Na Epifania Magingo,Manyara
maipacarusha20@gmail.com
Serikali imekabidhi gari yenye thamani ya Zaidi ya Shilingi milioni 200 kwa Mamlaka ya Maji safi na Usafi wa Mazingira Vijijini (RUWASA) ambayo itatumika kwenye Halmashauri ya Wilaya ya Kiteto Mkoani Manyara.
Gari hiyo imekabidhiwa RUWASA na Mkuu wa Mkoa wa Manyara Queen Sendiga ikiwa na lengo mahususi ya kusaidia shughuli za kiutendaji katika idara hiyo ili kufanikisha utoaji huduma kwa wananchi wa Wilaya ya Kiteto na maeneo jirani kwa wakati.
Akizungumza wakati wa makabidhiano ya gari hilo Meneja wa RUWASA Wilaya ya Kiteto Mhandisi Stefano Mbaruku amesema jiografia ya wilaya kiteto imesambaa na hivyo ikikosa vitendea kazi inaleta ugumu wa kutoa huduma kwa wakati.
"Kwakua tumepata kitendea kazi kwasasa ni budi kutoa huduma kwa wakati maana hatuna Tena kisingizio, kwakua kuna usafiri tutafika maeneo yetu kwa wakati kuwahudumia wananchi wa Wilaya yetu ya Kiteto". Alisema
Aidha, Meneja wa RUWASA Mkoa wa Manyara Mhandisi James Kionaumela amesema kwa miradi inayoendelea Mkoa wa Manyara unategemea kufikia lengo la Taifa kutoa huduma ya maji kwa maeneo ya Vijijini kwa asilimia 85 huku mjini ikiwa asilimia 95.
"Kila Wilaya ina miradi,tuna miradi 19 inaendelea kwa hiyo miradi hiyo wakandarasi wako saiti tutaendelea nao na tutaendelea kulinda ule upatikanaji wa Maji kuna vyombo vya utaoji maji ngazi ya Jamii vinaitwa SIBIUSO kwa hiyo wanaendelea pia kusimamia miradi".
Amesema, uendashaji wa miradi unahitaji uangalizi mkubwa huku akibainisha kwamba katika Wilaya ya Kiteto gari hilo ambalo limetolewa litasaidia kuondoa changamoto ya usafiri katika utoaji huduma.
Katika kukabidhi gari hilo Mkuu wa Mkoa wa Manyara Queen Sendiga amesema Serikali imetoa gari hilo ili kuongeza nguvu katika kitengo Cha maji kuhakikisha wananchi wa kiteto wanapata huduma ya Mji safi na salama.
"Viongozi wote wa kiteto wako hapa watachukua gari Yao, niwaombe kuchukua tahadhari tunapokwenda kipindi Cha mvua, maana tulipoteza gari na tumepata gari tumepoteza mtu na hatujapata mtu kwa hiyo tuchukue tahadhari katika kipindi hiki Cha mvua tuangalie maeneo tunayopita kwa uangalifu".
Hata hivyo Sendiga ameishukuru Serikali kwa kuongeza nguvu katika sekta ya maji na kufanya maboresho mbalimbali huku akitoa msisitizo kwa watumishi kuchukua tahadhari wakati wa kutoa huduma kwa wananchi ili kuyafikia malengo ya Taifa yaliyopangwa.
No comments:
Post a Comment