Na Mwandishi wetu, Mirerani
maipacarusha20@gmail.com
BENKI ya CRDB Tawi la Mirerani Wilayani Simanjiro Mkoani Manyara, imesherehekea wiki ya huduma kwa wateja duniani kwa kukutana na wadau mbalimbali wa eneo hilo.
Meneja wa CRDB Tawi la Mirerani, Renatus Rutajama amesema lengo ni kukutana na wateja wao, kusikiliza maoni yao na kubadilishana mawazo juu ya utendaji kazi unavyoendelea katika eneo hilo.
"Hii ni wiki ya huduma kwa wateja duniani nasi CRDB Tawi la Mirerani tumeungana na wateja wetu kupata kifungua kinywa na kuzungumza mawili matatu ya kuboresha huduma zetu kwao," amesema.
Afisa mwingine wa benki ya CRDB Tawi la Mirerani, Adam Mgava amewaasa wafanyabishara wa eneo hilo kuiga jambo hilo zuri kwa kukutana na kujumuika na baadhi ya wateja wao ili kuongeza tija.
"Pia tuwe na utamaduni wa kupokea changamoto na mapungufu tuliyonayo ili tuweze kupiga hatua zaidi kwani watu wengi wana tabia ya kupenda kupongezwa bila kutambua madhaifu yakielezwa kwao yanawajenga," amesema Mgaza.
Katibu wa Bakwata Wilaya ya Simanjiro, Nuru Mkireri ameipongeza CRDB kwa kuanzisha akaunti isiyo na riba kwani itaongeza wateja wenye imani na wasiopendelea kuweka riba.
Hata hivyo, Mkireri ametoa wito kwa CRDB kuongeza wigo wa huduma zao hasa maeneo na sehemu za vijiji ili huduma za fedha ziweze kupatikana.
Mkurugenzi wa Ngabomoa, Gasper Swai amepongeza maboresho yaliyofanyika ikiwemo kupunguza makaratasi mengi na kuondokana na foleni.
Swai ametoa ombi la huduma ya kutoa fedha kupitia Sim bank kuongeza fedha kwani kiasi cha shilingi milioni 8 kwa siku ni kidogo mno.
Mwenyekiti Mwenye wa Nyanza group, Kija Malimi amesema elimu ya fedha inapaswa kuendelea kutolewa kwa wachimbaji madini ya Tanzanite ili wapate uelewa zaidi na umuhimu wa kuhifadhi fedha benki.
Afisa mtendaji mkuu TEO wa mamlaka ya mji mdogo wa Mirerani, Isack Mgaya amepongeza kitendo cha benki ya CRDB kukutana na wateja wao ili kusikiliza maoni yao.
MWISHO
No comments:
Post a Comment