EACOP kushirikiana na vyombo vya habari ili kukuza uelewa kwa jamii - MAIPAC MEDIA TANZANIA

Breaking

MAIPAC MEDIA TANZANIA

A Centre for Indigenous and Pastoralists Community Informations




Wednesday 26 June 2024

EACOP kushirikiana na vyombo vya habari ili kukuza uelewa kwa jamii

 


Na Mwandishi Wetu, maipac 


maipacarusha20@gmail.com 


UONGOZI wa Mradi wa Bomba la Mafuta Ghafi la Afrika Mashariki (EACOP), umeahidi kushirikiana na vyombo vya habari nchini, ili kuhakikisha hatua zote za utekelezaji wa mradi Watanzania wanajua na kuelewa.


Ahadi hiyo ilitolewa na  Mkuu wa Mawasiliano wa EACOP upande wa Tanzania, Catherine Mbatia, wakati akizungumza na waandishi na wahariri wa vyombo vya habari kutoka vyombo mbalimbali, mwishoni mwa wiki.


Katika semina hiyo Mbatia na wenzake waliwaeleza washiriki hatua ambazo mradi huo imefikia na kwamba matarajio yao ni mradi kukamilika katika muda uliopangwa.


Mbatia amesema wameamua kukutana na kundi hilo la waandishi na wahariri wakiamini kuwa ni watu muhimu ambao watasaidia jamii kupata taarifa sahihi.


“Sisi kama EACOP tutafanya kazi kwa karibu sana na waandishi wote wa habari. Tunaamini nyinyi ni wadau muhimu wa mradi huu. Mkiuelewa jamii na umma mzima wa Watanzania watauelewa,” amesema Mbatia.


Mkuu huyo wa Idara amesema mradi upo kwenye hatua nzuri na matarajio yao ni siku chache zijazo uchimbaji wa mtaro wa usambazaji bomba utaanza, ili ifikapo 2030 mafuta ghafi kutoka Uganda yaanze kusafirishwa.  


Mbatia amesema kwa sasa wanakusanya mabomba kwenye karakana iliyopo mkoani Tabora ili kuendelea na hatua nyingine muhimu kabla ya kufukiwa chini.


Amesema mikakati yao ni kuhakikisha waandishi wanapata nafasi ya kuona hatua kwa hatua ya utekelezaji wa mradi ili waweze kuandika habari sahihi.


"Bomba la mradi wa EACOP  lina urefu wa kilomita 1,443 na linaanzia Wilaya Hoima nchini  Uganda  hadi  Rasi ya Chongoleani, jirani na Bandari ya Tanga. Ndani ya Tanzania bomba lina urefu wa kilometa 1,147 na kilometa 296 zilizobaki zimo ndani  ya Uganda.  Bomba linapita katika mikoa  ya Kagera, Geita, Shinyanga, Tabora, Singida, Dodoma, Manyara hadi Tanga.


Mhariri Nevile Meena, (Brains Media) ilifurahishwa na ahadi  ya uongozi wa EACOP juu ya ushirikiano baina na ya pande zote mbili; kazi iliyofanywa mpaka sasa na kusema kuwa  semina imewafungua macho na  kuwajengea uelewa wa pamoja wa mradi. 


Aliongeza kwamba  kwa uelewa huo siku zijazo wahariri wataweza kutoa taarifa sahihi kwa umma kuhusu hatua zote za maendeleo ya mradi huo.  Mhariri Meena pia ni  Mjumbe wa Kamati ya Utendaji wa Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF).


“Kazi kubwa sana imefanyika katika suala zima la maandalizi na wananchi wameshirikishwa ipasavyo katika eneo zima la mradi. Naipongeza EACOP kwa kazi nzuri sana ambayo wamefanya,” amesema Meena.


Aliwashauri wahariri kutumika weledi na kuwa makini wanapozihariri taarifa zinazohusiana na mradi huo na kujitahidi kuueleza umma  faida zinazotokana na mradi huo ambazo alisema  ni nyingi kwa jamii.


Mhariri Mgaya Kingoba, (Habari Leo), amesema semina imewafanya wahariri  kuufahamu vizuri mradi na kusema kuwa  kuna ushahidi fidia imetolewa kwa wananchi  ambako mradi umepita.


“Kwa hatua ya awali tumeona fidia imeshatolewa na tumeona tayari nyumba zaidi ya 400 zimeshajengwa. Mimi ni shahidi. Binamu yangu amelipwa fidia ya shamba lake pamoja mali zote  zilimo mle. Anaishi  wilaya ya Handeni, Mkoa wa Tanga,” amesema Kingoba.


Mhariri huyo alieleza kuwa  mradi wa EACOP una maslahi mapana ya kiuchumi na kijamii  kwa Tanzania na Uganda na kwamba  mradi huo  utasaidia kuchochea mzunguko wa pesa kutokana na ajira nyingi za moja kwa moja. 


Amesema kuna uwezekano mkubwa wa mradi kuchochea  maendeleo ya haraka katika mikoa nane  iwapo viongozi na wananchi watachangamukia fursa zinazotokana na mradi huo.


Mhariri Khamis Mkotya, (Channel Ten) amesema ndugu zake na yeye ni wanufaika wa moja kwa moja wa fursa za mradi  huo kwani umepita katika Wilaya yao ya  Chemba mkoani Dodoma.


“Huwa nasikitika sana ninaposoma au kusikia  habari zilizopotoshwa juu yua mradi wa EACOP.  Mimi nawajua watu wengi walionufaika na mradi huu. Wapo waliojengewa nyumba bora na kupewa fidia ya fedha pia,” amesema Mkotya.


Aliusifu uongozi wa EACOP kwa kuandaa semina ya  wahariri na kueleza kuwa huo ni mkakati mzuri wa ushirikiano katika kuwasiliana na umma. 


“Wahariri wasipoelewa taarifa inakuwa vigumu kufanya mawasiliano na jamii kupitia vyombo vya habari. Kwa hiyo semina hii imesaidia kutujengea uelewa mkubwa kuhusu mradi huu. Natumaini wa wahariri watakuwa  katika nafasi nzuri ya kuandikia juu ya maendeleo ya mradi huu ili ufanikiwe,” alieleza.


Kwa upande wake Mhariri Selemani Msuya wa (Gazeti la Raia Mwema), amesema utaratibu huo wa EACOP kukutana na waandishi na wahariri utasaidia jamii hasa walioguswa na mradi kupata taarifa sahihi.


"Sisi tunashukuru kwa uamuzi huo ambao umechukua kutukutanisha na nyie, ila nashauri na waandishi waliopo maeneo ya mradi msiwasahau ni watu muhimu kwenye hili mnalofanya. Pia nawaomba ikiwapendeza kutaneni na kundi hili la waandishi wa mitandaoni ni kubwa na lina nguvu sana kwa sasa," amesema.


Mhariri Hafidh Kido, (Taifa Tanzania) amesema semina imewasaidia wahariri kuelewa hatua ya mradi iliyofikiwa hadi sasa.


“Mafunzo haya yamekuwa ya thamini sana kwetu. Yametujengea uwezo na tumefahamu mradi vizuri na maendeleo yake hadi sasa,” amesema Kido na kuzipongeza serikali za Uganda na Tanzania katika kutekeleza mradi huo.

No comments: