CCM MORO YAITAKA CHADEMA KUACHA UPOTOSHAJI NA KUHARIBU MICHAKATO YA SERIKALI - MAIPAC MEDIA TANZANIA

Breaking

MAIPAC MEDIA TANZANIA

A Centre for Indigenous and Pastoralists Community Informations




Wednesday 8 May 2024

CCM MORO YAITAKA CHADEMA KUACHA UPOTOSHAJI NA KUHARIBU MICHAKATO YA SERIKALI

 




Na Lilian Kasenene, Morogoro 


maipacarusha20@gmail.com


CHAMA cha Mapinduzi (CCM) mkoa wa Morogoro kimekitaka chama cha Demokrasia na maendeleo (CHADEMA) kuacha tabia ya upotoshaji kwa wananchi ikiwemo mchakato wa ukusanyaji maoni ya katiba mpya wa Tume ya Jaji Warioba kwa kuingiza misimamo isiyothabiti ya uwepo wa Serikali ya Tanganyika jambo ambalo si kweli.


Katibu wa Siasa, Uenezi na mafunzo CCM mkoa wa Morogoro Zangina Shanang alisema hayo wakati akizungumza na vyombo vya habari kwenye ofisi za CCM mkoa wa Morogoro.


Alisema kauli za upotoshaji zilizotolewa na Makamu Mwenyekiti wa CHADEMA Tundu Lissu wakati wa mkutano baada ya maandamano mwishoni mwa mwezi Aprili hazivumiliki kuzinyamazia.


Alisema watanzania wanapaswa kutambua kuwa mpango wa Serikali ya Tanganyika uliibuka kwenye katiba ya Tume ya Jaji Warioba kwa kuwa UKAWA waliubaka mchakato wa tume hiyo na kuiaminisha kuwa ilikuwa inakusanya maoni ya wananchi lakini kiuhalisia CHADEMA ilipita kila mkoa kupandikiza watu ili waingize misimamo yao.


Hivyo aliwataka CHADEMA kuacha kulazimisha kuwepo kwa Serikali ya Tanganyika itakayoongeza mzigo wa kodi kwa watanzania sababu Serikali mbili zinatosha ambapo alisema kama wanataka Serikali tatu waanze na kubadilisha kwenye salamu yao kwa kuonesha vidole vitatu badala ya viwili na sio kuwarubuni wananchi.


Zangina alisema agenda ya uwepo wa Serikali ya tatu ya Tanganyika kuwa ni TAMISEMI sio hoja ya msingi sababu haipo na TAMISEMI ni Wizara ya Tawala za mikoa na Serikali za Mitaa ambayo ipo ndani ya Serikali Tanzania.


Aliitaka CHADEMA kutolazimisha agendaya serikali tatu ionekane ni hitajio la wananchi wakati ni mpango wa CHADEMA wa kuongeza utitiri wa Madaraka na kutaka kujiimarisha kisisasa na kisha kuuvunja muungano wa kuwa wamejaa roho ya ubaguzi kwa Zanzibar.


Aidha aliitaka CHADEMA kuacha kupotosha kuwa watanzania wananyimwa ardhi na ajira Zanzibar licha ya Muungano bali aliwataka kutambua kuwa kutopatikana nafasi hizo Zanzibar kutokana na utofauti wa idadi ya watu na kilometa za mraba zilizopo ukilinganisha na Tanzania bara.


Alisema Tanzania bara kuna jumla ya idadi ya watu Milioni 61.7 kwa mujibu wa sensa ya watu na makazi ya mwaka 2022 huku kukiwa na eneo lenye ukubwa Kilometa za mraba 945,000 na Tanzania visiwani kuna watu Milioni 1.8 na ukubwa wa ardhi ukiwa ni Kilometa za Mraba 1,650.


Hata hivyo alikemea tabia ya kuita uondoaji wafugaji kwenye hifadhi za Wanyama kuwa ni hoja za kitoto bali aliitaka jamii kutambua kuwa wafugaji wanazaliana mifugo inazaliana lakini ardhi haizaliani na kadri watu wanavyoongezeka ndivyo migogoro inavyozidi kuibuka kutokana na kuzaliana kwa mifugo na Wanyama kwenye ardhi ndogo.


Aidha aliitaka CHADEMA kutambua kuwa katiba sio taarifa ambayo unaweza kuiandika na kuifyatua haraka kama gazeti bali ni mwongozo ama sheria mama ya Taifa ambapo lazima mchakao wake ufanywe kwa utulivu mkubwa na umakini na si kushinikiza kupatikana katiba mpya kwa maandamano.


Hivyo aliishauri CHADEMA kuishukuru Serikali ya awamu ya sita kwa kutekeleza vyema dhana ya maridhiano na vyama vya upinzani na kuacha kushutumu sababu maandamano na mikutano wanayofanya ni sehemu ya utekelezaji wa maridhiano yao.


No comments: