Chakula kwa wanafunzi chaongeza ufaulu Meatu - MAIPAC MEDIA TANZANIA

Breaking

MAIPAC MEDIA TANZANIA

A Centre for Indigenous and Pastoralists Community Informations




Friday, 18 October 2024

Chakula kwa wanafunzi chaongeza ufaulu Meatu

 


Mkuu wa wilaya ya Meatu Fauzia Ngatumbura akizungumza na waandishi wa habari

Mkuu wilaya MeatuFauzia Mgatumbura akisalimiana na mwandishi wa habari hizi

Meneja miradi ya Maendeleo ya Jamii ya Taasisi  Friedkin  Tanzania Aurelia Mtui akigawa chakula kwa wanafunzi shule ya msingi Makao


Na: Mussa Juma, Maipac 


maipacarusha20@gmail.com 


Ufaulu umeongezeka kwa wanafunzi wilayani Meatu mkoa wa Simiyu kutokana na wanafunzi wengi kuanza kupata chakula Cha mchana shuleni.


Chakula hicho katika shule kimekuwa kikitolewa bure na kampuni ya Utalii ya Mwiba Holdings ltd ambayo imewekeza katika wilaya hiyo na katika shule nyingine kinachangiwa na wazazi.


Akizungumza na waandishi wa habari mkuu wa wilaya ya Meatu, Fauzia Ngatumbura, alisema tangu chakula kianze kutolewa mashuleni pia utoro umepungua mashuleni.


"Tunawashukuru sana wahisani wetu Mwiba holdings kwa kutoa bure chakula katika eneo la makao lakini pia tunawashukuru sana wazazi ambao nao wanachangia chakula maeneo mengine"alisema.


Wakizungumzia upatikanaji wa chakula shuleni, baadhi ya wanafunzi, Wazazi na Walimu wilayani Simiyu,walipongeza kampuni ya Utalii ya Mwiba kwa kutoa bure chakula lakini pia na wazazi wanachangia.


Mwalimu Mkuu wa shule ya msingi, Mshikamano B wilayani Meatu, Zuhura Ntandu alisema tangu chakula kianze kutolewa shuleni ufaulu unaongezeka na utoro umepungua sana.


"Wanafunzi wanasoma kwa utulivu, hawatoroki shule kutokana njaa   lakini pia usikivu umeongezeka darasani "alisema


Alisema katika shule hiyo, wanafunzi 427 kati ya wanafunzi 1022 wanapata chakula shuleni na wanaimani idadi itaongezeka.


Mwalimu Ntandu hata hivyo,aliomba wahisani na kampuni nyingine kujitokeza kusaidia kutoa chakula Cha bure mashuleni kama inavyofanya kampuni ya Mwiba.


Mzazi Rameki Mboje wa eneo la Machinjioni wilayani Meatu alisema amekuwa akichangia chakula Cha Mtoto wake na kuomba wazazi wajitokeze kwa wingi ikichangia.


"Sisi katika shule yetu hakuna mfadhili kama wenzetu wa Makao, lakini tunachangia chakula nauelewa wa watoto umeongezeka"alisema


Mwanafuzi wa shule ya msingi Mshikamano Leah Silasi alisema chakula kinachotolewa shuleni kumesaidia wanafunzi kufanya vizuri katika mitihani kwani wanakuwa watulivu darasani.


Wanafunzi wote  856 wa shule ya Msingi Makao, wilayani Meatu, wamekuwa wakipata chakula Cha bure Kila siku kupitia  mradi  unaofadhiliwa na Taasisi ya Friedkin Conservation Fund kupitia  kampuni yake ya  Mwiba Holdings LTD ambapo kila mwezi wanatoa kiasi sh 20.5 milioni.


Meneja wa miradi ya Maendeleo ya Jamii wa Friedkin Tanzania, Aurelia Mtui  alisema pia wamejenga jiko la kisasa kwa ajili ya shule hiyo kwa gharama ya sh 28.1 milioni na mradi wa uvunaji Maji ya mvua  uliogharimu sh 30.8 milioni 




No comments: