Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya mifugo na uvuvi anayeshughulikia mifugo Profesa Daniel Mushi akizungumza na wadau wa mifugo |
Baadhi ya wadau wa mifugo wakimsikiliza Naibu Katibu Mkuu Daniel Mushi |
Na Lilian Kasenene, Morogoro
maipacarusha20@gmail.com
Wizara ya Mifugo na Uvuvi imeeleza kuwa inatamani kuwa na maghala makubwa ya kuhifadhi malisho katika kila Halmashauri ili kuepuka changamoto ya ukosefu wa chakula kipindi Cha ukame.
Naibu Katibu Mkuu wa Wizara hiyo anayeshughulikia mifugo Profesa Daniel Mushi alisema hayo mjini Morogoro katika siku ya Malisho na Kongamano la Kisayansi la Nyanda za Malisho Tanzania linaloendelea.
Alisema kama kila Halmashauri itatenga na kujenga maghala ya Malisho kama ilivyo kwa Wizara ya Kilimo ambayo ina maeneo mengi yenye maghala ya kuhifadhi mazao mfano mahindi, ni Imani yake kuwa suala la mifugo kufa kwa wingi kipindi Cha ukame litaondoka kama sio kupungua.
Prof. Mushi alisema Wizara ya Mifugo kwa kushirikiana na OR-TAMISEMI, Tume ya Taifa ya Mipango ya Matumizi ya Ardhi na wadau wengine imeandaa mipango ya matumizi ya ardhi na kutenga maeneo ya malisho.
Wizara inaendelea kuhimiza utekelezaji wa Sheria ya Maeneo ya Malisho na Rasilimali za Vyakula vya Wanyama Sura 180 na Mwongozo wa Uendelezaji, Upatikanaji na Usimamizi wa Maeneo ya Malisho wa mwaka 2021 kwenye Halmashauri zote nchini ambapo utekelezaji utasaidia kuhakikisha upatikanaji wa malishao katika maeneo ya wafugaji yaliyopo kwenye Halmashauri.
"Tunahamasisha Halmashauri ziendelee kutenga bajeti na kushirikiana na wafugaji kuwezesha uandaaji wa mipango ya matumizi ya ardhi, upimaji na uwekaji wa alama zinazoonekana kwenye maeneo yaliyotengwa kwa ajili ya malisho ili tuweze kuyasajili na kupata ulinzi wa kisheria yasibadilishiwe matumizi na wafugaji wetu wafuge kwa kutulia katika maeneo hayo,"alisema.
Alisema maeneo ya malisho yamekuwa yakipungua na kupoteza ubora kutokana na sababu mbalimbali ikiwemo kuongezeka kwa watu, mifugo na shughuli nyingine za kiuchumi. Mfano idadi ya watu wakati wa uhuru ilikuwa milioni 9 na mifugo milioni 8, lakini kwa mujibu wa takwimu ya sensa ya watu na makazi ya mwaka 2023 idadi ya watu imeongezeka kufikia takribani milioni 61 na mifugo imeongezeka kufikia milioni 81.4 mwaka 2023/2024 wakati ardhi haiongezeki.
Alisema kutokana na changamoto wadau wananawajibu wa kuhakikisha wanaboresha maeneo ya malisho, wanafuga kisasa mifugo bora kwenye ardhi iliyopo iliyotengwa kwa ajili ya mifugo.
Kwa upande wake msajili wa Bodi ya Maziwa na katibu mkuu wa Chama Cha Nyanda za Malisho Prof George Msalya alisema Tanzania ni nchi ya pili kwa mifugo Afrika baada ya nchi ya Ethiopia hivyo ili mazao yaweze kustawi vyema lazima Nyanda za Malisho zihifadhiwe vizuri ili kuweza kupata mahitaji kama chakula, maji na makazi.
Aidha Prof Msalya alisema mabadiliko ya tabia nchi yamekuwa yakisababisha hali na Nyanda za Malisho kuhalibuka na kupungua.
Alisema pamoja na kufanyika kwa mkutano huo nchi nne zitashitiki kwa njia ya mtandao kwa kutoa uzoefu namna wanavyokabiliana na suala la ukame linalosababisha mifugo kufa na nchi hizo ni pamoja na Marekani,Argentina,Uzbekistan pamoja na Tanzania.
Naye Mkurugenzi Nyanda za Malisho na vyakula vya mifugo, Wizara ya Mifugo na Uvuvi Dk Asimwe Rwiguza,alisema wadau watahakikisha kutafuta suluhu ya changamoto zote zinazokabili maeneo ya malisho nchini na hivyo kuwa na afya bora ya Nyanda za malisho kwa maendeleo endelevu ya kiuchumi.
Alisema mkutano uwe fursa ya kujadili na kuweka mikakati madhubuti katika kuwezesha ustawi wa Sekta ya Mifugo hasa kuhusiana na upatikanaji wa malisho, kwani malisho ni muhimu katika uendelezaji na uzalishaji wa mifugo na mazao yake.
Pia changamoto zinazowakabili wafugaji na namna ya kuzitatua ili kufikia malengo ya ufugaji wenye tija kwa kuhakikisha kunakuwepo na upatikanaji wa malisho ya kutosha kama rasilimali muhimu kwa ajili ya mifugo.
Mwisho.
No comments:
Post a Comment