ARCHRAF HAKIMI WA PSG, ATOA MISAADA YA ZAIDI YA BILIONI MOJA KWA WANAFUNZI WENYE MAHITAJI MAALUM PATANDI JIJINI ARUSHA - MAIPAC MEDIA TANZANIA

Breaking

MAIPAC MEDIA TANZANIA

A Centre for Indigenous and Pastoralists Community Informations




Thursday 27 June 2024

ARCHRAF HAKIMI WA PSG, ATOA MISAADA YA ZAIDI YA BILIONI MOJA KWA WANAFUNZI WENYE MAHITAJI MAALUM PATANDI JIJINI ARUSHA

 






Na: John Mapepele, Arusha


maipacarusha20@gmail.com 


Mchezaji wa kimataifa wa  soka kutoka Morocco anayechezea timu ya PSG, Archraf Hakimi leo  ametoa msaada wa  vifaa mbalimbali kwa wanafunzi  zaidi ya 400 wenye uhitaji maalum kwenye shule ya Sekondari ya Patandi ya jijini Arusha vyenye gharama ya zaidi ya bilioni moja.


Baadhi ya vifaa hivyo ni pamoja na  komputa zaidi ya 50,  samani,  vifaa maalum alama nundu, Mashine za kuchomea taka na kuchemshia maji.


Katika hafla hiyo ambayo Waziri wa Maliasili na Utalii Mhe. Angellah Kairuki alikuwa mgeni rasmi ambapo aliwakilishwa na Katibu Mkuu wa Maliasili na Utalii, Dkt. Hassan Abbasi mchezaji huyo ameipongeza  Serikali inayoongozwa na Rais  Samia Suluhu Hassan kwa jitihada  kubwa zinazofanyika katika kutoa huduma za elimu kwa watoto wenye uhitaji maalum.


Mchezaji huyo ambaye ni mara yake ya kwanza kutoa misaada kupitia taasisi yake nje ya nchi ya Morocco ameuhakikishia Serikali kuwa ataendelea kushiriki kikamilifu kutoa misaada kwa jamii hapa nchini.


Aidha, Hakimi ambaye ameletwa nchini kwa mwaliko maalum wa Rais wa Yanga Mhandisi Hersi Said amesema amevutiwa na vivutio vya Utalii na kuahidi kuja tena.


Hakimi ni miongoni mwa wachezaji nguli duniani ambaye anawafuasi zaidi ya milioni 20 duniani pia ameshukuru Yanga, Wizara ya Maliasili na Utalii na Bodi ya Utalii kwa uratibu mzuri wa ziara yake.


Kwa upande wake Dkt. Abbasi amemshukuru Hakimi kwa misaada yake  na Mhandisi Hersi kwa kusaidia kuleta  watu mashuhuri kama Hakimi   ambao wanashaidia kutangaza utalii wa Tanzania na kutoa wito kwa watu wengine kufanya hivyo 


"Nakumbuka siku ambayo  Injinia ulikutana na Hakimi  Paris ulinipigia simu kuwa una "surprise" na ukasema tunataka kumletea Hakimi nikasema sawa kabisa mlete" amefafanua Dkt. Abbasi


Aidha, Dkt. Abbasi ameendesha harambee ya kuchangia  shule hiyo ambapo Klabu ya Yanga imetoa vitanda 40 na magodoro yake, na wadau wengine ambao waliweza kutoa zaidi ya milioni mbili na laki sita  na ahadi ya milioni 3.



Injinia Hersi amempongeza Mkuu wa shule ya Sekondari ya Patandi kwa  ufanyaji kazi wake  ambapo pia amefafanua kuwa wazo la kuichagua shule ya Sekondari ya Patandi lilitoka kwa Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe Angellah Kairuki.



Katika hafla hiyo wizara imeweza kumpatia zawadi Hakimi, Rais wa Yanga na Mkuu wa shule ya Sekondari ya Patandi Janeth Mollel kabla ya Hakimi kucheza mpira na vijana wafuasi wa Yanga.

No comments:

Post a Comment