MKATABA WA UBORESHAJI MSITU WASITISHWA, DC ATOA WIKI MBILI KUSAINIWA UPYA - MAIPAC MEDIA TANZANIA

Breaking

MAIPAC MEDIA TANZANIA

A Centre for Indigenous and Pastoralists Community Informations




Wednesday 3 July 2024

MKATABA WA UBORESHAJI MSITU WASITISHWA, DC ATOA WIKI MBILI KUSAINIWA UPYA

 





Na Lilian Kasenen,Morogoro 


maipacarusha20@gmail.com


Mkuu wa Wilaya ya Mvomero Judith Nguli amesema Mkataba wa uboreshaji wa maeneo ya msitu wa Kijiji cha Gonja wenye ekari zaidi ya 1900 uliosainiwa kati ya Serikali ya Kijiji hicho na Shirika la PAMS Foundation kutokana na mkataba huo umekiuka taratibu zilizotakiwa kufuatwa.


Akizungumza na wananchi wa kijiji cha Gonja Jana, Nguli alisema Serikali imesikia malalamiko ya wananchi wakidai kugomea mkataba huo kwa sababu makubaliano waliyoafikiana awali yamekiukwa.


Mkuu huyo wa Wilaya alisema alibainisha mapungufu yaliyopo kwenye mkataba huo yakiwemo kutokuwepo kwa ushirikishwaji wa wananchi wakati wa mabadiliko ya fedha kutoka shilingi milioni 180 waliyoahidiwa awali na kupewa shilingi milioni 34, shirika la PAMS halikufanya tathmini ya kina kujua ukubwa wa eneo linalotakiwa kufanyiwa maboresho. Hivyo Mkuu huyo wa Wilaya amesitisha mkataba huo pamoja na shuguli zote kwenye eneo la msitu. 


“Mie niusitishe kwa maana ya kwamba shughuli zote zisimame zisiendelee kwanza," alisema Mkuu wa Wilaya.


Sambamba na hilo, Nguli aliagiza kiasi cha sh milioni 34 zilizolipwa na shirika hilo zisitumike hadi muafaka utakapofikiwa baada ya wiki mbili, pia ametaka wananchi washirikishwe pindi zoezi la tathmini litakapofanyika.


Katika hatua nyingine, Mkuu wa Wilaya amemuagiza Mkurugenzi wa Halmashauri kuwachukulia hatua za kinidhamu kwa waliohusika na usumbufu huo.


Naye, Mwakilishi wa Mkurugenzi wa Shirika la PAMS Foundation Elisifa Ngowi akikiri kuwepo kwa mapungufu katika zoezi la tathmini ya eneo pamoja na ushirikishwaji wa wananchi kwenye mabadiliko ya fedha.


Aidha, alisema shirika hilo linajihusisha na uendelezaji wa maeneo ya misitu iliyoharibiwa kwa kupanda miti ili kurudisha uoto wa asili kama ilivyokuwa awali ambapo katika msitu wa kijiji cha Gonja zaidi ya ekari 300 kati ya 1900 ndizo waliingia mkataba wa kuziendeleza.


Kwa upande wake Afisa Maliasili Mkoa wa Morogoro Joseph Chuwa alisema Mkoa wa Morogoro una misitu ya vijiji 109 ambayo inasifa ya kupata miradi ya uwekezaji wa hewa ya ukaa lengo la uwekezaji huo ni kukabiliana na mabadiliko ya tabia nchi ambayo kwa hivi karibu dunia imeshuhudia athari zake ikiwemo mafuriko, vimbunga na ongezeko la joto.


Chuwa alisema elimu inatakiwa kutolewa kwa wananchi waelewe juu ya umuhimu wa uwekezaji huo..


Kwa mujibu wa Mkataba huo Kijiji cha Gonja kitapata kiasi cha sh milioni 34 kila mwaka kutoka kwa PAMS Foundation kwa kipindi cha miaka 30 ikiwa ni mapato yatokanayo na kukodisha msitu huo.

No comments: