Na Mwandishi wetu, Simanjiro
maipacarusha20@gmail.com
MKUU wa shule ya sekondari ya kidato cha sita ya Naisinyai Wilayani Simanjiro Mkoani Manyara, mwalimu Mbayani Kivuyo amemshukuru Rais Samia Suluhu Hassan kwa kufanikisha miradi ya maendeleo shuleni hapo ya thamani ya shilingi milioni 904.
Mwalimu Kivuyo akizungumza kwenye mahafali ya 14 ya kuhitimu kidato cha nne kwa wanafunzi wa shule hiyo ambayo hivi sasa pia ina wanafunzi kidato cha tano na cha sita amesema imepiga hatua.
Amesema Rais Samia ameipatia shule hiyo zaidi ya shilingi milioni 904 kwa ajili ya ujenzi wa miundombinu mbalimbali katika taasisi hiyo ambayo hivi sasa imeboreshwa zaidi.
"Rais Samia ni mama wa kipee kabisa kwani ameiangalia shule ya sekondari Naisinyai kwa jicho la kipekee na kutoa fedha hizo ambazo zimejenga majengo mbalimbali ambayo yamekamilika kwa asilimia kubwa," amesema mwalimu Kivuyo.
Ametaja majengo yaliyojengwa kupitia fedha hizo ni mabweni matano, vyumba tisa vya madarasa na matundu 14 ya vyoo hivyo kwa kiasi kikubwa kupunguza changamoto ya mahitaji hayo.
Amesema shule hiyo ilianzishwa mwaka 2006 ikiwa ya kidato cha kwanza hadi cha nne ikiwa na wanafunzi 93 kati yao wavulana 53 na wasichana 40 mkuu wa shule akiwa Emmanuel Kirenga.
Amesema mwaka 2021 shule hiyo ilipanda hadhi kwa kupokea wanafunzi wa kidato cha tano kwa mchepuo wa sanaa tahasusi ya HGK ya masomo ya historia, jiografia na kiswahili ikiwa na jumla ya wanafunzi 957.
"Tumefanikiwa kuongezewa idadi ya walimu kutoka 25 hadi 30 ili kukidhi hitaji la walimu katika shule yetu na tumejenga jiko banifu la kisasa ambalo linatumia kuni kidogo sana," amesema mwalimu Kivuyo.
Amesema wamefanikiwa kupata matokeo mazuri ya kidato cha sita mwaka 2024 ambapo ufaulu wao ni wa daraja la kwanza, la pili na la tatu mwanafunzi mmoja tuu hivyo kushika nafasi ya kwanza kiwilaya.
Amesema wamefanikiwa kuanzisha maabara ya kompyuta kupitia msaada wa shirika lisilo la kiserikali la Tanzania Enlightment Development Innovation (TEDI) wa kompyuta 10 na server moja zinazowasaidia wanafunzi kujifunza masomo kwa ufanisi kutokana na ukuaji wa sayansi na teknolojia.
"Tumefanikiwa kuendelea kuboresha mazingira kwa kupanda miti 1,000 katika mazingira ya shule kutoka Mali Hai club Moshi mkoani Kilimanjaro," amesema.
MWISHO
No comments:
Post a Comment