaye ni Mkurugenzi wa Takwimu na Mafunzo wa Wizara hiyo, amesema Serikali inaendelea kuwekeza kwenye miundombinu ya Utafiti itakayosaidia kupata taarifa za kisayansi  zitakazo tumika kwa uhifadhi endelevu na kuandaa bidhaa za utalii kusini.


Aidha, Dkt.Kohi amesema kituo cha Utafiti Nyanda za Juu Kusini  kina mchango mkubwa katika kukuza utalii ambapo amemtaka mkandarasi kufanya kazi ikiwezekana mchana na usiku ili kukamilisha ujenzi wa jengo hilo katika kipindi cha miezi 10 ya mkataba sambamba na TAWIRI kuhakikisha watumishi  wa kituo hicho wanakuwepo.


Kwa upande wake  Mkurugenzi  Mkuu  TAWIRI, Dkt Eblate Mjingo amebainisha manufaa ya kituo hicho ni kuharakisha  zoezi la  kufanya, kusimamia na kuratibu Tafiti za wanyamapori  katika eneo la kusini pamoja na kuwezesha ukaribu baina ya wadau wa uhifadhi, watafiti na waongoza utalii waliopo maeneo ya kusini. 


Naye Mwenyekiti wa Bodi ya wakurugenzi TAWIRI, Dkt.David Manyanza amesema Kituo cha Nyanda  za  Juu  Kusini kitawezesha juhudi za Mhe Dkt Samia Suluhu Hassan za kuitangaza nchi kupitia vivutio vyake ikizingatiwa Tanzania  ina utajiri mkubwa wa Maliasili  ya Wanyamapori  katika maeneo mbalimbali ikiwemo  eneo la kusini.


TAWIRI  ina vituo vinne vya utafiti ambavyo ni Njiro -  Arusha, Serengeti , Kingupira, Kituo cha Magharibi na Kituo hiki kipya cha Nyanda za Juu Kusini  kinakamilisha idadi ya vituo  vitano.

No comments: