MWANAFUNZI HAJI ANAYETUMUA VIDOLE VYA MIGUU KUANDIKA,KULANAOMBA MSAADA WA KUENDELEA NA MASOMO YA KIDATO VHA TANO - MAIPAC MEDIA TANZANIA

Breaking

MAIPAC MEDIA TANZANIA

A Centre for Indigenous and Pastoralists Community Informations




Friday 5 July 2024

MWANAFUNZI HAJI ANAYETUMUA VIDOLE VYA MIGUU KUANDIKA,KULANAOMBA MSAADA WA KUENDELEA NA MASOMO YA KIDATO VHA TANO

 







Na Lilian Kasenene, Morogoro 


maipacarusha20@gmail.com


Morogoro.Mwanafunzi mwenye ulemavu wa mikono na miguu ameiomba serikali na watu mbalimbali kujitokeza kumsaidia kuenedelea na masomo yake ya kidato cha tano baada ya familia yake kushindwa kumlipia ada


Mwanafunzi huyo Hamisi Haji(21) mkazi wa Mtimbila Wilaya ya Malinyi ambaye anatumia vidole vya miguu kuandika na kufanya shughuli nyingine ameiomba Serikali na wadau mbalimbali kumsaidia kupata fedha kwa ajili ya michango na mahitaji mengine ya shule ili aweze kuendelea na masomo ya kidato cha tano.


Haji ambaye amehitimu kidato nne na kufaulu kuchaguliwa kujiunga na kidato cha tano amekosa matumaini ya kuendelea na masomo yake kwa kile kinachotajwa kuwa ni ukosefu wa fedha na mahitaji muhimu kwani kutokana na familia yake kukosa uwezo wa kugharamia vitu hivyo.


Haji alisema kuwa alizaliwa akiwa na ulemavu wa mikono na miguu ambapo kiungo pekee kinachomsaidia kufanya kazi ndogo ndogo kama kula na kuandika ni miguu yake kwani mikono yake haina uwezo wa kufanya kazi kabisa na kwa sasa anaishi na bibi yake baada ya mama yake mzazi kufariki dunia akiwa darasa la tatu.


"Nilizaliwa na hali ya ulemavu wa mikono na miguu, mikono haifanyi kazi kabisa lakini miguu inanisaidia kufanya kazi ndogondogo ikiwemo kula, kuandika na kazi zingine lakini mikono yangu haiwezi kufanya chochote, kazi zingine kama kuoga, kufua nimekuwa nikisaidiwa hapa nyumbani na mdogo wangu pamoja na bibi," alisema Haji.


Alisema alipokuwa anasoma alikuwa anapata shida kwani shule aliyokuwa anasoma ilikuwa mbali na nyumbani lakini baadae alipofika kidato cha nne alipata msaada wa kuamishwa shule na afisa elimu wilaya na kupelekwa kwenye shule ya wanafunzi wenye uhitaji maalumu Kilosa na kuhitimu kidato cha nne Kwa kupata ufaulu wa divisheni 2 ya kumi na nane.


"Baada ya kufaulu nimechaguliwa kuendelea na kidato cha tano katika shule ya sekondari Liamungo iliyopo mkoani Kilimanjaro na familia yangu haina uwezo wa kunisomesha wala kunisaidia kwa chochote hivyo naiomba Serikali akiwemo Rais Samia Suluhu Hassani aweze kunisaidia pia wadau mbalimbali wajitokeze kunisaidia nikamilishe ndoto zangu za masomo," alisema.


Aidha alisema licha ya changaomoto za kimaisha anazokutana nazo lakini pia anauwezo wa kuchora picha mbalimbali kwa kutumia miguu yake kwani na kwamba alipokuwa shule ya msingi mwalimu wake aligundua kipaji alichonacho na kumsaidia kukikuza hadi sasa anauwezo wa kuchora vizuri.


Caroline Mwanda ni bibi yake Haji amesema hana uwezo wa kufanya kazi kutokana matatizo ya kiafya pamoja na umri alikuwa nao ni mzee tayari hivyo anaiomba jamii kuwapa msaada.


Alisema tegemezi pekee alionalo kwa sasa ni mjukuu wake mmoja aliyeshindwa kuendelea na masomo na kuamua kufanya kazi za ndani ili aweze kuisaida familia yake angalau kwa kiasi kidogo.


“Kwa sasa sina uwezo wa kufanya kazi kulima niliacha muda sana mimi kazi yangu ni kuchota maji yakuoga na kula siwezi kushika jembe nikidondoka na jembe shambani itakuwa nimejitakia mapigo ya moyo yanaenda kasi madaktari wamesema ni Presha mjukuu wangu mmoja ameenda kufanya kazi za ndani kwa watu atusaidie, namuomba mama Samia amsaidie mjukuu wangu sio kwamba anapenda kuomba ila hatuna uwezo," alisema Mwanda.


Mwandishi wa Habari hii alipata nafasi pia ya kuzungumza na mkaguzi msaidizi wa polisi kata ya Mtimbira, mkaguzi msaidizi wa polisi Henry Mwangake alisema alipokuwa katika utekelezaji wa majukumu ya kikazi alikutana na familia ya Haji na katika kuhoji familia yake aligundua kijana huyo anaulemavu wa viungo lakini pia anaishi kwenye familia ambayo aina uwezo wa kifedha hivyo anawaomba watanzania kumchangia kijana huyo ili aweze kujikimu maitaji yake pamoja na kujiendeleza kimasomo.


“Nilipokutana na familia ya Haji na kuwahoji licha ya kijana huyu kuwa na ulemavu wa viungo lakini niligundua kuwa familia hiyo haina uwezo wa kifedha na pia niligundua kuna mwanafunzi ambae amekatisha masomo yake ili aweze kuisaidia familia yake, niwaombe watanzania kwa ujumla kujitokeza na kumchangia ili aweze kuendelea na masomo lakini apate angalau hela ya kujikimu kimaisha” alisema mkaguzi Mwakate.


Mwisho.

No comments: