DC LULANDALA AWAONGOZA WANA SIMANJIRO KUMUENZI BABA WA TAIFA HAYATI NYERERE - MAIPAC MEDIA TANZANIA

Breaking

MAIPAC MEDIA TANZANIA

A Centre for Indigenous and Pastoralists Community Informations




Monday, 14 October 2024

DC LULANDALA AWAONGOZA WANA SIMANJIRO KUMUENZI BABA WA TAIFA HAYATI NYERERE

 



Na Mwandishi wetu, Mirerani 


maipacarusha20@gmail.com 


MKUU wa Wilaya ya Simanjiro Mkoani Manyara, Mwalimu Fakii Raphael Lulandala amewaongoza wakazi wa eneo hilo kwenye maadhimisho ya miaka 25 ya kifo cha Baba wa Taifa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere kwa kuitaka jamii kuenzi kwa vitendo falsafa, amani na fikra alizoziacha.


Lulandala akizungumza Oktoba 14 mwaka 2024 kwenye viwanja vya Mnyalu Complex mji mdogo wa Mirerani amesema hivi sasa watanzania wanaendelea kuishi kwa amani na kupendana bila kuulizana kabila wala maeneo waliyotoka.


"Hii ni tunu tuliyoachiwa na Baba wa Taifa hivyo tuendee kuienzi huku tukiiunga mkono serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Rais Samia Suluhu Hassan," amesema Lulandala.


Hata hivyo, amewaasa wananchi wa eneo hilo kujiandikisha katika orodha ya daftari la makazi ili waweze kushiriki uchaguzi wa serikali za mitaa iliyoanza Oktoba 11 hadi 20 mwaka 2024.


Katibu Tawala DAS wa Wilaya ya Simanjiro, Warda Maulid Abeid amesema pia kulifanyika bonanza la Nyerere day na lengo kubwa la kuhamasisha wananchi kujiandikisha kupiga kura.


Amesema bonanza lilifanyika katika Uwanja Mnyalu complex mji mdogo wa Mirerani, ambapo lilianza asubuhi saa 06:30 mpaka saa 08:00 kukimbia mbio fupi kuanzia uwanja wa Mnyalu mpaka geti la Magu na kurudi.


"Njia itakayotumika kwenda tutapita Manyara Inn uelekeo wa kwenda Kia kupita rafu road  kuzunguka geti la Magu na kurudi na kipande cha lami mpaka geti la mbuzi na mwisho tunamalizia uwanjani Mnyalu complex," amesema Warda.


Amesema pia walivuta kamba, kukimbia na magunia, kukimbiza kuku, mpira wa miguu, rede, kukuna nazi, tumealika timu sita kutoka mikoa mitatu ya Manyara, Arusha na Kilimanjaro.


"Timu hizo ni Tanzanite veteran ya Mirerani, Kia veterani, Old boys veterani ya Arusha, Watumishi Hai veterani ya Boma, Ushirikaa veterani ya Moshi, Siha veterani ya Sanya juu, Tanzanite sports Acadamy ya Mirerani na Old boys FC ya Arusha," amesema Warda.


Amesema zawadi mbalimbali zitatolewa kwa washindi ikiwa ni siku ya kumuenzi hayati Baba wa Taifa na siku ya kuhamasisha chaguzi za Serikali  za mitaa.


MWISHO

No comments: